Jumatano, 30 Mei, 2018
Leo ni Jumatano tarehe 14 Ramadhan 1439 Hijiria, sawa na tarehe 30 Mei 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1372 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Ramadhani mwaka 67 Hijria, aliuawa shahidi Mukhtar bin Abi Ubaida al Thaqafi, kiongozi wa harakati ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi wake na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na wafuasi wa Yazid bin Muawiya, akilinda dini tukufu ya Kiislamu. Mukhtar alianzisha harakati yake katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilianzisha mapambano dhidi ya utawala wa Bani Umayya, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar al Thaqafi alitawala Kufa kwa muda wa mwaka mmoja hivi, na hatimaye alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi katika siku kama hii ya leo.
Siku kama ya leo miaka 240 iliyopita sawa na tarehe 30 Mei 1778, Francois - Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84. Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kuwekwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza. Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, alifariki dunia Shamsud-Din Bahbahani, mmoja wa wataalamu wa theolojia na alimu mkubwa wa Iran katika karne ya 13 Hijiria. Akiwa kijana Bahbahani alipata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Muhaqiq Bahbahani. Alitambulika kwa elimu kubwa na kutokana na kuwa mtaalamu wa irfani na mwenye zuhudi. Aidha alifanya utalii mwingi na kuandika vitabu mbalimbali. Aliandika kitabu ambacho kilitupia jicho na kufafanua elimu ya usulu, kama ambavyo pia aliandika vitabu mbalimbali katika nyuga za theolojia na usulu.
Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, alifariki dunia Sayyid Muhammad Taqee Mumtaazul-Ulama, mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia nchini India. Mumtaazul-Ulama, ni mmoja wa maulama wa Kishia wa karne ya 13 Hijiria nchini India. Maktaba ya alimu huyo ilikuwa moja ya maktaba kubwa zaidi nchini humo. Sayyid Muhammad Taqee Mumtaazul-Ulama ameacha athari mbalimbali ambapo baadhi yake ni 'Irashadul-Mu'minina' 'Hadiqatul-Waaidhina' na 'Dhwahiiru sh-Shiiat fii Ahkaamu sh-Sharia.' Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78 mjini Lucknow, moja ya miji ya India na kisha kuzikwa ndani ya Husseiniya aliyoiasisi mwenyewe.
Siku kama ya leo 94 miaka iliyopita, alifariki dunia Ali Akbar Khan Nafisi aliyejulikana kama Naadhimul Atwiba, daktari na mtaalamu wa lugha wa Kiirani, katika mji wa Tehran. Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi alianza kujifunza masomo ya kidini na pia udaktari katika chuo cha Darul Funun cha Tehran. Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na Naadhimul Atwiba katika uwanja wa tiba vimetarjumiwa katika lugha za kigeni. Ali Akbar Khan Nafisi ambaye pia alikuwa mtaalamu wa lugha alifanya jitihada nyingi katika kukusanya maneno ya lugha ya Kifarsi na kuandika kamusi inayoitwa 'Kamusi ya Nafisi.'
Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita muwafaka na tarehe 30 Mei 1918, yalimalizika mapigano makubwa ya Maren yaliyotokea wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia kati ya jeshi la Ujerumani na vikosi waitifaki vilivyozijumuisha Marekani, Uingereza na Ufaransa. Vita hivyo vya siku tano vilijiri katika eneo karibu na Mto Maren ulioko kaskazini mashariki mwa Ufaransa ambapo majeshi ya Ujerumani yalijipatia ushindi na kuwashikilia mateka wanajeshi elfu hamsini na tano wa majeshi ya waitifaki.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita inayosadifiana na tarehe 30 Mei 1981, aliuawa Zia ur Rahman Rais wa Bangladesh baada ya kupigwa risasi katika mji wa Chittagong ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Rais Zia ur Rahman aliuawa baada ya kuchungulia dirishani kwenye nyumba ya wageni ya serikali katika mji huo. Watu wanane waliuawa kwenye shambulio hilo, wakiwemo wasaidizi na walinzi wa rais huyo.
Na siku kama ya leo miaka 26 iliyopita Dakta Jalal Samimi mtafiti na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ufundi cha San'at Sharif cha mjini Tehran alifanikiwa kugundua vyanzo vitano vya mionzi ya Gamma katika mzunguko wa kundi la sayari na nyota au Milky Way Gallaxy, baada ya kufanya utafiti na majaribio kwa miaka 20 katika uwanja huo. Inafaa kukumbusha hapa kuwa Dakta Samimi alizaliwa mwaka 1319 Hijiria Shamsia katika mji wa Zabol kusini mashariki mwa Iran na kuhitimu daraja ya udaktari katika somo la Fizikia. Dakta Jalal Samimi alifanikiwa katika ugunduzi huo muhimu baada ya kutwalii na kufanya uchunguzi wa kina na majaribio mengi kuhusiana na Nuclear Emulsion.