May 24, 2018 22:47 UTC
  • Ijumaa, Mei 25, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 9 Ramadhani, mwaka 1439 Hijria inayosadifiana na tarehe 25 Mei, mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo, miaka 658 iliyopita, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1360:

Kundi la mabaharia wa Kifraransa liligundua Ghuba ya Guinea. Ghuba ya Guinea iko magharaibi mwa bara la Afrika katika bahari ya Atlantiki. Baada ya muda kupita tangu kugunduliwa Ghuba ya Guinea, ushawishi wa Ufaransa ndani ya bara hilo ulianza, na taratibu ikaanza kuidhibiti ardhi iliyokuja kujulikana baadaye kama Guinea. Nchi ya Guinea iliendesha harakati za mapambano ya miaka mingi mpaka ikafanikiwa kupata uhuru wake mwaka 1958. Guinea ina eneo lenye ukubwa wa kilomitamraba zaidi 245,000 na imepakana na nchi za Senegal, Guinea Bissau, Mali, Ivory Coast, Liberia na Sierra Leone. 

Miaka 586 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 6 Ramadhani mwaka 853 Hijria:

Aliaga dunia Ulugh Beg, mwanasayansi mtajika wa elimu ya Unajimu. Alizaliwa mwaka 796 Hijria huko Sultaniyeh Zanjan, moja ya miji ya magharibi mwa Iran na akalelewa na kukulia kwenye kasri la babu yake Taimur, mwasisi wa ufalme wa kizazi cha Wataimur. Alipofikia umri wa miaka 16, Ulugh Beg aliteuliwa kuwa mtawala wa Mā warāʼ an-Nahr au Transoxiana, eneo la Asia ya Kati ambalo wakati huo lilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Kinyume na Taimur, Ulugh Beg hakupendelea kufuata sera ya kutuma majeshi kwa ajili ya kuhodhi ardhi zaidi, bali alijishughulisha zaidi na kazi za uhakiki na utafiti. Aliasisi Madrasah kwa ajili ya kustawisha elimu, ambapo somo la Unajimu (Astrology) ndilo alilolipa kipaumbele cha kwanza. Hatua nyingine muhimu aliyochukua Ulugh Beg ilikuwa ni kuanzisha Kituo cha Kuangalilia nyota (Observatory) cha jengo la ghorofa tatu katika mwaka 828 Hijria huko katika mji wa Samarkand. Kituo hicho kiliasisiwa kwa msaada mkubwa wa Ghiyathuddin Jamshidi-e-Kashani, mwanahisabati na mnajimu wa zama hizo za Ulugh Beg. Miongoni mwa mafanikio muhimu ya harakati za kielimu za Ulugh Beg ni jedwali la mahesabu ya kalenda na hali ya nyota pamoja na fani za hisabati zinazohusiana na Unajimu ikiwemo Trigonometria (Trigonometry) na Jiometria Mviringo (Spherical Geometry).

Ulugh Beg

Miaka 126 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1892:

Alizaliwa Josip Broz Tito, kiongozi wa zamani wa Yugoslavia, huko katika eneo la Hrvatsko Zagorje, kaskazini mwa Zagreb, mji mkuu wa Croatia. Mnamo mwaka 1915, wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Tito alikamatwa katika medani ya vita dhidi ya Urusi; na baada ya kuachiwa huru aliungana na Wakomunisti kupamaba na utawala wa Tsar. Tito aliasisi harakati ya ukombozi wa taifa baada ya Ujerumani  kuishambulia Yugoslavia wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Mnamo mwaka 1943 alipewa hadhi ya Jemadari (Marshal), mwaka 1953 akawa Mkuu wa Baraza la Utendaji wa Shirikisho na Kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Yugoslavia na hatimaye mwaka 1974, Josip Tito akatangazwa kuwa rais wa milele wa nchi hiyo. Katika sera za nje, Tito aliilinda Yugosalvia na ushawishi wa Shirikisho la Kisovieti la Urusi (USSR), na kwa sababu hiyo akajitoa kwenye kambi ya nchi za Kikomunisti duniani. Jemadari Josip Tito aliaga dunia tarehe 4 Mei mwaka 1980 baada ya kuugua kwa muda mrefu. 

Jemadari Josip Tito

Miaka 114 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, yaani tarehe 9 Ramadhani mwaka 1325:

Aliaga dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamedani. Alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa na arifu mashuhuri wa karne ya 13 na 14 Hijria hapa nchini Iran ambaye alitajika kwa taqwa na uchaMungu na ukamilifu wa elimu na matendo. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi, Ayatullah Hamedani alielekea chuo cha kidini cha Najaf nchini Iraq ili kuendelea na masomo ya juu. Baada ya kumaliza masomo yake alifanya kazi ya usomeshaji na udarsishaji. Athari za alimu huyo zimekusanywa katika kitabu kiitwacho "Tadhkiratul-Muttaqin".

Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamedani

Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1963:

Hati ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ilisainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 32 za bara hilo. Marais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Kwame Nkrumah wa Ghana na Ahmed Sekou Toure wa Guinea walikuwa miongoni mwa waasisi wa jumuiya hiyo. Jumuiya ya OAU ilielekeza jitihada zake katika kuleta umoja kati ya nchi za Afrika, kutatua hitilafu kati ya nchi hizo, kutetea haki ya kujitawala ya nchi wanachama na ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika zilizokuwa zingali zinakoloniwa. Mnamo mwezi Julai mwaka 2002, viongozi wa nchi wanachama wa OAU walifanya kikao nchini Afrika Kusini na kuamua kubadilisha jina la jumuiya hiyo kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) sambamba na kuanzisha taasisi kadhaa kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya umoja huo na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama. Hivi sasa Umoja wa Afrika una nchi 54 wanachama. Makao Makuu ya umoja huo yako Addis Ababa, Ethiopia na kikao cha viongozi wa nchi wanachama hufanyika kila mwaka katika moja ya nchi hizo.

Makao Makuu ya AU, Addis Ababa

Na tarehe 4 Khordad kwa mujibu wa kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya Hijria Shamsia imepewa jina la Siku ya Uhimilivu wa Dezful, ambao ni moja ya miji ya kusini mwa Iran. Sababu ya siku hii kupewa jina hilo ni muqawama na ungangari wa watu wa Dezful kukabiliana na hujuma na mashambulio ya makombora ya utawala wa Kibaathi wa Iraq wakati wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Wakati vilipoanza vita hivyo vya Kujihami Kutakatifu, mji wa Dezful ulishambuliwa kwa makombora zaidi ya 200 na kwa risasi zaidi ya elfu ishirini mpaka ukajulikana kwa jina la mji wa makombora. Pamoja na yote hayo wananchi katika mji wa Dezful waliendelea kuonyesha muqawama na uhimilivu kiasi kwamba hata katika mazingira hayo Sala ya Ijumaa iliendelea kusaliwa kila wiki kwa kuhudhuriwa na wananchi na wapiganaji waliokuwa kwenye medani za vita.