May 21, 2018 22:03 UTC
  • Jumanne, Mei 22, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 6 Ramadhani 1439 Hijria sawa na tarehe 22 Mei 2018 Milaadia

Tarehe Mosi Khordad kwa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia ni tarehe ya kukumbuka siku ya kuzaliwa Sadruddin Muhammad Qiwam Shirazi maarufu kwa jina la Mulla Sadra. Ṣadr ad-Dīn Muḥammad Shīrāzī maarufu kwa jina la Sadr-ol-Mote'allehin au Mulla Sadra alizaliwa mwezi 9 Mfunguo Nane mwaka 980 Hijria mjini Shiraz Iran. Msingi wa kielimu na kimaadili wa Mulla Sadra uliwekwa na Sheikh Bahai, alimu wa aina yake wa kipindi cha watala wa Kisafawi nchini Iran na baadaye mwanachuoni huyo mkubwa alipata malezi ya mwanachuoni mwingine mkubwa Mirdamad. Mulla Sadra alichota elimu za wapokezi wa hadithi, fikihi na usuli kutoka kwa Sheikh Bahai huku elimu za falsafa, akida, irfan na elimu nyinginezo akizichota kwa Mirdamad. Amma elimu nyingine kuhusu maumbile, hisabati, nujumi na nyota  alitabahari nazo kupitia kwa Hakim Abul Qasim Mir Fendereski, mmoja wa maulamaa wakubwa wa zama zake. Mulla Sadra ametoa mchango mkubwa sana kwa falsafa ya Kiislamu. Mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu amevirithisha vizazi vya baada yake zaidi ya vitabu 40 huku kitabu cha al Asfar al Arba'a kikiwa maarufu zaidi kuliko vitabu vyake vingine. Mwanafasafa na mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 1050 Hijria mjini Basra Iraq akiwa na umri wa miaka 70 na alizikwa katika mji huo huo.

Mulla Sadra

 

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita yaani tarehe 22 Mei 1980 Milaadia, vilianza vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Marekani ambayo ilipoteza kibaraka wake wake mkubwa nchini Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu iliamua kuwaweka chini ya mashinikizo makubwa wananchi Waislamu na wanamapambano wa Iran na pia kujaribu kuulazimisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ukubali kuburuzwa kwenye mazungumzo ya kudhalilishwa na Marekani. Baada ya Marekani kuchukua uamuzi huo, Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza wazi kuwa uchumi na maisha ya mataifa ya dunia hayamo mikononi mwa madola ya kibeberu na kuwatoa wasiwasi wananchi wa Iran kwa kuwaambia: Msiogopeshwe hata kidogo na mashinikizo hayo ya kiuchumi kwani iwapo watatuwekea vikwazo vya kiuchumi watakuwa wametupa fursa ya sisi wenyewe kujitegemea kiuchumi. Watu wanaoogopeshwa na vikwazo vya kiuchumi ni wale wanaoona kuwa uchumi ndio msingi wa kila kitu na dunia ndio mwanzo na mwisho wao.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara kukabiliana na vikwazo 

 

Miaka 133 iliyopita katika siku kama ya leo, mwaka 1885 Milaadia, aliaga dunia Victor Hugo mwandishi na malenga mashuhuri wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83. Hugo alikuwa muungaji mkono mkuu wa mabadiliko kwa maslahi ya matabaka ya wanyonge na masikini nchini humo. Victor Hugo alijitumbukiza kwenye uwanja wa kisiasa akiwa na umri wa miaka 25 na kufanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge. Lakini ulipofika wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu alilazimishwa kuacha siasa na kubaidishwa kwa muda wa miaka 20 baada ya kupinga siasa za dikteta Napoleon wa Tatu. Umaarufu mkubwa wa Victor Hugo ulitokana na uandishi wake hata inasemekana kuwa yenye ndiye mwanzilishi wa Romanticism, kwani wakati wake namna hiyo ya uandishi ilipata nguvu sana. Miongoni mwa vitabu maarufu vya mwandishi huyo wa Ufaransa ni Les Misérables, The Hunchback of Notre-Dame, The Man Who Laughs na Toilers of the Sea. 

Victor Hugo