Jun 18, 2018 07:12 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Juni 18

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita, haswa matokeo ya michuano ya Kombe la Dunia Russia.....

Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya Soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka mshindi wa bao moja kwa nunge katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia iliposhuka dimbani kuvaana na Morocco katika mji wa mjini St. Petersburg nchini Russia siku ya Ijumaa. Bao la ushindi la Iran lilipachikwa wavuni kunako dakika ya 95 katika muda wa ziada ambapo mchezaji wa Morocco Azizi Bouhaddou alijifunga katika mechi hiyo ngumu ya ufunguzi.

Mchuano wa Iran dhidi ya Morocco

 

Ushindi huo ni wa kwanza wa Iran katika kombe la dunia tokea mwaka 1998.  Morocco ilicheza vizuri katika dakika 30 za kwanza kabla ya Iran nayo ikaweza kuinuka na kupoteza nafasi ya kufunga kabla ya kumalizika nusu ya kwanza. Katika kipindi cha pili timu zote zilionekana kuwa na nguvu sawa na mechi ilikuwa inaelekea kumalizika kwa sare tasa, kabla Morocco kujifunga. Mji wa Tehran uliripuka kwa nderemo, vifijo, hoi na vigelegele baada ya ushindi huo, huku wakazi wa mji huo mkuu wa Iran wakimiminika mabarabarani kushangilia ushindi huo wa kwanza wa Iran kwenye mashindano hayo.

Awali, timu ya taifa ya soka ya Russia ilianza mashindano hayo ya soka ya Kombe la Dunia kwa kishindo baada ya kuigaragaza Saudi Arabia mabao matano kwa nunge katika ufunguzi wa duru ya 21 ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu. Katika mchezo huo wa kundi la A kwenye uwanja wa Luzhniki, mjini Moscow, timu ya Russia ilionyesha mchezo mzuri na wa kusisimua mbele ya washabiki wa nyumbani, na kufanikiwa kuifunga Saudia mabao matano bila jibu.

Wachezaji wa Russia wakishangilia bao dhidi ya Saudia

Gazeti la al-Youm Sabaa limenukuu Mkurugenzi wa timu ya taifa ya Saudia, Adel Ezzat akisema yumkini wachezaji watatu wa timu hiyo wakakabiliwa na adhabu ya kifungo jela watakaporejea nyumbani, kwa kufanya uzembe na kuruhusu kichapo hicho cha mbwa kutoka Russia, tena mbele ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Muhammad Bin Salman. Katika ufunguzi wa michuano ya kombe la dunia mwaka huu Rais Vladmir Putin wa Russia alisema kuwa zaidi ya watu bilioni moja duniani ni mashabiki wa mpira wa miguu na kwamba watu hao wanafuatilia michuano hiyo. Zaidi ya vongozi wa nchi 20 walihudhuria sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo siku ya Alkhamisi.

Huku hayo yakirifiwa, timu ya Misri inayowakilisha bara la Afrika, imeanza vibaya michuano ya Kombe la Dunia Russia 2018 kwa kukubali kipigo cha goli 1 – 0 dhidi ya timu ya Amerika Kusini, Uruguay. Misri ambayo ilicheza bila nyota wake Mohamed Salah, anayechezea timu ya Liverpool ya Uingereza, ilionyesha mchezo mzuri katika vipindi vyote kabla ya kuruhusu goli dakika za mwisho za mchezo. Kombora moja mlinda mlango wa Mirsi, Mohamed El-Shenawy, aliyekuwa nyota wa mchezo aliokoa na lingine kugonga mwamba. Si Luis Suarez kama wengi walivyodhani, bali alikuwa ni Jose Gimenez aliyezamisha jahazi la Misri katika dakika ya 90 alipouweka mpira nyavuni kwa kichwa kutoka mpira wa adhabu uliopigwa na Carlos Sanchez.

Mohammad Salah, kiungo nyota wa Misri anayeichezea Liverpool

Misri watakuwa tena uwanjani saa tatu usiku siku hiyo dhidi ya wenyeji Urusi. Mwakilishi mwingine wa Nigeria, au ukipenda Super Eagles ilisagwasagwa mabao 2-0 na Croatia katika mechi ya Kundi D.

Mbali na Morocco, Misri na Nigeria, timu nyingine zinazoliwakilisha bara Afrika ni Senegal na Tunisia. Katika mechi ya Kundi C, Ufaransa iliilaza Australia mabao 2-1 baada ya bao la Paul Pogba kuvuka mstari. Katika uwanja wa Spartak mjini Moscow, taifa ndogo la Iceland liliwashangaza wengi baada ya kucheza kufa kupona dhidi ya Argentina. Lionel Messi alinyimwa bao la penalti na kipa wa Iceland Hannes Halldórsson ambaye aliishia kutuzwa mchezaji bora wa mechi. Refa kutoka Poland Szymon Marciniak aliipa Argentina penalti dakika ya 63 baada ya Maximiliano Meza kulazwa na Rurik Gislason. Ingawa Aguero ailiiweka Argentina kifua mbele dakika ya 19, bao lake lilifutwa na Alfred Finnbogason dakika chache baadaye. Siku iliisha na mechi ya Kundi D kati ya Croatia na Nigeria. Makosa ya mabeki yalipelekea Nigeria kulazwa 2-0 na kuninginia mkiani. Timu hiyo imesalia na kibarua kigumu kwani ndio timu pekee bila alama katika kundi hilo. Kwengineko miamba ya soka Brazil ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Uswisi huku wafuatiliaji wa soka wakibakia midomo wazi baada ya Ujerumani kutandikwa bao moja la uchungu bila jibu na Mexico.

