Aug 26, 2018 02:25 UTC
  • Jumapili  26 Agosti

Leo ni Jumapili  tarehe 14 Dhul-Hijjah 1439 Hijria, sawa na tarehe 26 Agosti, 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1311 iliyopita alizaliwa Imam  Mussa al-Kadhim (as) ambaye ni mmoja kati ya wajukuu watukufu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Alilelewa na baba yake Imam Ja'far Swadiq (as) na kupata elimu na maarifa ya Kiislamu kutoka kwa mtukufu huyo kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Kadhim (as) alishika hatamu za Uimamu na uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35 na kukabiliana na mashaka mengi. Imam Kadhim (as) alipitisha kipindi kikubwa cha umri wake katika kuwazindua na kuwaelimisha Waislamu maarifa asili ya dini. Suala hili liliwatia hofu kubwa watawala wa Bani Abbas ambao walimkamata na kumfunga jela ili kumuweka mbali na Waislamu waliokuwa na kiu ya maarifa halisi ya dini yao. Imam Kadhim (as) alisifika kwa ukarimu mkubwa, uvumilivu na usamehevu. Tunatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kuadhimisha siku hii muhimu ya kuzaliwa mtukufu huyo.

Siku kama ya leo miaka 672 iliyopita, mzinga mkubwa ulitumika kwa mara ya kwanza katika historia. Siku hiyo jeshi la Uingereza lilitumia silaha ya mzinga dhidi ya askari wa Ufaransa. Katika vita hivyo Mfalme Philip wa Sita wa Ufaransa alishindwa vibaya na jeshi la Uingereza licha ya kwamba jeshi la Ufaransa lililokuwa lmekaribia kupata ushindi, lilikuwa na idadi kubwa ya askari na wapiganaji. Ushindi wa jeshi la Uingereza katika vita hivyo ulitokana na utumiaji wa silaha ya mzinga.

Aina ya mizinga

Siku kama ya leo miaka 275 iliyopita, alizaliwa mjini Paris Antoine Laurent Lavoisiere, mtaalamu wa kemia wa Kifaransa. Baada ya kumaliza masomo yake alianza kufanya utafiti katika elimu ya kemia. Miongoni mwa uvumbuzi wa msomi huyo ni kwamba, maji yanaundwa na vitu viwili yaani gesi za oksijeni na haidrojeni na mchango wa hewa ya oksijeni katika kuchomeka vitu mbalimbali. Mwaka 1794 Antoine Laurent Lavoisiere alituhumiwa kuwa anapinga mapinduzi na kunyongwa hapo baadaye.

Antoine Laurent Lavoisiere

Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, askari wa utawala wa Othmania walianza kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia. Waturuki wa Kiothmania walifanya mauaji hayo kwa kisingizio kwamba Waarmenia waliwasaidia Wagiriki katika ghasia zilizofanyika dhidi ya utawala wa Othmania. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wadogo wa Kiarmenia waliuawa kwa umati katika mauaji hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tano.

Mauaji ya umati yaliyofanywa na askari wa Othmania dhidi ya Waarmenia

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shahrivar 1358 Hijria Shamsia, Mahdi Iraqi na mwanawe Hissam waliuawa shahidi na magaidi wa kundi la Munafiqin. Mahdi Iraqi alikuwa mmoja wa shakhsia watajika wa Mapinduzi ya Kiislamju ya Iran na aliendesha mapambano kwa miaka kadhaa dhidi ya utawala wa shah na alikuwa na uhusiano wa karibu na Imam Khomeini MA. Mwanamapambano huyo muumini kwa miaka kadhaa alifungwa jela na utawala wa Shah na kukumbana na mateso mengi.

Mahdi Iraqi akiwa na Imamu Khomeini (MA)

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Wakati Saddam alipotumia silaha za kemikali kuua watu kwa halaiki

Na siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani, alimu mkubwa wa Waislamu. Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani alizaliwa mwaka 1285 Hijiria katika moja ya vijiji vya mji wa Zanjan nchini Iran. Awali alisoma kwa baba yake elimu ya dini na kidha akaelekea mjini Tehran kwa wasomi wakubwa wa zama hizo ambapo alifanikiwa kufikia daraja ya Ijtihad. Baada ya kufikia elimu ya juu katika dini alianza kazi ya kufundisha. Aliandika vitabu kadhaa juu ya sheria za Kiislamu ambavyo ni 'Kitaabul-Ijaarah' na 'Dhakhaairul-Ummah.' Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 75 huku akiwa ni marjaa wa Waislamu wa mji wa Zanjan.

Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani

 

Tags