Jun 10, 2018 09:57 UTC
  • Jumapili, Juni 10, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 25 Ramadhani 1439 Hijria, sawa na tarehe 10 Juni mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 228 iliyopita yaani sawa na tarehe 10 Juni 1790 vikosi vya Uingereza viliivamia ardhi ya Malaya inayojulikana hii leo kama Malaysia. Wakati huo Uholanzi ilikuwa ikiikoloni Malaya na kupora utajiri mkubwa wa nchi hiyo wa madini ya bati. Kwa kuingia vikosi vya Uingereza Malaya ilibidi Uholanzi ianze kuondoka nchini humo na ilipofikia mwaka 1824 ilikubali kuiachia Uingereza ardhi hiyo kwa sharti kwamba nayo iachiwe Indonesia ambayo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Uholanzi. Malaysia ilijipatia uhuru wake mwaka 1957 na Indonesia mwaka 1956.

Malaysia

Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, vita vya Marekani na Uingereza vilianza. Miongoni mwa matukio muhimu ya historia ya Marekani katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 ni vita hivyo vilivyodumu kwa miaka miwili. Sababu ya kuanza vita hivyo inasemekana kuwa ni kuzingirwa Ufaransa na Uingereza kutokea baharini na kuzuiwa safari za meli za Marekani katika maji yanayozunguka nchi za Ulaya. Lakini pamoja na hayo Marekani ilikuwa na sababu zingine za kuanzisha vita hivyo, muhimu kati yazo ikiwa ni madai ya uungaji mkono wa siri wa Uingereza kwa Wahindi Wekundu wa Marekani dhidi ya serikali kuu ya nchi hiyo. Kufuatia vita hivyo, tarehe 18 Juni 1812 askari jeshi wa Marekani walivamia vituo na mali za Uingereza huko Canada na kuuteketeza mji wa Toronto. Vita hivyo vilipamba moto kiasi kwamba, mwezi Agosti 1814 Uingereza ilituma askari wake katika pwani ya mashariki ya Marekani na kuendesha vita hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Washington DC. Hatimaye mazungumzo ya amani baina ya nchi mbili hizo yalitiwa saini huko Ubelgiji na kupelekea kusimamishwa vita hivyo mwezi Disemba mwaka huhuo wa 1814.

Bendera za Marekani na Uingereza

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 Pierre Loti, mwandishi mkubwa wa Ufaransa. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya juu, alijiunga na kikosi cha majini katika jeshi la Ufaransa sambamba na kuhudumia nyadhifa kubwa jeshini. Ni wakati huo ndipo alipoanzisha shughuli zake za fasihi huku akieneza machapisho yake. Muda mfupi baadaye Pierre Loti alipata umshuhuri ambapo mwaka 1891 aliteuliwa kujiunga na kituo cha utamaduni nchini humo. Baada ya hapo alifanya safari mashariki ya mbali, safari za baharini na Mashariki ya Kati na kupata kuandika kuhusu mambo mbalimbali duniani. Aidha Loti alifika nchini Iran na kuandika kitabu kuhusiana na mambo ya kuvutia ya mjini Isfahani. Pierre Loti aliacha athari mbalimbali ambazo baadhi zipo hadi leo katika maktaba za nchini Ufaransa.

Pierre Loti

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, aliuawa shahidi baada ya kuteswa kwa muda mrefu katika moja ya jela za utawala wa kitwaghuti wa Shah, Ayatullah Sayyid Muhammad Reza Saeedi, mmoja wa wasomi wakubwa na wanamapambano wa Iran. Alielekea mjini Qum na kujiunga na hawza ya kielimu kwa ajili ya kujifunza elimu ya dini ya Kiislamu ambapo akiwa mjini hapo alipata kusoma kwa maulama wakubwa akiwemo Ayatullahil-Udhma Borujerdi na Imamu Khomein (MA). Baada ya mwamko wa mapinduzi ya wananchi Waislamu nchini Iran, tarehe 15 Khordad 1342 Hijiria, alishadidisha harakati zake dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah. Katika uwanja huo, Ayatullah Sayyid Muhammad Reza Saeedi aliufanya msikiti wake kuwa ngome katika kuwafungua wananchi hususan vijana upeo wao ambapo hotuba zake nyingi zilijikita katika kufichua njama chafu za ukoloni na jinai za utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya raia madhlumu wa Palestina. Ni kwa ajili hiyo ndio maana alikamatwa mara kadhaa na kufungwa jela huku akiteswa vikali. Hata hivyo vitendo hivyo vya utawala wa Shah havikuweza kuathiri hata kidogo azma ya mwanazuoni huyo mtajika wa Kiislamu. Miongoni mwa athari za Ayatullah Sayyid Muhammad Reza Saeedi ni pamoja na kitabu cha ‘Umoja wa Kiislamu’ ‘Uhuru wa Mwanamke’ na ‘Kazi na Uislamu.’

Ayatullah Sayyid Muhammad Reza Saeedi,

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Bani Sadr Rais wa kwanza wa Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliuzuliwa na Imam Khomeini wadhifa wa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote kutokana khiyana na usaliti wake. Tangu awali baada ya kuchaguliwa kuwa rais, Bani Sadr alikumbwa na kiburi na ghururi na akawa anafuatilia suala la kuviweka kando vikosi vya mapinduzi vilivyokuwa vitiifu kwa Imam Khomeini, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha Bani Sadr alikuwa akishirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu. Bani Sadr alikwamisha utendaji wa serikali kutokana na kukwepa kwake kumkubali Waziri Mkuu Muhammad Rajai mmoja wa wanamapambano mashuhuri aliyekuwa amechaguliwa na bunge kwa wingi wa kura. Ukwamishaji huo wa Bani Sard ulifikia kilele katika vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran na kupelekea miji mingi ya Iran katika kipindi hicho cha vita kukaliwa kwa mabavu na utawala wa dikteta Saddam Hussein. Hatimaye katika siku kama ya leo, Imam Khomeini alimuuzulu Bani Sadr cheo cha Amiri Jeshi Mkuu. Siku chache baadaye bunge lilipasisha kwa wingi wa kura mswada wa kutokuwa na imani na uwezo wa kisiasa wa rais huyo.

Bani Sadr 

Na siku kama yaleo miaka 18 iliyopita Hafez al-Assad rais wa wakati huo wa Syria aliaga dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alizaliwa mwaka 1930. Aliteuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha Syria mwaka 1964 na kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo miaka mitatu baadaye. Hafez al-Assad aliipindua serikali ya wakati huo ya Syria mwaka 1970 na kuchukua uongozi wa nchi hiyo na kisha kuteuliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Asad aliimarisha jeshi la nchi hiyo kiasi kwamba mwaka 1973 alifanikiwa kurejesha sehemu ya milima ya Golan iliyotekwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel katika vita vya 1967. Siasa muhimu za Hafez al-Assad zilikuwa ni za kutofanya mapatano na utawala huo ghasibu.

Hafez al-Assad rais wa zamani wa Syria

Tags