Jumatatu tarehe 7 Mei 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 20 Shaabani 1439 Hijria sawa na Mei 7, 2018.
Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mei 1888, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilianzisha uvamizi katika ardhi ya Zimbabwe ya sasa. Mipango ya kuikalia kwa mabavu Zimbabwe ilibuniwa na mwanasiasa na mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina la Cecile Rhodes, ambaye aliasisi shirika la Afrika Kusini la Kiingereza nchini humo. Kwa kusaidiwa na jeshi la Uingereza, Rhodes aliuwa kwa umati maelfu ya raia wazalendo na kuwakamata mateka wengine wengi, na hivyo kuweza kuidhibiti ardhi yote ya Zimbabwe na kuipachika jina lake la Rhodesia.
Miaka 210 iliyopita katika siku kama ya leo wananchi wa Uhispania walianzisha harakati dhidi ya vikosi vya jeshi la Mfalme Napoleon wa Ufaransa, vilivyokuwa vinakalia kwa mabavu nchi yao. Wakati huo Uhispania pia ilikuwa ikihesabiwa kuwa moja ya makoloni makubwa ya Ulaya na ilikuwa ikikalia kwa mabavu ardhi nyingi nje ya bara hilo. Lakini wananchi wa Uhispania walikuwa wameonja uchungu wa nchi yao kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya kigeni. Baada ya miaka mitano ya mapambano dhidi ya vikosi vamizi vya Ufaransa, walifanikiwa kuvifukuza vikosi hivyo mwezi Disemba mwaka 1813 kutoka nchini kwao. Wakati huo huo kutokana na kushindwa katika Amerika ya Kusini, Uhispania ililazimika kuziacha huru nchi kadhaa ilizokuwa ikizikoloni.
Na siku kama ya leo miaka 1054 iliyopita alifariki dunia Ibn Nadim mpokezi hadithi na mtaalamu wa vitabu wa Kiislamu aliyekuwa na umashuhuri katika zama zake hizo. Ibn Nadim alijulikana sana kutokana na kitabu chake maarufu kwa jina la "Al Feherest". Ndani ya kitabu hicho msomi huyo wa Kiislamu aliarifisha sayansi zote za kisasa katika utamaduni wa Kiislamu wa zama hizo na baadaye akasherehesha maisha ya wasomi watajika katika uwanja wa sayansi hizo.