May 10, 2018 00:11 UTC
  • Alkhamisi, Mei 10, 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Sha'ban 1439 Hijria inayosadifiana na tarehe 10 Mei, 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1135 iliyopita, alifariki dunia Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh, maarufu kwa lakabu ya Nasser Kabir, alimu na mwanamapambano mkubwa miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Alizaliwa mwaka 230 Hijiria mjini Madina, na baada ya watawala wa Bani Abbas kuwaua na kuwabaidisha watu wa familia ya Mtume akiwemo Imamu Hassan Askari (as), Ali Atroosh alipelekwa mjini Samarra, kaskazini mwa mji wa Baghdad, Iraq kwa amri ya watawala hao ikiwa ni baada ya baba yake kubaidishwa mjini hapo. Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh alijifunza elimu ya dini mjini Baghdad na Kufa na kutokea kuwa msomi mkubwa huku akitabahari pia katika uwanja wa mashairi. Mbali na hayo alijihusisha na harakati za kisiasa ambapo katika kipindi cha mwamko wa Maalawi mjini Tabarestan, kaskazini mwa Iran, Atroosh alikimbilia katika eneo hilo. Baada ya kuanguka utawala huo, aliufufua huku akitawala sehemu kubwa ya maeneo ya kaskazini mwa Iran kwa uadilifu na usawa, sambamba na kueneza mafundisho ya dini ya Mtume Muhammad (saw). Katika harakati zake alifanikiwa kuwaingiza maelfu ya watu katika dini ya Uislamu. Vitabu vya 'Al-Bisat' 'Tafsir al-Utrush' na 'Imamatul-Kabir ni miongoni mwa makumi ya vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo.

Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh, maarufu kwa lakabu ya Nasser Kabir

Siku kama ya leo miaka 706 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Hussein bin Abdallah Tayyebi aliyekuwa na lakabu ya Sharafud-Deen, mpokezi wa hadithi na mwanafasihi mkubwa wa karne ya nane Hijiria. Abdallah Tayyebi alibobea katika elimu za fasihi ya lugha ya Kiarabu na alihesabiwa kuwa miongoni mwa shakhsia wakubwa na wasomi katika zama zake. Aidha alimu huyo alikuwa akitilia mkazo juu ya kufundisha tafsiri ya Qur'ani pamoja na hadithi. Vitabu vya 'Tafsirul-Qur'an' na 'Meshkat' ni miongoni mwa vitabu alivyoandika

Hussein bin Abdallah Tayyebi

Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita alizaliwa François-Marie Raoult, mwanakemia wa Ufaransa. Baada ya kuhitimu masomo yake katika hatua ya PHD katika Chuo Kikuu cha mjini Paris, alipanua wigo wa utafiti wake wa kielimu. Baada ya hapo alifanikiwa kuwa mmoja wa waasisi wapya wa elimu ya kemia na fizikia. François-Marie Raoult alifanikiwa pia kubuni nadharia zake katika uwanja huo.

François-Marie Raoult, mwanakemia wa Ufaransa

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita alifariki dunia alimu mkubwa wa kidini Ayatullah Muhammad Kuhestani Behshahr. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi eneo alikozaliwa, Ayatullah Kuhestani Behshahr alielekea mjini Najaf, Iraq na kushiriki darsa za wasomi wakubwa kama vile Ayatullah Mirza Naini na Sayyid Abul-Hassan Isfahani. Baada ya kupanda kielimu na kufikia hatua ya ijtihad, alirejea mjini Kuhestan na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji na kuwaelekeza watu. Katika harakati yake hiyo alifanikiwa kujenga shule kadhaa huku akilea wanafunzi kupitia masomo ya kidini. Ayatullah Muhammad Kuhestani Behshahr alifariki duani tarehe 14 Rabiul-Awwal 1391 Hijiria kutokana na maradhi ya moyo.

Na siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, kundi linalopigania uhuru wa Sahara Magharibi liliasisi Harakati ya Kupigania Uhuru ya Polisario. Harakati hiyo ilikaribishwa na wakazi wa eneo hilo na ikaanzisha mapambano dhidi ya wakoloni wa Kihispania hadi wakoloni hao walipoondoka Sahara mwaka 1975. Hata hivyo serikali ya Uhispania ilikabidhi mamlaka ya eneo hilo kwa serikali za Morocco na Mauritania. Mauritania ililazimika kuondoka Sahara Magharibi kutokana na mapambano makali ya Polisario na hali mbaya ya ndani ya nchi hiyo. Morocco iliendelea kukabiliana na wapigania uhuru wa Polisario hadi mwaka 1991 ambapo mapigano kati ya pande hizo mbili yalisitishwa chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa. Eneo hilo lingali linakaliwa na Morocco.

Bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahara Magharibi