Oct 01, 2018 08:36 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Okt 1

Ufuatao ni ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita, yakiwemo matokeo ya Debi la Kariakoo na Debi la Sarkhobi

Voliboli ya Ufukweni: Iran yaibuka ya pili Thailand

Timu ya taifa ya voliboli inayochezwa ufuoni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili katika mashindano ya bara Asia ya mchezo huo yaliyofanyika nchini Thailand. Katika mchezo wa fainali uliopigwa siku ya Ijumaa katika mkoa wa Satun ulioko kusini mwa Thailand, timu hiyo ya wanaume ya Iran ambaye iliingia uwanjani kama bingwa mtetezi, ilishindwa kufurukuta mbele ya Qatar na kukubali kuzabwa seti 2-0 za (21-18, 21-11), katika mashindano hayo ya mabingwa wa voliboli yanayofahamika kwa Kiingereza kama Asian Senior Beach Volleyball Championships. Qatar iliingia uwanjani ikijiamini, ikitiliwa maanani kuwa iliibuka kidedea pia katika fainali za Michezo ya Asia ilipovaana na Indonesia.

Voliboli ya ufuoni

 

Katika safu ya wanawake, Australia ilitwaa ubingwa baada ya kuipeleka mchakamchaka China, na kuitandika seti 2-1 za (21-17, 19-21, 15-9). Katika duru ya mwaka jana 2017, Iran iliibuka mshindi baada ya kuigaragaza Indonesia katika fainali dhidi ya Indonesia.

Debi la Sarkhobi laishia kwa sare tasa

Mchuano wa kukata na shoka kati ya klabu ya Esteqlal na Persepolis uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na shauku kuu na mashabiki wa soka hapa nchini uliishia kwa sare tasa siku ya Alkhamisi. Hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenziwe, licha ya makombora ya hapa na pale katika debi hilo la 88 la watani wa jadi wa soka hapa nchini.

Kwa sare hiyo, Persepolis ilisogea kileleni mwa jedwali la ligi angalau kwa masaa machache, ikiwa na alama 16, pointi nane mbele ya Esteqlal ambayo kwa sasa haina budi kuridhika na nafasi ya 11.

Debi la Sarkhobi

 

Mwezi Machi mwaka huu, timu mbili hasimu za soka hapa nchini zilishuka dimbani kuvaana katika debi la aina yake linalofahamika hapa nchini kama Sarkhobi, au debi la wekundu na buluu. Katika kitimutimu hicho cha aina yake kilichofuatiliwa na makumi ya maelfu ya mashabiki wa soka hapa nchini, vijana wa The Blues walifanikiwa kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Wekundu wa Tehran, katika mchuano uliofuatiliwa kwa karibu pia na Rais wa FIFA. Bao la kipekee na la ushindi la Esteqlal lilitiwa kimyani na kiungo aliyetajwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo Vouria Ghaffouri kunako dakika ya 40, na kuwanyanyua mashabaki kutoka vitini huku uwanja ukihinikiza kwa shangwe, nderemo na vifijo.

Gor Mahia yatwaa Ligi Kuu ya Soka Kenya

Klabu ya Gor Mahia wametawazwa rasmi ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka nchini Kenya baada ya kukamilika kwa msimu wa ligi nchini humo. Gor imekabidhiwa rasmi kombe hilo siku ya Jumapili, katika Uwanja wa Moi mjini Kisumu. Gor imetwaa kombo hilo licha ya kutoa sare ya mabao 2-2 na klabu ya Mathare United siku hiyo. Gor Mahia ukipenda Jeshi la Kijani ilitawala mchezo huo mbele ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, ingawaje ilipoteza fursa nyingi ya kuongeza mabao.

Wachezaji wa Gor Mahia wakinyanyua kombe

 

Kogalo bado inashikilia rekodi ya ubingwa nchini humo kwa kunyakua mataji hilo mara 17 ikiwa ni pamoja na kushinda taji hilo mara tatu mfululizo mwaka 2013, 2014 na 2015.

Klabu ya Bandari ambao ndio wawakilishi wa pekee ukanda wa Pwani kwenye ligi kuu nchini wamejiandikia Historia baada ya kumaliza kwenye nafasi ya pili ya ligi kuu.  Hii ni mara yao ya kwanza kumaliza kwenye nafasi hiyo tangu kupanda kwenye ligi kuu mwaka 2010 waliporudi baada ya kushukishwa daraja mwaka mmoja uliopita. Chini ya ukufunzi wa Bernad Mwalala Bandari hawajapoteza mchezo wowote wa ligi. Bandari wana alama 59 baada ya mechi 32 huku mechi mbili pekee zikisalia kabla ya ligi kukamilika huku AFC leopards ambao wako kwenye nafasi ya tatu wana alama 51 ishara kuwa hawawezi kufikia Bandari.

