Jumanne, Juni Tano, 2018
Leo ni Jumanne 20 Ramadhani mwaka 1439 Hijria Qamaria sawa na 15 Khordad mwaka 1397 Hijria Shamshia zinazosadifiana na Juni Tano mwaka 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita jeshi la Kiislamu lililokuwa na wapiganaji elfu kumi chini ya uongozi wa Mtume Muhammad SAW liliukomboa mji wa Makka. Mtume Mtukufu alichukua hatua hiyo baada ya makafiri kukiuka makubaliano ya amani ya Hudaibiya ambayo yalisainiwa mwaka wa Sita Hijria kati yake na wakuu wa Makuraishi. Mtume Muhammad SAW alitoa msamaha kwa wakazi wote wa Makka baada ya kukombolewa mji huo katika hali ambayo huko nyuma watu hao walikuwa wakipinga na kupiga vita Uislamu na pia walimuudhi mno Mtume na kuwatesa Waislamu wengi. Muamala huo wa huruma na upendo wa Mtume SAW uliwavuta watu wa kabila la Kuraishi kuingia katika dini tukufu ya Uislamu. Kwa msingi huo mji wa Makka ulikombolewa pasina kuwepo umwagaji damu.

Miaka 813 iliyopita katika siku kama ya leo Yaqut Hamawi mmoja wa waandishi na msomi mtajika wa Kiislamu wa karne ya Saba Hijria na mtaalamu mashuhuri wa jiografia aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 539 Hijria huko Baghdad ambapo ujanani mwake alikamatwa mateka na kufanywa mtumwa. Hata hivyo baada ya kupita muda mfanyabiashara mmoja wa Baghdad alimnunua Hamawi na baadae akamuachia huru. Miongoni mwa athari za uandishi za Yaqut Hamawi tunazoweza kuziashiria ni vitabu vyake viwili alivyovipa majina ya "Muujamul-Buldan" na Muujamul- Udabaa."

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran baada ya kupata habari kwamba Imam Khomeini (MA) alikuwa amekamatwa na utawala dhalimu wa Shah, walifanya maandamano makubwa kote nchini dhidi ya utawala huo. Siku kadhaa kabla yake, Imam Khomeini alikuwa ametoa hotuba kali katika Chuo cha Kidini cha Faidhiyya akifichua maovu yaliyokuwa yakifanywa na utawala wa Shah, jambo ambalo liliuchukiza sana utawala huo na kuamua kumtia nguvuni. Suala hilo liliwakasirisha sana wananchi wa Iran ambao waliamua kufanya maandamano ya kushinikiza kuachiliwa kwake mara moja. Ili kukabiliana na wimbi la malalamiko hayo, utawala wa Shah uliamua kuwashambulia waandamanaji ambapo uliua na kuwajeruhi wengi kati yao. Harakati hiyo ya mapambano ambayo inafahamika humu nchini kama Mapambano ya Tarehe 15 Khordad, kwa hakika ulikuwa mwanzo wa mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi shupavu wa Iran dhidi ya utawala wa kitaghuti wa Shah, mapambano ambayo yaliainisha mustakbali wa kisiasa na kijamii wa Iran. Mapambano hayo yaliendelea kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipofikia ushindi mwaka 1979.

Siku kama ya leo miaka 235 iliyopita baluni lilirushwa angani kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya jitihada za mwanadamu za kutaka kupaa angani. Baluni hilo lilikuwa na watu wawili, mmoja wao akiwa ni mwanafizikia wa Kifaransa aliyejulikana kwa jina la Jean-Francois Pilatre de Rozier. Tangu alipokuwa shuleni de Rozier alikuwa akifikiria jinsi ya kutengeneza chombo cha kupaa angani na hatimaye baada ya ndugu wawili wa Montgolfier kutengeneza baluni, naye pia alitengeneza baluni lake na akapaa nalo angani katika siku kama hii ya leo. Mwanafizikia huyo alianguka chini na kufariki dunia katika moja ya safari zake za uhakiki angani.

Miaka 14 iliyopita Ronald Reagan, rais wa zamani wa Marekani aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer. Alizaliwa mwaka 1911 na kuhitimu masomo yake ya juu katika taaluma ya uchumi na masuala ya kijamii. Reagan alianza kufanya kazi kwenye redio na kisha akawa msanii kwenye televisheni. Taratibu alianza kujishughulisha na masuala ya siasa ambapo kwanza alikuwa mwanachama wa chama cha Democrats na kisha kujiunga na chama cha Republicans. Mwaka 1970 aliteuliwa na chama hicho kuwa gavana wa California na kisha mwaka 1980 akafanikiwa kuwa rais wa Marekani baada ya kumshinda mpinzani wake Jimmy Carter. Katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minane Reagan alitekeleza siasa za kijeshi na kichokozi dhidi ya nchi nyingine za dunia. Alianzisha mpango wa kijeshi wa Star Wars na kutoa amri ya kufanyika mashambulio ya kijeshi dhidi ya baadhi ya nchi. Pia alichochea na kuunga mkono kijeshi, kifedha, kipropaganda na kisiasa uvamizi wa utawala wa kidekteta wa Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Na Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, vita vya tatu vikuu kati ya utawala ghasibu wa Israel na nchi za Kiarabu vilianza. Katika uvamizi wa kushtukiza na wa ghafla, ndege za kivita za Israel ziliingia katika anga ya nchi za Misri, Syria na Jordan na kushambulia kwa muda wa masaa mawili mfululizo majeshi na taasisi za anga za nchi hizo na kukaribia kuvitokomeza kabisa. Baada ya hapo jeshi la nchi kavu la Israel lililokuwa likiungwa mkono na Marekani pamoja na Uingereza, kwa muda wa siku sita, lilivamia kwa silaha nzitonzito na za kisasa majeshi ya nchi hizo tatu za Kiarabu na kuyashinda kikamilifu.