Jun 29, 2018 07:45 UTC
  • Ijumaa tarehe 29 Juni, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 15 Shawwal 1439 Hijria sawa na Juni 29, 2018.

Siku kama ya leo miaka 1187 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 252 Hijria, alifariki dunia Abdul-Adhim Hassani. Mtukufu huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW kupitia shajara ya Imam Hassan Al-Mujtaba (AS). Abdul-Adhim al Hassani alikuwa mashuhuri sana kwa karama zake nyingi. Maimamu watukufu walithibitisha ukweli na uchamungu wake na walikuwa wakinukuu hadithi kutoka kwake. Baada ya kushadidi dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bani Abbas, Abdul-Adhim al Hassani alilazimika kuhajiri na kuhamia mjini Rey kusini mwa Tehran ya leo. Mtukufu huyo anajulikana pia kama shahidi ambaye aliuawa kwa kupewa sumu. Haram Tukufu ya Abdul-Adhim Hassani ipo katika mji wa Rey na wapezi wa Ahlul Bayt AS kutoka kona mbalimbali za dunia humiminika katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kufanya ziara.

Haram ya Abdul Adhim al Hassani, Rey

Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita aliaga dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Miaka 105 iliyopita vilianza vita vya pili vya Balkan kati ya Bulgaria na muungano wa nchi za Serbia, Ugiriki, Montenegro, Romania na utawala wa Kiothmania. Bulgaria, Serbia, Ugiriki na Montenegro ambazo zilikuwa chini ya mamlaka ya Othmania karibu mwaka mmoja kabla ya hapo zilifanya uasi dhidi ya utawala huo na kufanikiwa kujikomboa kutokana na udhaifu wa watawala wa Kiothmania.

Vita vya pili vya Balkan

Miaka 42 iliyopita katika siku inayosadifiana na tarehe 29 Juni mwaka 1976, muungano wa visiwa vya Ushelisheli ulipata uhuru na kila inapowadia siku kama hii husherekewa visiwani humo kama siku ya taifa. Hadi kufikia katikati ya karne 18, wakati ambapo Wareno walikuwa wakiikalia kwa mabavu ardhi hiyo, visiwa vya Sychelles vilikuwa havijagunduliwa na havikuwa na watu wakazi. Kuanzia wakati huo Ufaransa nayo ikaanza kupenyeza nchini humo. Mwishoni mwa karne ya 18 wakati kulipopamba moto mapinduzi ya Ufaransa, wanajeshi wa Uingereza waliokuwa katika eneo la Afrika walivamia Ushelisheli. Mapambano ya kuikomboa nchi hiyo yalipamba moto tangu mwaka 1960 na kuendelea, na miaka 16 iliyofuata visiwa vya Ushelisheli au Sychelles vikapata uhuru na kuasisi mfumo wa Jamhuri. Ushelisheli inaundwa na visiwa kadhaa vilivyoko katika bahari ya Hindi huku ikipakana kwa karibu na jirani yake Madagascar.

Visiwa vya Ushelisheli