Ulimwengu wa Spoti, Okt 22
Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tuangazie baadhi ya matukio ya michezo yaliyogonga vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa……
Ukweaji: Muirani atuzwa medali China
Mwanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameibuka wa tatu na kutunukiwa medali ya shaba katika mashindano ya ukweaji yaliyofanyika katika mji wa Wujiang mkoani Jiangsu kusini mwa China. Reza Alipour aliibuka kidedea katika kategoria ya wanaume siku ya Jumapili katika mpambano wa kumtafuta mshindi wa tatu dhidi ya Mrusi Aleksandr Shilov, kwa kutumia sekunde 5.660.
Alipour ambaye anafahamika kwa jina la utani kama Duma wa Uajemi, ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kukwea ukutani kwa kasi ya juu, ya sekunde 5.48. Mwaka jana 2017 alitajwa kuwa mwanariadha wa mwaka wa tuzo za Shirikisho la Kimataifa la Michezo au kwa Kiingereza, International World Games Association (IWGA).
Katika mashindano ya kombe la dunia ya IFSC Climbing Worldcup mwaka huu 2018 yaliyofanyika kati ya Jumamosi na Jumapili nchini China, raia wa Indonesia, Aspar Jaelolo ndiye aliyeibuka mshindi katika safu ya wanaume na kutunukiwa medali ya dhahabu, huku Muitaliano Ludovico Fossali akiibuka wa pili na kutuzwa fedha. Duru ya mwisho ya mashindano ya kimataifa ya ukweaji almaarufu IFC Climbing Worldcup of the year 2018 itafanyika kati ya Oktoba 27 na 28 katika mji wa Xiamen nchini China.
Wanariadha wa Iran wazoa medali lukuki kimataifa
Wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali kochokocho katika mashindano kadhaa ya kimataifa yaliyofanyika mwishoni mwa wiki. Tuanze na taekwondo ambapo wanataekwondo wa Iran wamezoa medali tatu ikiwemo ya dhahabu iliyotwaliwa na Armin Hadipour Seighalani baada ya kumchachafya Mkorea Tae-Hun Kim katika safu ya wanataekwondo wenye kilo zisizozidi 58.
Mirhashem Hosseini aliipa Iran medali ya fedha huku Sajjad Mardani akitunukiwa medali ya shaba katika mashindano hayo ya dunia yanayofahamika kwa Kiingereza kama World Taekwondo Manchester Grand Prix. Katika upande wa mieleka, Hassan Yazdani Charati na Parviz Hadi Basmanj walitwaa medali ya shaba kila mmoja siku ya Jumapili katika mieleka mtindo wa kujiachia au Freestyle kwenye mashindano ya Wrestling World Championships katika mji mkuu wa Hungary, Budapest.
Si hayo tu, wanariadha wa Iran ya Kiislamu kwa sasa wanaendelea kuchota medali lukuki katika mashindano ya kimatifa ya kuendesha mitumbwi kwa walemavu yanayoendelea hivi sasa katika mji wa Samarkand, nchini Uzbekistan.
Hadi tunaenda mitamboni, Iran ilikuwa imeshinda medali 8 zikiwemo 6 za dhahabu. Kwenye mashindano hayo ya vijana wa bara Asia wenye chini ya umri wa miaka 23, Shahla Behrouzi Rad alitwaa dhahabu ya kwanza katika kategoria ya VL3, huku dhahabu nyingine zikitiwa kibindoni na Nader Eyvazi safu ya KL3, Roya Soltani VL2, huku Amin Aghandeh akituzwa medali ya fedha katika kitengo cha KL3. Mashindano hayo ya kupeleka mitumbwi ya walemavu (Paracanoe) huandaliwa na Shirikisho la Mitumbwi Duniani au ukipenda International Canoe Federation ICF.
Afcon: Tiketi mkononi
Timu za taifa za soka za Madagascar, Senegal, Tunisia na Misri zimejikatia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON, mwaka ujao nchini Cameroon. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa kisiwa cha Madagascar kutinga fainali hizo. Madagascar imejipatia tiketi baada ya kupata ushindi muhimu dhidi ya Equitorial Guinea kwa kuifunga bao 1-0 lililotiwa kimyani na Njiva Rakotoharimalala. Ndoto ya Madagascar imetimia baada ya kujaribu kufuzu katika mashindano haya mara 18 bila mafanikio. Senegal nayo iliishinda Sudan bao 1-0 na kujihakikisha nafasi ya kwenda nchini Cameroon, katika mechi iliyochezwa jijini Khatroum siku ya Jumanne. Misri ambao wanashikilia rekodi ya kushinda taji hili mara saba, walipata matokeo mazuri siku ya Jumanne baada ya kuifunga Eswatini (Swaziland) mabao 2-0 mjini Manzini licha ya kukosa huduma za Mohammed Salah anayekipiga Liverpool na ambaye kwa sasa anauguza jeraha.