Debi la Kariakor, Simba yatoshana nguvu na Yanga

Watani wa jadi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara (TPL), Simba na Yanga walishuka dimbani siku ya Jumapili kumaliza ubishi, lakini mchuano huo ukamalizika bila mzizi wa fitina kukatwa. Mchezo huo wa aina yake uliochezeshwa na muamuzi wa kimataifa raia wa Tanzania, Jonesiah Rukya, katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam uliokuwa umefurika furifuri, Simba walifanikiwa kuutawala mchezo na kupata nafasi nyingi zaidi ya Yanga, kitu ambacho kilizidisha furaha kwa mashabiki wa Simba wakiamini timu yao itaondoka na point zote tatu. Lakini licha ya kupata nafasi zaidi ya saba ya kucheka na nyavu, Yanga walifanikiwa kuidhibiti Simba na kuufanya mchezo umalizike kwa sare tasa 0-0.

Wachezaji wa Simba dimbani

 

Hii ndio mara ya kwanza kwa kocha wa Yanga Mwinyi Zahera na kocha wa Simba Patrick Aussems kuziongoza timu hizo katika mchezo wa watani wa jadi (Kariakoo Debi). Sare hiyo sasa inaifanya Yanga kutimiza jumla ya pointi 13 katika msimamo wa Ligi wakati Simba wanafikisha jumla ya point 11. Kadhalika sare hiyo imewakata ngebe mashabiki wa timu mbili hizo, ambao kabla ya mechi walitupiana cheche za maneno ya kejeli.

Mechi ya Simba na Yanga ni mojawapo ya debi kubwa Afrika, ikitajwa kulinganishwa na mchezo baina ya Zamalek na Ahly nchini Misri, Kaizer Chiefs na Orlando Pirates nchini Afrika Kusini au Gor Mahia na AFC Leopards nchini Kenya. Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera amewalaumu baadhi ya wachezaji wake kwa kupotea kwenye kipindi cha kwanza katika mtanange huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Kocha wa Wekundu wa msimbazi Patrick Aussems, anasema Yanga bahati ilikuwa kwao na kwamba watakaza buti katika mechi zijazo. Simba walifanikiwa kuutawala mchezo kwa asilimia 62 kwa 38 dhidi ya Yanga kwa dakika zote 90.

Real Madrid yamuenzi mwanaharakati wa Palestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeghadhabishwa mno na hatua ya klabu mashuhuri ya soka ya Uhispania ya Real Madrid kumuenzi kwa kumtunuku jezi nambari 9 Ahed Tamimi, binti mwanamapambano wa Kipalestina. Emanuel Nachshon, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: Aibu ilioje kwa Real Madrid kumpokea gaidi ambaye anachochea chuki na ghasia. Kuna uhusiano gani kati ya hilo na mpira wa miguu? Ofisa mwingine wa utawala haramu wa Israel aliyeonesha kuingiwa na kiwewe kwa kitendo hicho cha Madrid kumuenzi mwanaharakati huyo wa Palestina ni Daniel Kutner, balozi wa Israel nchini Uhispania ambaye ameandika: Ahed Tamimi sio mtetezi wa amani, ni mtu anayeunga mkono ghasia na ugaidi. Taasisi zilizompokea na kumtunuku zinaunga mkono kwa njia isiyo ya moja kwa moja ya uvamizi na machafuko na wala sio mazungumzo na maelewano tunayopigania. 

Tamimi mjini Madrid

 

Ahed Tamimi ambaye kwa sasa amekuwa nembo ya muqawama katika ardhi za Palestina, kwa sasa anazitembelea nchi za Ulaya baada ya kuachiwa huru na jeshi la utawala haramu wa Israel. Itakumbukwa kuwa askari wa utawala katili wa Kizayuni walimkamata msichana huyo mwenye umri wa miaka 17 na ambaye amegeuka kuwa nembo ya muqawama, tarehe 19 Septemba mwaka jana kwa tuhuma za kumshambulia askari wa utawala huo vamizi, huku akiachiliwa huru tarehe 29 Julai mwaka huu, baada ya kubakia jela kwa miezi minane.

……………………..TAMATI………………….