May 29, 2018 00:52 UTC
  • Jumanne, Mei 29, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 13 Ramadhan, 1439 Hijiri sawa na tarehe 29 Mei 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1344 iliyopita inayosadifiana na tarehe 13 Ramadhani mwaka 95 Hijria, alifariki dunia Hajjaj bin Yussuf Thaqafi, liwali katili na dhalimu katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah. Hajjaj bin Yussuf Thaqafi aliishi katika kipindi cha Abdul Malik Marwan na Hisham bin Marwan, na alikuwa mashuhuri kwa kuwatesa na kuwauwa wapinzani wa utawala wa Bani Umayyah, hasa wafuasi wa Imam Ali bin Abi Talib AS na watu wa familia ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Baadhi ya wanahistoria wameandika kuwa, zaidi ya watu 120,000 waliuawa kutokana na amri iliyotolewa moja kwa moja na Hajjaj bin Yussuf Thaqafi. Miongoni mwa jinai zilizowahi kufanywa na Hajjaj Thaqafi ni pamoja na kushambulia mji mtakatifu wa Makka na kuharibu al Kaaba katika mwaka 74 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 565 iliyopita sawa na tarehe 29 Mei 1453 ilikombolewa bandari ya Constantine iliyokuwa makao makuu ya ufalme wa Roma ya Mashariki na vikosi vya Sultan Muhammad Fatih, mtawala wa dola la Othmaniya. Amri ya kwanza iliyotolewa na Muhammad Fatih baada ya kuudhibiti mji huo ilikuwa ni kudhaminiwa usalama na uhuru wa wakaazi wake. Mfalme huyo alitoa amri ya kukarabatiwa mji huo na kujengwa msikiti, ambao leo hii unajulikana kwa jina la Msikiti wa Sultan Ahmed. Ilipofika mwaka 1930 mji wa Constantine ulibadilishwa jina na kuitwa Istanbul, na ni miongoni mwa miji muhimu zaidi ya Uturuki ulioko magharibi mwa nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita alifariki dunia Mirza Jahangir Khan Ghashghaei, faqihi na mtaalamu wa Irfan wa nchini Iran. Alizaliwa eneo la Ghashghaei katikati mwa Iran na kuanza kujifundisha elimu na maarifa ya Kiislamu ambapo aliinukia kielimu. Baadaye Mirza Jahangir Khan Ghashghaei alielekea mjini Isfahan moja  ya miji mikubwa ya Iran na kujishughulisha na kazi ya kulea wanafunzi ambapo alichukua karibu miaka 50 kwenye kazi hiyo. Miongoni mwa wanafunzi wake mashuhuri alikuwa ni Ayatullah Mudarres na Ayatullah Borujerdi. Alifariki dunia akiawa na umri wa miaka 85 na kuzikwa mjini Isfahani.

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita muwafaka na tarehe 29 Mei 1953, Edmund Hillary mpanda milima kutoka New Zealand na Tenzing Norgay mpanda milima kutoka Nepal walifanikiwa kufika kilele cha mlima Everest, ambao ni mlima mrefu zaidi duniani. Mlima wa Everest wenye urefu wa mita 8,848, ni kilele kirefu zaidi cha silsila ya milima ya Himalaya nchini Nepal. Baada ya Hillary na Norgay kufanikiwa kupanda mlima huo mwaka 1953, makundi mengine ya wapanda milima kutoka katika nchi nyingine duniani pia yaliweza kukwea kilele cha mlima huo katika miaka iliyofuata.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Khordad mwaka 1368 Hijiria Shamsia alifariki dunia Ayatullah Mir Sayyid Ali Fani Isfahani msomi wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Isfahan mwaka 1294 Hijira Shamsia na alianza kujifunza elimu ya msingi ya Kiislamu akiwa na miaka 9. Alimu huyo alistafidi na maulama wakubwa na kufikia daraja ya ijtihad ambapo alihamia Najaf nchini Iraq na kwa muda wa miaka 30 alifundisha kwenye mji huo masomo ya fikih, usul, ilmul qalam na akhlaq. Mwaka 1352 Hijria Shamsia alirejea Iran na kuendelea kufundisha mjini Qum. Miongoni mwa vitabu vya Ayatullah Mir Sayyid Ali Fani Isfahani ni Dastur Hajj wal Umrah, Fawaid Rijaliyah, Arubain Hadith na Tafsiri ya Suratul Faatiha.