Jul 31, 2018 22:20 UTC
  • Jumatano tarehe Mosi Agosti 2018

Leo ni Jumatano tarehe 18 Dhulqaada 1439 Hijria sawa na tarehe Mosi Agosti 2018.

Tarehe Mosi Agosti ni siku ya kimataifa ya Maziwa ya Mama. Utumiaji mkubwa wa maziwa ya kopo na vyakula vya watoto vilivyotengenezwa viwandani ulilikithiri sana baada ya Vita vya Pili vya Dunia hususan katika nchi zilizostawi na suala hilo limezidisha wasiwasi wa jamii ya kimataifa. Hivyo suala la kunyonyesha watoto kwa maziwa ya mama na kuzidisha uelewa wa umma kuhusu faida kubwa na za aina yake za maziwa ya mama kwa mtoto na katika usalama na afya yake lilihitajia kuchukuliwa hatua kubwa na za kimsingi. Kwa msingi huo Shirika la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) tarehe Mosi Agosti mwaka 1990 ziliitisha mkutano katika wa Florence nchini Italia na kutia saini taarifa iliyosisitiza udharura wa kudumishwa, kutangaza na kusisitiza suala la kuwalisha watoto wadogo kwa maziwa ya mama. Taarifa hiyo ilitilia mkazo umuhimu wa mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama katika kipindi cha miezi sita ya awali ya maisha yake na taathira yake kubwa kwa afya ya mtoto na mwama.

Siku ya Maziwa ya Mama Duniani

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Kiislamu Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa. Ayatullah Kashiful Ghitaa alizaliwa katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya wasomi na wacha-Mungu na kuanza kutafuta elimu akiwa bado mtoto mdogo. Baada ya kukamilisha elimu ya msingi, Ayatullah Kashiful Ghitaa alihudhuria darsa za maulamaa wakubwa wa zama hizo na kukwea daraja za juu za elimu katika kipindi kifupi. Alifanikiwa kulea wasomi na maulamaa wakubwa na kufanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu pia alikutambua kushiriki katika masuala ya kisiasa na kutilia maanani masuala ya serikali na utawala kuwa ni katika mambo ya wajibu na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha Harakati ya Kitaifa ya Iraq. Ayatullah Kashiful Ghitaa alishiriki vilivyo katika mapigano ya jihadi ya wananchi wa Iraq wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya jeshi vamizi la Uingereza. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.

Ayatullah Kashiful Ghitaa

Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Benin ilipata uhuru kutoka kwa Ufaransa. Wafaransa walianza kuingilia masuala ya kisiasa na kiuchumi ya Benin katika nusu ya pili ya karne ya 19 na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo mwaka 1892. Ufaransa iliendelea kuikoloni Benin hadi mwaka 1958 na hatimaye mwaka 1960 katika siku kama ya leo nchi hiyo kajipatia uhuru. 

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, mkutano wa wakuu wa Urusi ya zamani, Marekani na Canada na nchi za Ulaya isipokuwa Albania ulianza huko Helsinki mji mkuu wa Finland. Mkutano huo ambao ulipewa jina la Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya ulifanyika kwa lengo la kuondoa mivutano kati ya nchi za kambi ya Mashariki chini ya uongozi wa Urusi ya zamani na kambi ya Magharibi chini ya uongozi wa Marekani. Hata hivyo mkutano huo wa usalama na ushirikiano haukuwa na mafanikio muhimu katika kuzikurubisha pamoja kambi mbili hizo hasa kufuatia uvamizi uliofanywa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani nchini Afghanistan mwaka 1979. 

Mkutano wa Usalama na Ushirikiano Ulaya

Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, mwafaka na tarehe Mosi Agosti mwaka 2005, Fahd bin Abdulaziz Mfalme wa zamani wa Saudi Arabia alifariki dunia baada ya kuugua kwa miaka mingi. Mfalme Fahd alizaliwa mwaka 1921 huko Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia. Mwaka 1967, Fahd bin Abdulaziz alikuwa Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo na miaka minane baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1982 akiwa mfalme wa tano wa silsila ya Al-Saud baada ya kufariki dunia kaka yake, Khalid bin Abdulaziz. Wakati wa vita vya kichokozi vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Mfalme Fahd alikuwa akimuunga mkono dikteta Saddam.

Fahd bin Abdulaziz