May 18, 2018 23:46 UTC
  • Jumamosi, Mei 19, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 3 Ramadhani 1439 Hijria mwafaka na tarehe 19 Mei 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1026 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Muhammad bin Nu'man mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na mwanafaqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na kisha kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Miongoni mwa harakati za kifikra na kiutamaduni za Sheikh Mufid ilikuwa ni kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu mbalimbali vyenye thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usuulul Fiqh. ***

Sheikh Mufid

Katika siku kama ya leo miaka 872 iliyopita aliaga dunia Ibn Khashhab mhakiki na mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria. Alizaliwa mwaka 492 Hijria huko Iraq na kuanza kujifunza masomo ya zama hizo tangu akiwa mdogo. Ibn Kashshab hatua kwa hatua alijifunza masomo ya mantiki, hadithi na uandishi na kuanza kuandika vitabu mbalimbali katika nyanja hizo. Ibn Khashshab alikuwa shakhsiya wa aina yake na ndio maana akafahamika sana kwa jina la Allamah. Aidha alitajwa kama bwana wa maqarii wa zama zake kutokana na umahiri wake katika kusoma na kufahamu vyema Qur'ani Tukufu. ***

Miaka 497 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya utawala wa kifalme wa Othmania yaliuteka mji muhimu wa Belgrade, uliokuwa mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani. Mwishoni mwa karne ya 14 Miladia Utawala wa Othmania ulianza kusonga mbele katika eneo la Balkan na kuweza kulitawala karibu eneo lote hilo. Miaka 20 baadaye yaani mwaka 1541 utawala huo uliweza kuyadhibiti maeneo ya Hungary.***

Utawala wa Othmania kabla ya kugawanywa

Siku kama ya leo miaka 256 iliyopita, alizaliwa katika familia masikini Johann Gottlieb Fichte mwanafalsafa wa Kijerumani. Johann alikuwa mmoja wa waasisi wakuu wa harakati ya kifalsafa iliyojulikana kama "German Idealism", harakati ambayo ilitokana na maandiko ya kinadharia na kimaadili ya rafiki yake Immanuel Kant. Johann Gottlieb Fitche aliathiriwa sana kinadharia na mwanafalsafa mwenzake huyo na kumkabidhi baadhi ya kazi zake. Johann Fitche ameandika vitabu vingi muhimu ambapo baadhi ni vile alivyovipa majina kama vile" Foundations of Nature Right, Mustakabali wa Binadamu na makala ya The Way Towards the Blessed Life.***

Johann Gottlieb Fichte

Miaka 93 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Malcolm X, kiongozi wa harakati za kupigania uhuru Wamarekani wenye asili ya Afrika. Malcolm X alizaliwa katika familia masikitini nchini humo na akiwa na umri wa miaka minne, alishuhudia kijiji chao kikiteketezwa moto na watu wa jamii ya Ku Klux Klan kutokana na mashambulizi ya kibaguzi. Baadaye alienda kujiunga na shule ya kutwa hata hivyo akiwa na umri wa miaka 15 hakuweza kukamilisha masomo yake kutokana na umasikini, hivyo akalazimika kufanya kazi katika mgahawa mmoja ambapo alijikuta akijiunga na utumiaji wa madawa ya kulevya na unyang’anyi. Kufuatia hali hiyo akiwa na umri wa miaka 21 alihukumiwa kifungo cha miaka  mitano jela kutokana na hali hiyo. Akiwa jela alifahamiana na wafungwa wengi wenye asili ya Kiafrika waliotokana na familia za Kiislamu kama ambavyo pia alikuwa na mahusiano na Elijah Muhammad, kiongozi wa harakati ya siri ya Wamarekani weusi. Mahusiano na kiongozi huyo yaliendelea hata baada ya Malcolm X kutoka jela. Baada ya hapo alianza kusoma na kufanya utafiti mwingi kuhusiana na Uislamu ambapo kwa msaada wa Waislamu alifanikiwa kujenga misikiti miwili katika mji wa Detroit, Philadelphia nchini Marekani. ***

Malcolm X

Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, Thomas Edward Lawrence mwanasiasa na afisa wa ujasusi wa Uingereza alipoteza maisha yake katika ajali ya gari. Lawrence alizaliwa mwaka 1888 Miladia. Katika kipindi cha miaka kati ya 1910 hadi 1914, mwanasiasa huyo wa Uingereza aliwakilisha kamati ya masuala ya akiolojia (elimu kale) na pia kuhudumu huko Iraq, Syria na Palestina. Aidha alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na mwaka 1916 aliteuliwa kuwa mkuu wa idara ya ujasusi ya jeshi la Uingereza nchini Misri. Thomas Edward Lawrence alichangia pakubwa kuingia madarakani kwa wafalme Fadhil huko Syria, Abdallah nchini Jordan na Mfalme Abdulaziz huko Saudi Arabia.***

Thomas Edward Lawrence

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, rada ilivumbuliwa na Robert Watson Watt mvumbuzi wa Kiingereza. Kifaa hicho ambacho ni muhimu kinachotumiwa katika ugunduzi na utambuzi kwenye oparesheni mbalimbali za kijeshi na kiraia, kwa mara ya kwanza kilitumika katika moja ya viwanja vya ndege vya Uingereza. Rada ilihesabiwa kama chombo muhimu cha kutoa tahadhari katika Vita vya Pili vya Dunia na hivi sasa kinatumika katika masuala mbalimbali. ***

Robert Watson Watt

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, watu 90 wa familia ya Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim walitiwa mbaroni huko Iraq na kunyongwa baada ya siku sita. Jinai hiyo ilikuwa ni mwendelezo wa utawa wa dikteta Saddam wa kukandamiza aina yoyote ile ya harakati ya kukabiliana na utawala huo. Muda mchache baada ya tukio hilo, watu wengine 10 wa familia hiyo ya Ayatullah Muhsin Hakim walinyongwa. Ayatullah al-Udhma Hakim alikuwa mmoja wa marjaa taqlidi wakubwa nchini Iraq. Watoto wake na watu wengine wa familia ya Hakim waliondokea kuwa watu wa elimu na maarifa.***

Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim

Na miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, Allama Muhammad Taqi Shushtari aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 93 baada ya kuishi maisha yaliyojaa harakati ya kueneza elimu.  Muhammad Taqi Shushtari alizaliwa katika familia ya elimu na wanamapambano na akitumia akili na kipaji cvha hali ya juu alichokuwa nacho, alifanikiwa kukwea haraka daraja za kielimu. Aliondoka nchini Iran na kuelekea Iraq akiwa na umri wa miaka 32 akilalamikia marufuku ya Hijabu iliyotangazwa na Reza Shah mfalme wa wakati huo wa Iran. ***

Allama Muhammad Taqi Shushtari