May 26, 2018 02:20 UTC
  • Jumamosi, Mei 26, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 10 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1439 Hijria sawa na tarehe 26 Mei 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1442 yaani tarehe 10 Ramadhani mwaka wa tatu kabla ya hijra, aliaga dunia katika mji wa Makka, Bibi Khadija (as), mke mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Bibi Khadija (as), ambaye alikuwa mmoja wa wanawake matajiri na watajika wa Kikureishi alifunga ndoa na Bwana Mtume SAW miaka 15 kabla ya mtukufu huyo kubaathiwa na kupewa Utume. Bibi huyo mtukufu alikuwa mtu wa mwanzo aliyeuamini Utume wa Nabii Muhammad SAW na akajitolea nafsi yake na mali na utajiri wake wote kuihami dini tukufu ya Uislamu. Kuwepo kwa Bibi Khadija kulikuwa na umuhimu mkubwa kwa Bwana Mtume, kiasi kwamba Mtukufu huyo alikuelezea kufariki dunia kwa Bibi Khadija kuwa ni msiba mkubwa mno, hata akaupa mwaka wa kufariki kwake na ambao alifariki pia msaidizi wake mwengine mkubwa, yaani Ami yake Abu Talib kuwa ni "Mwaka wa Huzuni". Baada ya kufariki dunia Bibi Kahdija (as), Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa kila mara akimtaja kwa wema. Miongoni mwa aliyoyasema kuhusu Mama huyo mtukufu wa Waumini ni kwamba: "Wallahi Mwenyezi Mungu hajanipa aliye mbora kuliko Khadija. Aliniamini wakati watu walipokuwa wakikanusha na akanisadikisha wakati watu walipokuwa wakinikadhibisha". ***

Miaka 954 iliyopita, Khoja Nidham al-Mulk waziri msomi na maarufu wa silsila ya Saljuqiyan aliuawa na wapinzani wake. Alizaliwa 410 Hijria Qamariya katika mji wa Tus kaskazini mashariki mwa Iran. Alihudumu katika utawala wa Saljuqiyan kwa muda wa miaka 40. Nidhamul Mulk aliteuliwa kuwa waziri katika utawala wa silsila ya Saljuqiyan na kufanya jitihada kubwa ya kusimamia masuala ya nchi. Katika kipindi hicho Khoja Nidham al-Mulk aliasisi shule kama Nidhamiya ambayo ilifundisha humo Fikifi, Tafsiri na elimu nyingine zilizokuwa zimeenea kkatika zama hizo. Kitabuu mnashuhuri cha msomi huyo ni "Siyasat Nameh".***

Khoja Nidham al-Mulk

Katika siku kama ya leo miaka 219 iliyopita, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow. Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake. Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru. ***

Alexander Pushkin

Miaka 138 iliyopita katika siku kama ya leo, Charles Louis Alphonse Laveran, daktari wa Kifaransa aligundua chanzo cha ugonjwa wa malaria duniani. Baada ya kupata shahada yake ya uzamifu, Daktari Alphonse Laveran alisafiri Algeria kwa lengo la kuhudumia watu wa nchi hiyo kuhusiana na masuala ya afya na tiba. Akiwa huko alipata fursa ya kuchunguza na kufanya utafiti wa kina kuhusiana na malaria, ugonjwa ambao ulikuwa ukiwaangamiza watu wengi katika pembe tofauti za dunia, ambapo mwaka 1880 alifanikiwa kupata chanzo cha ugonjwa huo. Aligundua kuwa ugonjwa huo ulisababishwa na mbu waanaoitwa Anopheles ambao huishi katika sehemu za unyevunyevu na zilizo na maji yaliyotuama. Mwaka 1907 Alphonse Laveran alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na juhudi kubwa alizofanya katika uwanja wa tiba na ugunduzi wake wa chanzo cha ugonjwa wa malaria. ***

