Chuki dhidi ya dini ya Kiislamu katika nchi za Kimagharibi 40 + Sauti
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 40 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.
Katika kipindi kilichopita tulizungumzia kuendelea kampeni ya Waislamu nchini Uingereza ya kuwafungulia milango ya misikiti, watu wasio kuwa Waislamu kwa lengo la kuwaelemisha na kuwafahamisha juu ya Uislamu ambapo kabla ya hapo walikuwa hawajui chochote kuhusu dini hiyo inayolingania amani, upendo na uadilifuu. Ndugu wasikilizaji mnapaswa kufahamu kwamba chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu, haifutiki kwa kufunguliwa tu milango ya misikiti kwa watu wasio Waislamu kwa ajili ya kujibiwa shubuhati kuhusu mafundisho ya ubinaadamu yanayolinganiwa na dini ya Uislamu.
Hii ni kusema kuwa, katika nchi nyingi, kumekuwa kukifanyika makongamano na vikao tofauti kwa ajili ya kuyaarifisha mafundisho ya dini ya Uislamu. Moja ya makongamano hayo ni lile lililofanyika hivi karibuni mjini Qum, Iran ambao unafahamika kuwa moja ya vituo muhimu vya hauza ya kielimu vya madhehebu ya Shia nchini hapa. Kongamano hilo lililopewa jina la 'Uislamu Barani Ulaya, Mitazamo na Changamoto' lilihudhuriwa na wahadhiri na watafiti kutoka vyuo vikuu vya Ulaya na shule pamoja na asasi za Kiislamu mjini hapo. Aidha kongamano hilo lilijadili maudhui nne kuu ambazo ni hali ya Uislamu katika kuamiliana na mataifa ya Ulaya, mitazamo na changamoto katika mahusiano kati ya Uislamu na Ulaya, hali ya Ulaya katika kuamiliana na dini ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla na historia ya muamala wa Uislamu barani humo. Kongamano hilo lilihudhuriwa na wahadhiri kutoka nchi za Uingereza, Croatia, Jamhuri ya Czech, Italia, Canada, Uholanzi na watafiti kadhaa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Miongoni mwa washiriki maarufu walioshiriki kongamano hilo ni kama vile, Robert M. Gleave, profesa na muhadhiri wa masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Exeter nchini Uingereza, Andrew J. Newman, muhadhiri na mtaalamu wa masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland, Profesa Joseph Eulwell, muhadhiri wa Chuo Kikuu cha mjini Roma, Italia, Profesa Vedran Abochina, muhadhiri wa Chuo Kikuu Croatia, Profesa Daniel Krizek, Profesa Jaroslav Franck na Peter Pelican kutoka Jamhuri ya Czech wakiwemo pia wahadhiri kutoka vyuo vikuu tofauti vya Jamhuri ya Czech, Uholanzi na Iran.
*****
Mwanzoni mwa kongamano hilo Ayatullah Muhsen Malek Afzali, mkuu wa taasisi ya 'al-Hekmat' alisema: "Katika miongo iliyopita, tulishuhudia ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu kati ya wafuasi wa dini za mbinguni hususan barani Ulaya." Aliendelea kufafanua baadhi ya sababu za ongezeko hilo la chuki dhidi ya dini ya Uislamu kwa kusema: "Vitendo vya ukatili na jinai za makundi ya kigaidi na ukufurishaji kama vile Daesh (ISIS) Telaban, Jab'hatu Nusra, Boko Haram, ash-Shabab, propaganda za vyombo vya Kizayuni dhidi ya dini ya Uislamu na kadhalika harakati za vyama na shakhsia tofauti wa kisiasa wenye ubaguzi, ni sababu ya kuibuka chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu." Mwisho wa kunukuu.
Naye kwa upande wake, Ayatullah Mehdi Hadavi Tehrani mmoja wa wahadhiri wa hauza na chuo kikuu alihutubia mkutano huo kuhusiana na hali ya Uislamu barani Ulaya na kupatiwa njia ya utatuzi wa chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu kwa kusema: "Watu wengi katika nchi za Magharibi wanadhani kwamba mauaji ya umati, kama yale yanayoshuhudiwa leo nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya, na kuwafanya wahajiri na wakimbizi Waislamu kutoka nchi zao asilia ndio njia ya kumaliza chuki dhidi ya Uislamu. Katika hali ambayo njia ya utatuzi wa suala hilo ni ya amani na kuishi pamoja." Msomi huyo mtajika aliendelea kufafanua kwamba: "Kuishi pamoja na kadhalika kushirikiana ni mambo yanayowezekana. Ili kufikiwa mahusiano mkabala kwanza lazima kuwepo mtazamo chanya kuhusu upande wa pili." Akiendelea kufafanua misimamo mikali na kuchupa mipaka ambayo kimsingi haikuwa na faida ghairi ya kuusababishia Uislamu matatizo makubwa alisema: "Misimamo mikali na kuchupa mipaka ipo pia hata kwa Mayahudi na Wakristo, Mayahudi wenye kuchupa mipaka na siasa kali ndio hawa Mazayuni ambao idolojia yao inakosolewa vikali hata na Mayahudi wengi duniani. Lakini pia tunayo misimamo mikali isiyo ya kidini kama vile Usekulari.
