Jumamosi, 9 Juni , 2018
Leo ni Jumamosi 19 Khordad mwaka 1397 Hijria Shamsia sawa na 24, Ramadhani mwaka 1439 Hijria Qamaria inayosadifiana na Juni 9 mwaka 2018 Miladia
Siku kama ya leo miaka 729 iliyopita alifariki dunia Qutbuddin Shirazi, tabibu, mwanahesabati, mwanafikizia na mwanafalsafa wa Kiirani katika mji wa Tabrizi huko kaskazini magharibi mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi. Alibobea pia katika elimu za mantiki na irfani. Alifanya hima kubwa kutafuta elimu ya tiba na alihudumu kwa miaka mingi kama tabibu katika hospitali ya Shiraz, kusini mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu wa kwanza kufanya uchunguzi kuhusu upinde wa mvua na kupata tafsiri ya kisayansi kuhusu suala hilo. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai, mmoja wa maulamaa na wataalamu wa elimu ya irfani. Sayyid Muhammad Tabatabai alizaliwa mjini Tabrizi kaskazini mwa Iran, mwaka 1325 Hijiria. Akiwa na miaka 19 alielekea mjini Najaf, Iraq akiwa na kaka yake mkubwa Allamah Muhammad Hassein Tabatabai na kupata kusoma elimu ya dini mjini hapo. Baada ya kutabahari katika elimu ya Kiislamu alirejea eneo alikozaliwa la Tabriz na kujishughulisha na kuwalea wanafunzi.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita moto mkubwa ulitokea katika Chuo Kikuu cha Algiers mji mkuu wa Algeria. Moto huo ulichoma zaidi ya nakala laki tano za vitabu vyenye thamani kubwa zilizokuwa kwenye maktaba ya chuo hicho. Asilimia kubwa ya vitabu vilivyoungua vilikuwa miongoni mwa marejeo muhimu na nadra. Chuo Kikuu cha Algiers na maktaba yake vilichomwa moto na jeshi la siri la Ufaransa nchini Algeria. Jeshi hilo la siri liliundwa na askari wa Ufaransa waliokuwa wakipinga suala la kupewa uhuru Algeria. Moto huo ulikuwa miongoni mwa makumi ya mioto kadhaa iliyotokea katika siku hiyo nchini Algeria na mingi ilisaabishwa na jeshi la siri la Ufaransa.

Miaka 133 iliyopita muwafaka na leo, jeshi la Ujerumani lilivamia ardhi ya Togo huko magharibi mwa Afrika. Wakati huo maeneo ya pwani ya Togo yalikuwa sehemu bora kwa watu wa Ulaya kwa ajili ya biashara ya utumwa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Togo imekuwa maarufu kwa jina la "Pwani ya Utumwa." Wakoloni wa Ujerumani waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi ya Togo hadi wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya hapo Togo ilikoloniwa na Wafaransa na Waingereza. Nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 1960.