Charles Louis Alphonse Laveran,

Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita, Ufaransa ilianza rasmi kuikoloni Tunisia. Kabla ya hapo Ufaransa ilianza kupenya Tunisia kupitia harakati za kiuchumi na kibiashara. Aidha kwa miaka kadhaa Tunisia ilikuwa ikidhibitiwa na Ufaransa. Hata hivyo katika muongo wa 1930 Miladia zilianza harakati za kupigania uhuru kwa uongozi wa Habib Bourguiba, na ilipofika mwaka 1957 nchi hiyo ikajipatia uhuru wake huku Bourguiba akiwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Hata hivyo hadi kufikia mwaka 1987 Bourguiba alianza kuiongoza nchi hiyo kwa mabavu na hivyo kupelekea kupinduliwa na Zine El Abidine Ben Ali. Ben Ali ambaye naye pia aliendeleza sera za udikteta na ukandamizaji aling'olewa madarakni kupitia mapinduzi ya wananchi ya mwezi Januari 2011, na kukimbilia Saudi Arabia. Tunisia yenye ukubwa wa kilometa mraba 163,610 iko kaskazini mwa Afrika na inapakana na nchi za Libya, Algeria na Bahari ya Mediterania. ***

Bendera ya Tunisia

Katika siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, kisima cha kwanza cha mafuta cha Iran kilianza kutoa mafuta katika mji wa mji wa Masjid Suleiman katika mkoa wa Khozestan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Kisima hicho kilichokuwa na urefu wa mita 600 kilianza kutoa mafuta ambayo yalijaa hadi mita 25 kutoka ardhini. Mji wa Masjid Suleiman una utajiri mkubwa wa madini na mafuta na hadi sasa zaidi ya visima vya mafuta 250 vimechimbwa katika mji huo. Si vibaya kukumbusha hapa kwamba, Iran ina utajiri mkubwa wa mafuta suala ambalo limeifanya ihesabiwe kuwa miongoni mwa nchi muhimu duniani. Pia baada ya Russia Iran ni nchi ya pili kuwa na utajiri mkubwa zaidi wa akiba ya gesi duniani. ***

Kisima cha kwanza cha mafuta cha Iran

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, nchi ya Guyana inayopatikana kaskazini mwa Amerika ya Kusini ilipata uhuru wake. Ardhi ya Guyana iligunduliwa na mabaharia wa Kihispania huko kaskazini mwa Amerika ya Kusini karibu miaka 500 iliyopita na baadaye nchi hiyo ikawa chini ya mkoloni Mhispania. Hata hivyo mwanzoni mwa karne ya 17 Miladia, vita vilizuka kati ya makoloni ya Ulaya kwa ajili ya kulidhibiti eneo hilo ambalo lilijumuisha Guyana, Guyana ya Ufaransa, Surinam na baadhi ya maeneo ya Brazil na Venezuela ya sasa. ***

Bendera ya Guyana

Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, kuliundwa rasmi Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Baraza hilo linazijumuisha nchi 6 za kusini mwa Ghuba ya Uajemi ambazo ni Saudi Arabia, Kuwait, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Qatar na Oman. Malengo ya kuundwa baraza hilo ni kuweko ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kushirikiana nchi wanachama katika kukabiliana na vitisho vya kigeni. ***

Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi

Na katika siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, aliaga dunia Ustadh Rahim Moazzen Zadeh Ardabili mwadhini mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa katika familia ambayo ilikuwa ikishughulisha zaidi na harakati za kidini na kuuadhini. Rahim Moazzen Zadeh Ardabili alikuwa mtoto mkubwa wa Sheikh Abdul-Karim na alifuata njia ya baba yake kwa nguvu zake zote.  Baada ya kufariki dunia baba yake, Rahim Moazzen Zadeh Ardabili akaendeleza kazi ya mzazi wake huyo ya kuadhini. Hatimaye mwadhini huyo mashuhuri wa Iran aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 80. ***

Ustadh Rahim Moazzen Zadeh Ardabili