Jumapili 17 Juni
Leo ni Jumapili tarehe Tatu Shawwal 1439 Hijiria, sawa na tarehe 18 Juni 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 442 iliyopita, sawa na tarehe 17 Juni 1576, William Silent kiongozi wa harakati ya wananchi wa Holland dhidi ya Uhispania, alitangaza uhuru wa nchi hiyo. Harakati hiyo ilianza mwaka 1568 na iliandaa uwanja wa kuundwa nchi moja baada ya kuungana majimbo 8 ya Holland. Ingawa Holland ilitangazwa kuwa huru lakini wananchi wa nchi hiyo waliendelea kukandamizwa na wanajeshi wa Uhispania hadi mwaka 1609 yalipotiwa saini makubaliano ya amani kati ya viongozi wa Holland na mafalme wa Uhispania, na kutambua rasmi kujitawala kwa Holland. Nchi hiyo baada ya kujitawala taratibu ilianza kuzidhibiti na kuzikalia kwa mabavu nchi nyingine na ilipofika karne ya 17 Miladia Holland iliingia katika kundi la nchi zenye nguvu za Ulaya zilizozikoloni nchi nyinginezo.
Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita sawa na tarehe 17 Juni 1925, ulitiwa saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za vijidudu na kemikali mjini Geneva Uswisi. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utumiaji vitani wa aina yoyote ya silaha za vijidudu, gesi zinazoua, sumu za kemikali na nyinginezo kama hizo ulipigwa marufuku. Licha ya kufikiwa makubaliano hayo, lakini baadhi ya nchi bado ziliendelea kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku duniani. Ujerumani ilitumia silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Marekani katika vita vya Vietnam na utawala wa zamani wa Iraq kutumia silaha hizo wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, wakazi wa kisiwa cha Iceland walifanikiwa kupata uhuru wao kutoka mikononi mwa Denmark. Kisiwa cha Iceland kiligunduliwa tarehe 10 Julai 874 Miladia na kuanzia wakati huo, ndipo wahajiri wa Norway, Scotland na Ireland wakaanza kuishi katika kisiwa hicho. Hadi kufikia karne ya 13 Miladia ilikuwa ni nchi huru hata hivyo muda baadaye iliunganishwa na Norway na kisha Denmark. Mwaka 1874 Denmark iliruhusu kuundwa baraza la watunga sheria (yaani bunge) katika kisiwa hicho cha Iceland. Aidha serikali ya ndani ya kisiwa hicho iliendelea kufuatilia haki zake zaidi ingawa bado kiliendelea kutambuliwa kuwa sehemu ya Denmark, hadi tarehe 17 Juni 1944 ambapo kulitangazwa kuvunjwa muungano huo baada ya kurejelewa maoni ya wakazi wa Iceland. Kuanzia wakati huo, wakakazi wa Iceland wanaitambua siku kama ya leo kuwa siku ya kitaifa.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 27 Khordad 1358 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, Imam Khomeini (M.A) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuanzishwa Jihadi ya Ujenzi wa taifa kwa lengo la kujitawala na kujitosheleza taifa la Iran na kujikwamua na umasikini na matatizo mbalimbali hasa vijijini. Kufuatia amri hiyo, wananchi wa matabaka mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wanachuo na vijana wenye imani na wasomi waliungana nayo ili kujenga na kukarabati maeneo yaliyokuwa duni na yaliyokuwa nyuma kimaendeleo. Jihadi ya ujenzi wa taifa ambayo ni matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu ilibadilisha sura ya maeneo mbalimbali duni nchini, kutokana na hatua muhimu zilizochukuliwa za ujenzi wa miundo mbinu. Baadaye jihadi ya ujenzi ilibadilishwa na kuwa wizara na kisha kuunganishwa na wizara ya kilimo na kuwa Wizara ya Jihadi ya Kilimo.