Jun 25, 2018 07:05 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Juni 25

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita, haswa matokeo ya michuano ya Kombe la Dunia Russia.....

Iran yang'ara Voliboli, yaziadhibu Korea, Bulgaria na Ujerumani

Timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumapili ilishuka uwanjani kutoana udhia na Ujerumani, katika mashindano ya kimataifa yanayofahamika kama Volleyball Men's Nations League yanayosimamiwa na Shirikisho la Voliboli Duniani FIVB. Wachezaji wa Iran waliendeleza wimbi la ushindi kwa kuwatandika Wajerumani seti 3-2 za (25-20, 23-25, 25-22, 22-25, 15-11). Wachezaji nyota wa Iran Milad Ebadipour na Morteza Sharifi waliongoza kikosi cha Iran kuibamiza Ujerumani wasijue la kufanya.

Iran dhidi ya Ujerumani

 

Chini ya kelele za kushangiliwa na mashabiki wa nyumbani katika Ukumbi wa Michezo wa Azadi hapa Tehran, wanavoliboli wa Iran waliutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa na kuupa maana msemao, mcheza kwao hutuzwa.

Awali timu hiyo iliicharaza Bulgaria seti 3-1 za (25-22, 25-15, 23-25 na 25-14) siku ya Jumamosi. Aidha timu hiyo ya voliboli ya Iran iliisasambua Korea Kusini seti 3-1 za (27-25, 23-25, 25-22, 25-23) siku ya Ijumaa katika Ukumbi wa Michezo wa Azadi magharibi mwa Tehran. Mashindano hayo yalianza Mei 25 na yanatazamiwa kumalizika Julai 8. Timu 16 zilizogawanywa katika makundi manne zitacheza jumla ya mechi 120, ambapo timu 4 bora zitavaana katika hatua ya mwisho ya mashindano hayo.

Wanariadha wa Iran wazoa medali lukuki Tunisia

Wanariadha wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali kochokocho katika Duru ya 12 ya Riadha ya Walemavu huko nchini Tunisia. Ijumaa ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya mashindano hayo yanayofahamika kwa Kimombo kama 12th Tunis International Meeting, Africa's Grand Prix of the Year, wanariadha wa Iran walizoa jumla ya medali 6, zikiwemo 3 za dhahabu.

Wanariadha walemavu wakiwemo wa Iran mjini Tunis

Wanariadha 20 wa Iran wameshiriki mashindano hayo katika michezo 12 tofauti huko Tunis, mji mkuu wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Miongoni mwa Wairani waliobuka kidedea na kushinda dhahabu ni Eshrat Kordestian katika mchezo wa kurusha kitufe (Shot put), na Davoud Ali Ghasemi aliyeshinda mbio za mita 100.

Dondoo za Kombe la Dunia

Juni 20, timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliambulia kipigo cha goli 1-0 kutoka Hispania katika mchuano mwingine wa aina yake wa fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea kufukuta nchini Russia. Goli pekee la Hispania katika mchezo huo lilifungwa na Diego Costa kunako dakika ya 54.

Mechi ya Iran na Uhispania

 

Hata hivyo Hispania ambayo ni katika miamba ya soka duniani ilitazamiwa kupata magoli mengi katika mchezo huo lakini vijana wa Iran walidhibiti mambo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei ni miongoni mwa viongozi wa Iran waliotuma jumbe jumbe za pongezi kwa wanasoka wa Iran kwa kuonesha mchezo mzuri wa kujituma licha ya kukubali kushindwa na Hispania. Kabla ya hapo Iran iliibuka mshindi wa bao moja kwa nunge katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia iliposhuka dimbani kuvaana na Morocco. Mchuano wa Jumatatu wa Iran na Ureno utaamua iwapo vijana wa Team Melli watasonga mbele kwenye Hatua ya 16 Bora ya mashindano hayo ya dunia au la.

Senegal dhidi ya Japan

 

Mbali na hayo, mwakilishi wa Afrika katika mashindano hayo ya dunia, timu ya Senegal iliilazimisha Japan sare ya kufungana mabao 2-2 siku ya Jumapili katika mchuano wa kusisimua wa Kundi H. Sadio Mane ambaye pia anakipiga katika klabu ya Liverpool aliifungia Senegal bao la kwanza kunako dakika ya 11, baada ya kipa wa Japan kufanya uzembe.

Hata hivyo Takashi Inui alifanya mambo kuwa 1-1 baada ya kuifungia Japan katika dakika ya 34. Moussa Wague aliifungia timu hiyo ya Afrika Magharibi bao la pili kunako dakika ya 71, lakini ushindi huo haukudumu, kwa vijana wa Japan walijitutumua na kusawazisha kupitia kiungo Keisuko Honda dakika saba baadaye. Kwa sare hiyo, Senegal watalazimika kusubiri matokeo ya mechi yao ya mwisho ya makundi ili kujua iwapo itatinga Hatua ya 16. Sare yoyote itawatosheleza vijana hawa wa Kiafrika.

