Jun 25, 2018 07:53 UTC
  • Jumatatu tarehe 25 Juni, 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 11 Shawwal 1439 Hijria sawa na tarehe 25 Juni 2018.

Tarehe 11 Shawwal miaka 1442 iliyopita Mtume Muhammad (S.A.W) alielekea katika mji wa Twaif karibu na Makka kwa lengo la kuwalingania Uislamu watu wa kabila la Thaqif. Safari hiyo ya Mtume mtukufu ilifanyika katika kipindi ambacho alikuwa ameondokewa na ami yake na mlezi wake kipenzi Abu Twalib, jambo lililowafanya Maquraishi wa Makka wazidishe maudhi na manyanyaso dhidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) na wafuasi wake. Hivyo ilitarajiwa kuwa, iwapo wakazi wa Twaif wangekubali Uislamu, mji huo ungeweza kuwa kituo na makazi salama kwa Waislamu waliokuwa wakidhulumiwa wa Makka. Hata hivyo viongozi wa kabila la Thaqif sio tu kwamba hawakumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja na risala ya Mtume Muhammad (S.A.W), bali pia baadhi ya watu wa kabila hilo walimfanyia maudhi, dhihaka na kumjeruhi Mtume mtukufu.

Ramani ya Twaif

Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita kundi la watumwa wa Marekani wenye asili ya Afrika ambao waliachiwa huru na wamiliki wao wazungu wa nchi hiyo, walirejea Afrika na kuanzisha makazi katika ardhi ambayo leo hii inajulikana kama Liberia. Raia hao weusi wa Marekani walianzisha harakati ya ukombozi mwanzoni mwa karne ya 19 kwa lengo la kujiondoa utumwani na kuunda nchi yao. Kwa sababu hiyo kundi la Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika lilihamia Magharibi mwa Afrika na kuasisi nchi ya Liberia kwa kusaidiwa na taasisi ya wahamiaji, baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi huko Marekani. Awali Liberia ilikuwa ikiendeshwa kama moja ya majimbo ya Marekani, lakini mwaka 1847 nchi hiyo iliasisi mfumo wa jamhuri na rais wake wa kwanza akawa Joseph Roberts, mtumwa kutoka jimbo la Virginia.

Bendera ya Liberia

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, yaani tarehe 25 Juni mwaka 1975, Msumbiji ilipata uhuru. Mwishoni mwa karne ya 15 kundi moja la mabaharia wa Kireno likiongozwa na mvumbuzi mashuhuri Vasco da Gama lilifika Msumbiji na kuanzia hapo mabaharia hao wakaanza kuikoloni nchi hiyo, ukoloni ambao uliendelea kwa karne tano. Wareno walianza kupora maliasili na utajiri wa Msumbiji na makumi ya maelfu ya wananchi wapigania ukombozi wa Msumbiji waliuawa wakitetea nchi yao.

Bendera ya Msumbiji

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita yaani tarehe 4 Tir 1367 Hijria Shamsiya, ndege za utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq, kwa mara nyingine tena ziliwashambulia kwa mabomu ya kemikali wapiganaji wa Kiirani waliokuwa katika visiwa vya Majnun. Mamia ya wanajeshi wa Iran waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Saddam. Utawala wa zamani wa Iraq ulitumia silaha za maangamizi ya umati za kemikali tangu mwanzoni mwa vita vyake dhidi ya Iran mwaka 1359 Hijria Shamsiya, na kuzidisha matumizi ya silaha hizo sambamba na ushindi wa wapiganaji wa Iran.

Mashambulizi ya mabomu ya kemikali

 

Tags