Dondoo za Kombe la Dunia

Waziri wa Vita wa Utawala wa Kizayuni wa Israel ametoa matamshi ya kijinga sana kumuhusu nyota wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi baada ya timu yake kutoka sare na Iceland katika kombe la dunia nchini Russia. Katika mechi hiyo ya Jumamosi, Messi alikosa mkwaju wa penalti na hatimaye timu hizo mbili zikatoka sare ya bao moja kwa moja na hivyo Argentina ikapata pointi moja. Kufuatia matokeo hayo, Waziri wa Vita wa Utawala wa Kizayuni wa Israel Avigdor Lieberman ametoa matamshi ya kijinga kumhusu Messi na kusema: "Iwapo Argentina ingecheza mechi ya kirafiki na Israel, Messi angekuwa na uwezo bora zaidi katika kombe la dunia. Messi amepoteza penalti hiyo kwa sababu hakuwa amejitayarisha vya kutosha." Ikumbukwe kuwa kufuatia mashinikizo makubwa ya kimataifa na malalamiko makali ya Wapalestina na waungaji mkono wa ukombozi wa Palestina kote duniani, mechi ya kirafiki kati ya timu ya taifa ya Argentina na timu ya utawala wa Kizayuni iliyokuwa ichezwe Juni tisa nchini Cyprus ilifutiliwa mbali.

Mbali na hayo afisa mmoja wa Russia Andrei Ermak amewaonya mashabiki wa Nigeria kutoingia uwanjani na kuku au ni juju vile? Mashabiki hao wa Nigeria wameonywa na Waziri wa eneo la Kaliningrad anayehusika na Tamaduni na Utalii Andrei Ermak dhidi ya kubeba kuku ambao wako hai uwanjani wakati Super Eagles itakapokuwa ikicheza. Mabingwa hao mara tatu wa Afrika walianza kampeni ya kulisaka Kombe katika kundi D siku ya Jumamosi walipovaana na Croatia katika uga wa Kaliningrad, na kuzabwa bao 1-0.

Mieleka ya Viziwi: Iran yatwaa ubingwa Russia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Kimataifa ya Mieleka ya Freestyle ya wanamieleka wenye matatizo ya kusikia yaliyofanyika katika mji wa Vladimir nchini Russia. Iran imeibuka kidedea baada ya kuzoa jumla ya alama 193 katika kategoria mbalimbali. Wanamileka wa Iran wanaondoa Russia huku kapu lao likiwa limesheheni medali 5 za dhahabu, 1 ya fedha na 2 za shaba. Medali za dhahabu za Iran zilitwaliwa na wanamieleka bingwa Mohammad Siavoshi (57kg), Hossein Nouri (70kg), Hossein Darikvand (74kg), Mohsen Manouchehri (86kg) na Mohammad-Rasoul Qamarpour (92kg).

Timu ya mieleka ya Greco Roman ya Iran

Uturuki imeibuka ya pili licha ya kuwa na pointi 193 kama Iran, lakini imetwaa dhahabu nne. Mwenyeji Russia amefunga orodha ya tatu bora kwa kuzoa jumla ya alama 180. Juni 15, wanamieleka wa Iran mtindo wa Greco Roman waliibuka wa tatu baada ya kutia kibindoni medali 4 za fedha na 3 za shaba. Duruy ya 5 ya mashindano hayo ya dunia yanayofahamika kwa Kimombo kama World Deaf Senior Freestyle Wrestling Championships iling'oa nanga Juni 11 na kisha linafunga pazia lake Jumanne hii ya Juni 19.

Cecafa yakubali ombi la Yanga

Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limekubali maombi ya Yanga ya kujiondoa katika mashindano ya Kombe la Kagame baada ya kutuma barua iliyoeleza kuomba kujitoa Yanga ilituma barua kupitia TFF ikiomba kujiondoa ili kuwapa nafasi wachezaji wake mapumziko kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia FC ya Kenya. Barua hiyo ilieleza kuwa ratiba ya michuano imekuwa si rafiki kwao na itakuwa inawabana sababu wanapaswa kuwajibika kwenye mashindano ya shirikisho pia wachezaji wake wengi hawana mikataba. Kutokana na maombi hayo, CECAFA wamemua kuuwaalika Vipers SC ya Uganda kuchukua nafasi ya Yanga ambapo katika kundi C wataungana na Simba, Dakadaha ya Somalia na St. George ya Ethiopia.

Yanga uwanjani

 

Wakati huo huo, Mabingwa wa Ligi Kuu soka Tanzania, Simba wanatarajia kuanza maandalizi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuanzia wiki ijayo. Kwa sasa kikosi hicho kilichokuwa Kenya kwa michuano SportPesa Super Cup hivi karibuni, kimekwenda mapumziko kisha kitarejea kambini kuanzia Ijumaa kwa maandalizi ya michuano hiyo ya kikanda. Meneja wa Simba, Richard Robert alisema kikosi hicho kitakaporejea kitaanza kampeni zake za maandalizi ya ushiriki wa Cecafa kuhakikisha wanafanya vizuri.  

Mashirikisho ya Soka wanachama wa Cecafa

 

Michuano hiyo inayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28, mwaka huu, huku ikisubiriwa kwa hamu na klabu mbalimbali, ambazo zitatumia mashindano hayo kusajili na kupima wachezaji wao wapya.

……………………...TAMATI………………….