Kiungo nyota wa Nigeria, Ahmed Musa akishangilia bao

 

Kwengineko, timu ya taifa ya Nigeria baada ya kupokea kipigo chake cha kwanza katika mchezo wao dhidi ya Croatia kwa magoli 2-0, ilicheza mchezo wake wa pili dhidi ya Iceland, na kufanikiwa kupata ushindi wa magoli 2-0. Kiungo wa Nyota wa Leicester City Ahmed Musa ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo huo kufunga magoli yote mawili katika dakika ya 48 na 74 kutokana na kuwa na utulivu katika eneo la hatari na kuzitumia nafasi zote mbili kwa ufasaha.

Ushindi huo sasa unawaweka pazuri Nigeria na kuwapa imani Argentina kuwa wanaweza kufuzu hatua ya 16 bora kwani kufuzu kwa Argentina na Nigeria kutatokana na timu zote mbili kupata ushindi zitakapo kutana Juni 26 ila Nigeria hata sare inamvusha hatua inayofuata. Croatia tayari amefuzu Hatua ya 16 kutokana na kupata ushindi mechi mbili na kuwa na point 6, wakati Nigeria wao wapo nafasi ya pili kwa kuwa na point tatu, Iceland nafasi ya tatu kwa kuwa na point moja sawa na Argentina walio nafasi ya nne kwa kutofautiana magoli ya kufungwa.

Ufaransa ilipocheza na Australia

 

Huku hayo yakijiri, timu ya taifa ya Ufaransa nayo imefanikiwa kusonga Hatua ya 16 ya Kombe la Dunia ikiwa na mchezo mmoja mkononi baada ya kuifunga Peru bao 1-0 Alkhamisi. Ufaransa ikiongozwa na mastaa kadhaa akiwemo Paul Pogba, ilipata ushindi huo licha ya mchezo kuwa mgumu ambapo mfungaji alikuwa Kylian Mbappe katika dakika ya 34 akimalizia kazi nzuri ya Pogba na Olivier Giroud. Kwa matokeo hayo, Ufaransa imefikisha pointi 6 na kuongoza Kundi C ikifuatiwa na Denmark yenye pointi 4, zote zikisaliwa na mchezo mmoja. Mchezo wa Peru ulikuwa mgumu hasa kipindi cha pili ambapo vijana hao walikuwa na makali na kuwapa wakati mgumu Ufaransa. Katika mchezo wa mapema, Denmark na Australia zilitoka sare ya bao 1-1, huku mshambuliaji wa Denmark mwenye asili ya Tanzania, Yussuf Poulsen akipata kadi ya njano kwa kuunawa mpira ndani ya boksi na hivyo kutakiwa kuukosa mchezo wa mwisho wa Hatua ya Makundi kwa kuwa ana kadi mbili za njano.

Kwengineko timu ya taifa ya soka ya Croatia Juni 21 iliidhalilisha Argentina na nyota wake mkubwa, Lionel Messi, baada ya kuichabanga magoli matatu kwa sifuri katika uwanja wa Nizhny Novgorod. Matokeo hayo yameipatia timu ya taifa ya Croatia tiketi ya kuingia duru ya pili ya mashindano hayo yanayoendelea nchini Russia. Hii ni mara ya kwanza wa timu ya taifa ya soka ya Croatia kufanikiwa kuingia duru ya pili ya Kombe la Dunia katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Juni 23 Tunisia ilisagwasagwa na Ubelgiji mabao 5-2 katika mchezo wa Kundi G.

WHO: Watoto wasiachwe waogelee kwenye 'video games'

Shirika la Afya Duniani (WHO) limewaonya wazazi dhidi ya kuwaacha wanao waogelee katika michezo ya tarakilishi na rununu almaarufu video games. Ripoti mpya ya WHO inasema michezo hiyo inadhoofisha uwezo wa watoto kutafakuri na yumkini ikawasababishia matatizo ya akili wakiicheza kupindukia. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, WHO imesema kuwa video games zinaathiri asilimia tatu ya wachezaji wake waliokubuhu. WHO imesema waraibu wa michezo hiyo huachana na shughuli zao za kawaida ili kucheza michezo hiyo, kwani wasipofanya hivyo, huonekana wanyonge wadhaifu.

"Blue whale" ni moja ya michezo maarufu ya video game

 

Baadhi ya watoto hupakuwa michezo hii katika simu za rununu na kutumia muda wao mwingi kuicheza, badala ya kufanya mambo ya msingi kama kusoma au kusaidia kazi za nyumbani. Michezo hii haijawa na taathira hasi kwa watoto tu. Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, zaidi ya watu bilioni mbili duniani wanacheza michezo hiyo.

Watoto wadogo, wahanga wakuu wa michezo ya tarakilishi na rununu

 

Shirika la WHO limesema kwamba sababu ya kuorodhesha michezo hiyo ya video games kama inayochangia ugonjwa wa akili ni kuhamasisha watu kuhusu hatari ya kucheza kwa kupitiliza michezo hiyo.

…………………….TAMATI.……………….