Nov 09, 2018 02:40 UTC
  • Ijumaa tarehe 9 Novemba mwaka 2018

Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na Novemba 9, mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita, Mtume Muhammad (saw) alianza Hijra yake ya kuhama Makka na kuelekea Madina, ikiwa imepita miaka 13 tokea alipobaathiwa na kupewa Utume. Mtume wa Allah alihama Makka kutokana na kushadidi vitimbi vya washirikina wa mji huo ambao walikusudia kumdhuru na kumuua wakati wa usiku akiwa amelala nyumbani kwake. Imam Ali AS alijitolea mhanga, kwa kuamua kulala kwenye kitanda cha Mtume, ili maadui wasitambue kwamba Mtume wa Allah ameondoka mjini Makka. Hijra ya Mtume (saw) na matukio ya baada yake yalikuwa na umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Uislamu kiasi kwamba tukio hilo lilitambuliwa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Mtume (saw) ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia hijra yake kama mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwani barua zote zilizoandikwa na mtukufu huyo kwa wakuu wa makabila na shakhsia maarufu alizisajili kwa kalenda hiyo.

Tarehe Mosi Rabiul Awwal miaka 1375 iliyopita, ilianza harakati ya Tawwabin kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu. Awali, watu wa Kufa walimuomba Imam Hussein AS aelekee mjini humo kwa lengo la kuongoza harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Yazid bin Muawiya lakini alizingirwa njiani na jeshi la mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya, na kuuawa shahidi. Tawwabin ni kundi la watu wa Kufa ambalo lilijuta kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake na kumuacha Imam Hussein na wafuasi wake wachache peke yao wapambane na majeshi ya Yazid. Kwa minajili hiyo watu hao walitubia makosa yao na kuamua kuanzisha harakati ya kulipiza kisasi wakiongozwa na Sulaiman bin Sorad dhidi ya jeshi la Yazid. Kundi hilo lilipigana kishujaa na jeshi la Yazid na wengi kati ya wapiganaji wake wakauawa shahidi.

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, alizaliwa nchini Pakistan Allama Muhammad Iqbal Lahori mwandishi, mwanafikra na malenga mzungumza lugha ya Kifarsi. Baada ya kumaliza masomo yake ya juu, Iqbal Lahori alielekea katika nchi za Ujerumani na Uingereza kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu zaidi katika taaluma ya falsafa. Alianza kusoma mashairi akiwa kijana na shairi lake la kwanza alilipa jina la 'Naleh Yatiim' kwa maana ya kilio cha yatima. Allama Iqbal Lahori alikuwa mwanaharakati pia aliyepambana kwa minajili ya kuikomboa Pakistan kutoka mikononi mwa India. Allamah Muhammad Iqbal alifariki dunia mwaka 1938.

Muhammad Iqbal Lahori

Miaka 100 iliyopita sawa na tarehe Tisa mwezi Novemba mwaka 1918, mfumo wa jamhuri ulitangazwa huko Ujerumani kufuatia kushindwa mara kadhaa jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Waitifaki katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kuzuka uasi nchini humo. Matukio hayo yalipelekea kujiuzulu Wilhelm wa Pili mtawala wa mwisho wa kifalme wa nchi hiyo. Siku mbili baadaye mfalme huyo alikimbilia Uholanzi na hivyo utawala wa kifalme ukawa umehitimishwa nchini Ujerumani. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kufutwa utawala wa kifalme, Friedrich Ebert alishika madaraka ya nchi kama rais wa kwanza wa nchi hiyo.

Wilhelm wa Pili

Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, ukuta wa Berlin ambao ulikuwa ukiugawa mji huo katika sehemu mbili za mashariki na magharibi kwa kipindi cha miaka 28 hatimaye ulivunjwa. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa mji huo lilikuwa likidhibitiwa na Urusi ya zamani, huku eneo la magharibi likidhibitiwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Machafuko yaliyotokea mjini Berlin hapo mwaka 1961 na wakazi wa mashariki kukimbilia upande wa magharibi, kulizitia wasiwasi serikali za Urusi ya zamani na Ujerumani mashariki, suala lililozipelekea nchi hizo kujenga ukuta huo ambao baadaye uliokana kuwa nembo ya kuwaganywa Ujerumani. Hata hivyo kuporomoka kwa Urusi ya zamani ambako kuliacha taathira kubwa pia katika tawala za kikomunisti za Ulaya mashariki kulipelekea kuvunjwa ukuta huo wa Berlin hapo mwaka 1989.

Ukuta wa Berlin

 

Tags