Watu wenye misimamo mikali ya kigaidi kama vile Mabudha wa nchini Myanmar na Wahindu nchini India, wanashuhudiwa kila siku na walimwengu." Kadhalika Ayatullah Mehdi Hadavi Tehrani ambaye ni mmoja wa wahadhiri wa hauza na chuo kikuu aliendelea kusema: "Suala la Waislamu wa Shia kwa wao kuamini akili na naqli (mapokezi) linafanana na lile la Wakristo wa Kikatoliki, katika kutumia akili na kushikamana na kitabu cha Mwenyezi Mungu, lakini wapo Mawahabi na Masalafi ambao wanawakufurisha Waislamu hao wa Shia. Suala ambalo ni sawa na wafuasi wa kanisa la Orthodox ambao nao wanawaona Wakristo wa madhehebu ya Ukatoliki kuwa ni makafiri na wasio Wakristo wa kweli." Mwisho wa kunukuu???!!!
*****
Kama kwanza ndio unafungua redio yako, kipindi kilichoko hewani ni makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi hii ikiwa ni sehemu ya 40. Katika uwanja huo, Profesa Joseph wa chuo cha elimu ya kisiasa Jamhuri ya Czech, ni mmoja wa wahadhiri waliokemea chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu katika kongamano hilo la mjini Qum, Iran ambapo alielezea athari mbaya za miendo hiyo nchini kwake. Aidha sambamba na kuashiria uwepo wa Waislamu 3000 wenye asili ya Jamhuri ya Czech na wahajiri elfu 20 Waislamu ambao kila uchao hushuhudia wimbi la chuki na ubaguzi hata kutoka kwa viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo alisema: "Wanachama wa mrengo wa kulia na wenye misimamo mikali ya kigaidi wamepenyeza sana katika siasa za Jamhuri ya Czech, hivyo hawafurahishwi kuona dini ya Uislamu ikipanuka." Mwisho wa kunukuu.
Naye kwa upande wake Robert M Gleave, mkuu wa kituo cha utafiti wa Kiislamu katika chuo cha Exeter, nchini Uingereza aliyataja makundi ya kufurutu ada yanayoeneza chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu na kadhalika makundi ya Kisalafi na Kiwahabi ambayo yanawakufurisha watu wengine kuwa ndio tishio pekee la jamii ya Ulaya. Akijibu swali kupitia mahojiano aliyofanyiwa kuhusu hali ya makundi ya kufurutu ada katika jamii ya Ulaya, alisema: "Hivi sasa moja ya masuala ambayo yamewazidishia wasi wasi walio wengi barani Ulaya ni kudhihiri makundi ya kibaguzi ya mrengo wa kulia. Makundi hayo ambayo yana itikadi zinazokaribiana na zile za Wanazi yamekuwa yakifanya mashambulizi dhidi ya jamii za walio wachache wakiwemo Waislamu. Kwa hakika makundi hayo yamebadilika na kuwa tishio kwa uthabiti wa kiutamaduni na kwa jamii ya Ulaya. Hii ni aina ya siasa kali (kufurutu ada) inayoshuhudiwa hii leo katika nchi za Magharibi. Aina nyingine ya hali hiyo inayotia wasi wasi mkubwa ni Usalafi ambao wakati mwingine huakisi kwa daraja ya kwanza mienendo ya kufurutu ada.
Kuenea kwa Usalafi hususan Usalafi unaolingania upanga, ni suala ambalo limesababisha wasi wasi mkubwa kwa kuwa katika matukio mengi tunakabiliana na vijana ambao hawaheshimu hata shakhsia wakubwa wa kielimu katika jamii. Na hayo yanashuhudiwa pia katika mitandao ya kijamii ya intaneti. Katika mitandao hiyo, vijana hao hukutana na masheikh wa Kisalafi na Kiwahabi ambao baadaye huweza kuwarubuni na kupewa itikadi kali. Na aina hii ya utumiwaji mbaya wa mitandao ya kijamii inazini kuongezeka siku hadi siku." Mwisho wa kunukuu.
*******
Ndugu wasikilizaji tulisema kuwa tangu alipoingia madarakani Rais Donald Trump katika ikulu ya Marekani White House, wimbi la chuki na ubaguzi nchini humo limeshika kasi mara dufu.
Kwa mfano tu hivi karibuni 'Kituo cha Sheria ya Umasikini' kituo ambacho kinajihusisha na kufuatilia haki za raia nchini Marekani kiliripoti kwamba mwaka 2017 ambao ni mwaka mmoja tangu Trump alipoingia madarakani, makundi yenye kueneza chuki dhidi ya Uislamu yaliongezeka kutoka 101 na kufikia 114. Kadhalika kituo hicho kilitangaza kuwa, makundi mengine yanayoeneza chuki katika jamii ya Marekani yameongezeka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kufikia asilimia 20. Hadi kufikia mwaka jana 2017 jumla ya makundi 954 yanayoeneza chuki yalikuwa yakiendesha harakati zake nchini humo ongezeko ambalo ni asilimia nne ikilinganishwa na miaka ya hapo kabla.
Ndugu wasikilizaji sehemu ya 40 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./