Jun 20, 2018 22:39 UTC
  • Alkhamisi tarehe 21 Juni 2018

leo ni Alkhamisi tarehe 7 Shawwal 1439 Hijria sawa na Juni 21, 2018.

Siku kama hii ya leo miaka 1436 iliyopita kulipiganwa vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina. Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika vita vya Badr walianzisha vita hivi vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa na zana kamili kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakiwa 700 tu. Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake juu ya namna atakavyopambana na Maquraishi na iliamuliwa kuwa, vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kuendelea kubakia mlimani, Waislanu hao walishuka mlimani kwa tamaa za kupata ngawira hali iliyowafanya washirikina kuwashambulia Waislamu na kudhoofika nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi wa moja kwa moja na hivyo wakalazimika kurejea Makka.

Picha ya eneo la vita vya Uhud

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Juni 1970, alifariki dunia Dakta Ahmed Sukarno mpigania uhuru wa Indonesia. Sukarno alizaliwa mwaka 1901, na alikuwa mstari wa mbele katika mapambano yake dhidi ya mkoloni Mholanzi nchini humo. Kwa minajili hiyo, Sukarno aliwahi kukamatwa na kufungwa jela miaka minne na utawala wa kikoloni wa Uholanzi. Baada ya kifungo hicho alitiwa tena mbaroni na kubaidishwa. Mnamo mwaka 1949 alichaguliwa kuwa rais wa Indonesia na ilipofika mwaka 1965 Ahmed Sukarno aliondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Janerali Suharto.

Dakta Ahmed Sukarno

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita inayosadifiana na tarehe 31 Khordad 1360 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 21 Juni mwaka 1981, aliuawa shahidi Dakta Mustafa Chamran, msomi na kamanda shujaa wa vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Dakta Chamran alifanikiwa kupata shahada katika fani ya elektroniki na kisha alielekea Marekani ambako alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu. Kwa miaka kadhaa Dakta Chamran alikuwa nchini Lebanon kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo waliokuwa wakipambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mara baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Dakta Chamran alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na kisha akawa mbunge wa Tehran. 

Dakta Mustafa Chamran

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, inayosadifiana na 31 Khordad 1369 Hijria Shamsia, mikoa ya Gilan na Zanjan iliyoko kaskazini na kaskazini magharibi mwa Iran ilikumbwa na mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7.3 kwa kipimo cha rishta, na kuleta maafa makubwa. Zaidi ya watu elfu hamsini walifariki dunia na wengine zaidi ya elfu sitini kujeruhiwa, na laki tano kukosa makaazi. Mtetemeko huo licha ya kuleta maafa kwa binadamu, ulisababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa wananchi na serikali, na hasa kwenye miundombinu.