Misri iliitandika timu hiyo 4-1 huko Alexandria walipokutana mara ya kwanza siku ya Ijumaa, mabao yaliyofungwa na Ahmed Elmohammady, Amr Warda, Ahmed Trezeguet na Mohammed Salah. Mafarao hao sasa watavaana na Tunisia mwezi ujao huko Alexandria kabla ya kukamilisha ratiba yao dhidi ya Niger mwezi Machi mwakani. Tunisia iliilemea Niger na kuigaragaza mabao 2-1 jijini Niamey. Baada ya mechi nne, Tunisia inaongoza Kundi J kwa alama 12 huku Misri ikiwa ya pili kwa alama 9. Ifahamike kuwa, Cameroon ina tiketi mfukoni ya kushiriki fainali hizo, kwa kuwa ni ni timu mwenyeji. Sudan Kusini na Eswatini tayari zimebanduliwa kwenye mbio hizo za kutinga AFCON. Uganda nayo inaelekea kufuzu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Lesotho jinini Maseru. Mechi ya kwanza, ilipata ushindi wa mabao 3-0 jijini Kampala. The Cranes, wanaongoza kundi L kwa alama 10, ikifuatwa na Tanzania ambayo ina alama 5. Matumaini ya Taifa Stars ya Tanzania kufuzu katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 bado yangalipo baada kuichabanga Cape Verde 2-0 jijini Dar es Salaam.
Huu ulikuwa ni mchezo wa marudiano wa kundi L ambapo Tanzania ilifungwa Ijumaa iliyopita goli 3-0 na kufanya matumaini ya taifa hilo la Afrika mashariki kwenda Cameroon kwa michuono ya Afcon mwakani kufifia. Ushindi huo wa Oktoba 16 unaifanya Tanzania kufikisha pointi 5 baada ya kucheza michezo 4. Rais wa Tanzania John Magufuli Oktoba 19 alikutana na timu hiyo ya taifa na kuichangia Shilingi milioni 50 kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Lesotho.
Huku hayo yakiarifiwa, timu ya taifa ya Kenya Harambee stars itasubiri zaidi kabla ya kujua hatma yao kuhusiana na iwapo wamefuzu kwa dimba la bara Afrika AFCON au watatarajiwa kuwavaa Sierra Leone kwanza. Hii ni baada ya shirikisho la kandanda ulimwenguni FIFA kushindwa kuja na hatua muafaka kuhusiana na marufuku ya Sierra Leone ambayo imewafanya kutoshiriki mechi zake dhidi ya Ghana ugenini na nyumbani. Harambee stars wanaoongoza kundi F wakiwa na alama saba wanasubiri uamuzi huo kujua kama iwapo tayari wamefuzu ama watalazimika kuwavaa Siera Leone kabla ya kufuzu. Harambee Stars wameahidiwa shilingi Milioni 50 na naibu wa rais William Ruto iwapo watafuzu kwa AFCON baada ya kukaa nje kwa miaka kumi na nne ambapo walishiriki mara ya mwisho mwaka 2004 nchini Tunisia.
Brazil Bingwa Olimpiki ya Vijana 2018
Brazil ndio mabingwa wa mchezo wa soka kwa vijana, katika mashindano ya Olimpiki ambayo yalifanyika mjini Buenos Aires nchini Argentina. Vijana wa Brazil walinyakua medali ya dhahabu kwa kuifunga Urusi mabao 4-1, miaka miwili baada ya kushindwa kwa mabao 7-1 katika fainali ya kombe la dunia na kuwahuzunisha mashambiki wengi wa taifa hilo. Kadhalika Brazil walitwaa dhahabu baada ya kuiadhibu Russia mabao 3-1 kwenye fainali ya mchezo wa futsal, au soka inayosakatwa ukumbini katika Olimpiki hiyo ya kimataifa nchini Argentina siku ya Alkhamisi. Wachezaji wa Misri nao walifanikiwa kunyakua medali ya shaba, baada ya kumaliza wa tatu. Katika mechi ngumu, vijana kutoka Misri waliwashinda wenyeji Argentina mabao 5-4. Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, Thomas Bach ameikabidhi Japan Bendera ya Olimpiki, ili iandae mashindano yajao ya Olimpiki katika majira ya kiangazi ya mwaka 2020. Senegal itakuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki kwa vijana, itakayofanyika jijini Dakar mwaka 2022.
……………………..TAMATI……………….