Jumatano, tarehe 17 Oktoba, 2018
Leo ni Jumatano tarehe 7 Safar mwaka 1440 Hijria inayosadifiana na tarehe 17 Oktoba 2018.
Tarehe 7 Safar kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw) katika mwaka wa 50 Hijria. Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali AS. Mjukuu huyo wa Mtume aliuawa shahidi kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Miaka 45 iliyopita katika siku kama hii ya leo nchi za Kiarabu zinazouza nje mafuta ya petroli zilianza kutekeleza vikwazo vya mafuta dhidi ya Marekani, Uingereza na makampuni yanayouuzia mafuta utawala wa Kizayuni wa Israel. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Uingereza kwa utawala ghasibu wa Israel katika vita vya Israel dhidi ya Syria na Misri. Hatua hiyo ilipandisha sana bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kutoa pigo kubwa kwa nchi hizo za Magharibi. Muda mfupi baadaye nchi za Kiarabu zilikiuka vikwazo hivyo vya mafuta na kuanza tena kuiuzia mafuta Marekani na Uingereza. Vikwazo hivyo vilionesha kuwa nchi za Kiislamu zina silaha muhimu inayoweza kutumiwa dhidi ya uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kwa utawala katili wa Israel.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, aliaga dunia mtaalamu wa masuala ya jamii wa Kifaransa kwa jina la Raymond Aron. Aron alizaliwa mwaka 1905. Msomi huyo wa Kifaransa alikuwa akifundisha pia taaluma hiyo ya masuala ya jamii katika Chuo Kikuu cha Sorbonne, Paris kwa miaka kadhaa. Vilevile alikuwa akiandika makala katika majarida ya Le Figaro na Express mjini Paris. Raymond Aron ameandika vitabu vingi na hapa tunaweza kuashiria vitabu vyake vichache alivyovipa majina ya "Kuanza Vita vya Nyuklia, "Mapambano ya Kitabaka" na "Miaka ya Mwishoni mwa Karne".
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Shahrivar 1369 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, usul fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhimain na Najaf nchini Iraq. Miongoni mwa athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar-ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko katika mji wa Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake na ina vitabu zaidi laki tatu.
Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na umasikini duniani. Umoja wa Mataifa uliainisha siku hii katika kuhamasisha jamii na serikali kupambana na umasikini. Mwaka 1992 Mkutano Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa ulitamka na kuifanya siku hii kuwa “Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini.” Tangu wakati huo, juhudi zinafanyika kuhakikisha kuwa kila mwandamu anapata mahitaji muhimu ya kimaisha ikiwa ni pamoja na chakula, makazi, mavazi na huduma muhimu za kijamii na tiba. Hata hivyo wakati dunia ikiadhimisha siku ya kung'oa mizizi ya umaskini, idadi kubwa ya watu bado wanaishi katika umasikini wa kupindukia na wanashindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku, wengi wakiwa ni kutoka katika nchi za ulimwengu wa tatu.
