Jumatano, 22 Agosti, 2018
Leo ni Jumatano tarehe 10 Dhul-Hijja mwaka 1439 Hijria, sawa na tarehe 22 Agosti mwaka 2018.
Leo tarehe 10 Dhilhaj ni sikukuu ya Idul Adh'ha, moja ya sikukuu kubwa za Kiislamu. Katika siku hii mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu waliokwenda Makka, huchinja mnyama kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mola wao na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii Mtukufu Ibrahim (as). Mwenyezi Mungu aliijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumwamuru amchinje mwanawe kipenzi Ismail (as). Licha ya mashaka ya utekelezwaji wa amri hiyo, Nabii Ibrahimu (as) aliandaa mazingira ya kutekeleza amri hiyo na kumlaza chini mwanaye na kuanza kuikata shingo yake lakini kisu kilikataa kuchinja. Hapo ndipo alipoambiwa na Mwenyezi Mungu kuwa amefaulu mtihani huo na akamtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanaye Ismail. Tukio hili lenye ibra na mafunzo tele linawapa wanadamu somo la kujitoa mhanga, kujisabilia kwa ajili ya Allah, kushinda matamanio na matakwa ya nafsi na kusalimu amri mbele ya amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii kubwa.

Miaka 391 iliyopita katika siku kama ya leo, vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa. Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle. Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kutekwa La Rochelle.

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita katika siku kama ya hii ya leo Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani. Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada kubwa ilimuwezesha kuendeleza masomo yake ya fizikia hadi chuo kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni. Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kiliweza kurusha mawimbi ya televisheni katika umbali wa mita 30 na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine.

Na tarehe 10 Dhulhija miaka 3 iliyopita katika sikukuu ya Idil Adh'ha ardhi tukufu ya Mina huko Saudi Arabia ilikuwa machinjio ya maelfu ya mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kutokana na azembe wa maafisa na wasimamizi wa Hija wa Saudia. Siku hiyo ilishuhudia tukio baya zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 3 asubuhi wakati baadhi ya mahujaji walipokuwa wakielekea eneo la Jamarat kumpiga mawe Shetani. Ghafla maafisa wa Saudi Arabia walifunga barabara za kuelekea eneo hilo na kukatokeo msongamano mkubwa kupita kiasi wa maelfu ya mahujaji, suala lililosababisha vifo vya zaidi ya mahujaji 7 kutoka nchi mbalimbali duniani. Mahujaji 464 wa Iran pia waliaga dunia katika tukio hilo ambazo lilidhihirisha tena uzembe na kutokuwa na uwezo wa kusimamia vyema ibada ya Hija wa serikali ya Saudia.
