Jul 02, 2018 08:10 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Julai 2

Ufuatao ni ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita, yakiwemo matokeo ya michuano ya Kombe la Dunia Russia.....

Upigaji makasia: Iran yazoa medali 4

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ya kupiga makasia yaliyofanyika katika mji wa Chungju nchini Korea Kusini, ambapo wachezaji wake wamezoa medali 4 zikiwemo 3 za dhahabu. Dhahabu ya kwanza ya Iran ilitwaliwa na Mohsen Shadi, baadaya kuibuka kidedea katika fainali ya upigaji makasia kwa upande wa wanaume wenye uzani mzito, kwa kutumia dakika 7 na sekunde 8 na nukta 9. Medali nyingine za dhahabu za Iran zilizolewa na Reza Ghahremani katika kategoria ya mtu mmoja na Milad Allahverdian na Shirzad Ghaderi katika kategoria ya watu wawili.Kikosi cha cha wanawake cha upigaji makasia cha Iran kiliibuka ya pili na kutunukiwa medali ya fedha. Wanadada hao wa Iran ni pamoja na Asra Javanmardi, Kimiya Zarei, Forough Aghabalazadeh na Haniyeh Bidad.

Timu ya wanawake wa Iran ya mchezo wa kupiga makasia

 

Mashindano hayo yanayofahamika kwa Kimombo kama 2018 Asian Rowing Junior Championships yalianza Juni 26 na kufunga pazia lake Jumamosi ya Juni 30.

Basketboli: Iran yaibamiza Qatar

Timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibaiza Qatar vikapu 77 kwa 75 katika mchezo wa kusaka tiketi za kushiriki Kombe la Dunia la mchezo huo mwaka 2019. Katika kitutimu hicho cha Ijumaa katika Ukumbi wa Michezo wa Al Gharafa, vijana wa Iran waliutawal mpira wakiongozwa na kiundo wa safu ya katikati Hamed Ehadadi.

Timu ya mpira wa kikapu ya Iran

 

Vijana wa Qatar waliofanya timu yao ing'are liche ya kuchachawizwa na Iran ni Clinton Johnson, Mohamed Yousuf Mohammed na Mansour Elhadary.  Kocha wa Qatar, Tim Lewis amesema ingawaje timu yake ilionyesha mchezo mzuri pia, lakini waliruhusu alama tano ziwaponyoke na kubadilisha kabisa muundo wa mchuano. Iran inatazamiwa kuvaana na Kazakhstan katika mchezo mwingine wa Kundi D hapa mjini Tehran, huku Qatar ikitoana udhia na Iraq. Timu tatu bora katika kila kundi zitatinga fainali za Kombe la Dunia zinazosimamiwa na Shirikisho la Basketboli Duniani FIBA.

Kilio cha Cecafa huku Kombe la Kagame likianza

Huku michuano ya soka ya Ligi ya Mabingwa Afrika Mashariki na Kati, (Kombe la Kagame) ikianza Ijumaa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Baraza la vyama vya soka ukanda huo, Cecafa, Nicholus Musonye amesema viongozi wa vyama wanachama wanahujumu. Akizungumza na waandishi wa habari Musonye alisema wamejiandaa vizuri kufanikisha michuano hiyo itakayomalizika Julai 13, lakini hakusita kuweka wazi dukuduku lake kuwa viongozi wa vyama wanachama ndio wanaohujumu mashindano hayo kwa kuweka nguvu kwenye mashindano yenye fedha nyingi na kuacha kusapoti kazi ya kukuza michezo katika ukanda wao hali inayofanya kudorora.

CECAFA

 

Pia Musonye alisema yeye amehudumu kwa muda mrefu kwenye Cecafa kama Katibu Mkuu lakini akitakiwa kuondoka ili waweke mtu mwingine yeye yupo tayari. Yanga na St George ya Ethiopia ndizo zilizojitoa kwenye michuano hiyo zikidai kutaka muda wa kujiandaa zaidi na michuano ya Afrika. Kaimu Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani alisema wamejiandaa ipasavyo kukamilisha michuano hiyo ya Kombe la Kagame. Baadhi timu zinazoshiriki michunao hiyo ya kikanda ni JKU ya Zanzibar, Vipers ya Uganda, Azam FC ya Tanzania, Kator ya Sudan Kusini Singida United ya Tanzania na APR ya Rwanda.

Dondoo za Kombe la Dunia

Timu za taifa za soka za Ureno na Argentina zimeyaaga mashindano ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Russia baada ya kupoteza michezo yao ya kuwania tiketi ya robo fainali. Argentina ikiongozwa na nahodha wake Lionel Messi imetupwa nje ya mashindano hayo baada ya kubamizwa mabao 4-3 na timu kali ya Ufaransa. Argentina ambayo tangu yaanze mashindano ya hayo haijaonyesha makeke ilijitutumua lakini ilijikuta ikiyaaga mashindano hayo mbele ya Ufaransa ambayo ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi ya kutwaa kombe hilo. Kijana chipukizi na machachari Kylian Mbappe ndiye aliyekuwa mwiba kwa Argentina baada ya kupachika mabao mawili peke yake na kumfanya Messi na wenzake wayaage mapema mashindano hayo.

Messi na Ronaldo, miamba ya soka ya Argentina na Ureno

 

Masaa machache baadaye Ureno ikiwa na nahodha wake Cristiano Ronaldo ikaingia msambweni kupepetana na timu ngumu ya Uruguay iliyokuwa ikiongozwa na wachezaji machachari kama Edson Cavani na Luis Suarez. Uruguay imeitupa nje Ureno baada ya kuitandika mabao 2-1. Edson Cavani ndiye aliyepeleka habari ya msiba Ureno baada ya kutikisa nyavu mara mbili.

Ufaransa sasa itapambana na Uruguay katika mechi ya robo fainali kuwania tiketi ya nusu fainali. Mwenyeji Russia pia ietinga robo fainali baada ya kuisasambua Uhispania mabao 4-3 katika upigaji penati, baada ya timu hizo kutoa sare ya baoa 1-1 katika dakika 120 za ada na nyongeza Jumapili. Russia ilijifunga bao la kisigino kunako dakika ya 12, baada ya mchezaji wake Sergei Ignashevich kufanya masikhara. Hata hivyo Artem Dzyuba alifanya ngoma kuwa draw, ka mkwaju wa penati, baada ya Gerard Pique kuunawa mpira kwenye sanduku la hatari. Kipa wa Russia ndiye aliyeonekana nyota wa mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa Luzhniki mjini Moscow, kwa kuzuia mabao mengi ikiwemo kuudaka mpira wa penati.

Timu ya taifa ya soka ya Russia

 

Aidha Croatia imetinga robo fainali kwa kuibuka kidedea kwenye mikwaju ya penati, baada ya mechi yake dhidi ya Denmark kuishiakwa sare ya bao 1-1, Jumapili katika Uwanja wa Nizhny Novgorod.

………………….TAMATI……………….