Nov 03, 2018 10:52 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (71)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 71.

Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu kinaanza kukaribia ukingoni. Kwa hivyo katika kipindi chetu cha leo tutaanza kuzipitia tena nukta kuu tulizozijadili katika mifululizo 70 ya kipindi chetu hiki na hatimaye kufanya majumuisho na hitimisho kuhusu suala la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kutokana na yote tuliyozungumza katika vipindi vilivyopita tunaweza kusema kuwa umoja wa Kiislamu unatokana na mafundisho ya msingi katika dini ya Uislamu; na suala hili limefuatiliwa katika pande mbili za kinadharia na kivitendo katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa kuanzia, katika kipindi hiki tutaizungumzia tena kimapitio nafasi ya umoja baina ya Waislamu katika uga wa nadharia hususan wa rai na mitazamo ya wanafikra na warekebishaji umma wa Kishia na Kisuni; na baada ya hapo, katika vipindi vitakavyofuatia, tutafanya majumuisho kuhusu yale tuliyoyazungumza huko nyuma juu ya utekelezaji na uchukuaji hatua za kivitendo za kuleta umoja na mshikamano baina ya Waislamu.

Suala la umoja wa Kiislamu, ambao ni daghadagha la msingi walilonalo Waislamu katika dunia ya leo, chimbuko la umuhimu wake linatokana na ukweli kwamba tunapozipitia takwimu zilizopo tunabaini kuwa hivi sasa kuna Waislamu wasiopungua bilioni moja na milioni mia mbili katika maeneo tofauati ya dunia; na katika nchi zipatazo 57, wao ndio wanaounda jamii ya waliowengi katika nchi hizo. Aidha katika nchi nyingine nyingi, Waislamu wanaunda jamii ya waliowachache, lakini wenye sauti na ushawishi. Mbali na nchi za Kiislamu kuwa na karibu theluthi moja ya viti vya wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zina utajiri mkubwa pia wa nishati za mafuta na gesi, mbali na kuwepo kwenye maeneo hasasi na ya kistratejia duniani kwa upande wa kijiografia, suala ambalo linazipa nafasi ya kuwa na uwezo mkubwa kiuchumi, kisiasa na kijeshi. Lakini licha ya kuwa na fursa za kuzifanya ziwe na uwezo huo mkubwa wa kiuchumi, kisiasa na kijeshi, ambao kama utaendeshwa na kutumiwa kwa njia sahihi unaweza kuzifanya nchi za Kiislamu ziwe kitovu na mhimili mkubwa duniani, lakini kwa masikitiko ni kwamba kutokana na kutokuwa na umoja na mshikamano, nchi hizo hazina hadhi na nafasi ya kuridhisha katika mfumo wa kimataifa; na hata ndani ya mipaka yao zenyewe pia zinakabiliwa na matatizo kadha wa kadha hususan migogoro na mizozo ya ndani pamoja na ukata wa kiuchumi.

Lakini mbali na hayo, mifarakano iliyopo baina ya Waislamu, ambayo ni sababu kuu ya kubaki nyuma kimaendeleo nchi za Kislamu ni moja ya mambo yaliyozishughulisha sana fikra za wasomi, wanafikra, warekebishaji umma na hata wanasiasa wa Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa mtazamo wa warekebishaji umma wengi wa Ulimwengu wa Kiislamu, kujiweka mbali Waislamu na thamani za asili za dini yao na kufufua taasubi na ukereketwa wa kikabila, rangi na asili zao wa zama za ujahilia, ndiyo sababu kuu ya mpasuko na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa sababu hiyo, warekebishaji umma hao wamependekeza njia mbalimbali za kujenga umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu. Lakini licha ya jitihada na hatua za uelimishaji zilizochukuliwa na muslihina hao, yaani warekebishaji umma, hususan wanafikra mashuhuri kama Sayyid Jamaluddin Asad Abad, Iqbal Lahore na Imam Khomeini (RA), kwa kutilia mkazo udharura wa kuzinduka Ulimwengu wa Kiislamu na kuwepo umoja baina ya nchi za Kiislamu kwa kuzingatia misingi na usuli, itikadi  madhubuti za dini yao na masuala yanayowaunganisha pamoja kama imani yao juu ya Mungu mmoja pekee, yaani Tauhidi, Utume wa Nabii Muhammad SAW, Qur’ani moja iliyohifadhika na kuongezwa au kupunguzwa chochote na pia kibla chao cha pamoja, la kusikitisha ni kwamba, hadi sasa Ulimwengu wa Kiislamu haujaweza kuchukua hatua za dhati kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano; na ndiyo maana Waislamu wengi wanateseka na kutaabika kwa ufakiri na ukata wa kiuchumi, kwa kuwa na nafasi duni kisiasa katika uga wa kimataifa na pia kwa kuandamwa na matatizo na masaibu mbalimbali yanayosababishwa na uingiliaji wa kisiasa na kijeshi wa madola yenye nguvu.

 

Katika aya ya 103 ya Suratu Aal Imran, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewataka Waislamu washikamane na kamba yake na kuutaja umoja kuwa ni neema kwao. Sehemu ya aya hiyo inasema: (Kiarabu) Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Kwa mujibu wa Qur’ani tukufu kumwabudu Allah ndilo chimbuko la kupatikana umma mmoja, na kumfuata asiyekuwa Yeye ndiyo sababu ya mfarakano. Na kwa kutumia msingi huo, kuanzia siku alipoanza kuwalingania watu Uislamu hadi lahadha ya mwisho ya uhai wake, Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa akiwausia na kuwasisitizia Waislamu suala la umoja na kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na maadui kwa msingi wa kumwabudu Allah SW. Wakati katika zama za ujahilia kulikuwepo na aina za mifarakano na hasama za kikaumu na kikabila baina ya Waarabu, ambazo kila mara zilisababisha mapigano na umwagaji damu, Uislamu ulikuja na sha'ar na kaulimbiu ya "umoja na udugu na kuepukana na mifarakano na uadui kwa kushikamana na kalima ya Tauhidi ya "Laaila illa Allah" na kuweza kuwaunganisha wafuasi wake na kuwafanya kitu kimoja. Dini ya Uislamu iliweza kuutekeleza umoja kivitendo kwa kuifanya taqwa na uchaji Mungu kuwa ndicho kigezo cha kulinganishia watu na kuzikana sababu nyinginezo wanazotumia kwa ajili ya kujikweza kama taasubi na ukereketwa wa kikaumu, kikabila, nasaba, asili na lugha zao.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa, nikitumai kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshaallah, katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 72 ya mfululizo huu nakuageni, huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu…/

Tags