Nov 26, 2018 07:54 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Nov 26

Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio yaliyogonga vichwa habari viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa...

Soka: Iran yaanza vyema IFCPF Asia-Oceania

Timu ya taifa soka ya wachezaji wenye utindio wa ubongo (cerebral palsy) ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanza vyema mashindano ya mabingwa wa mchezo huo ya bara Asia, ya mwaka huu 2018, baada ya kuitia skulini Thailand. Iran siku ya Jumamosi ilishuka dimbani kuvaana na Thailand katika mchuano wake wa ufunguzi, ambapo waliigeuza timu hiyo kichwa cha mwendawazimu na kuinyoa mabao 7-1 bila maji.

Iran ikipambana na Thailand

 

Katika mchuano huo uliopigwa katika kisiwa cha Kish, nahodha wa timu hiyo ya Iran, Abdorreza Karimizadeh ndiye aliyekuwa nyota wa mechi, ambapo alifanikiwa kuchena na nyavu mara tano. Iran ilitawala mchuano huo wa nyumbani katika mashindano hayo yanayofahamika kama (International Federation of Cerebral Palsy Football) Asia-Oceania Championship. Australia pia ilianza vyema kwa kuichachafya Korea Kusini mabao 11-0. Iran ni mwenyeji wa Australia, Korea Kusini, Jordan na Thailand katika mashindano hayo ya siku nane yatakayomalizika Novemba 30.

Iran yalazimishwa sare na Venezuela

Timu ya taifa soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Venezuela katika mchuano wa kirafiki uliopigwa Jumanne katika Uwanja wa Al Ahli mjini Doha, Qatar. Venezuela ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kiungo Darwin Daniel katika dakika ya 35. Hata hivyo dakika 7 baadaye, Ali Gholizadeh aliwapiga chenga mabeki wa Venezuela na kuachia shuti kali kutoka nje ya sanduku na kumduwaza kipa wa timu hiyo hasimu.

Mchezaji wa Team Melli akimpiga chenga beki wa Venezuela

 

Iran iliinyuka Trinidad and Tobago bao 1-0 katika mchuano mwingine wa kirafiki uliopigwa Alkhamisi ya Novemba 15 katika Uwanja Taifa wa Azadi hapa jijini Tehran.  Kabla ya hapo pia waliichabanga Bolivia mabao 2-1 na kuilambisha sakafu Uzbekistan kwa bao 1 bila jibu. Wachezaji hao wa mkufunzi Carlos Queiroz wanatumia michuano hiyo ya kirafiki kama sehemu ya kupasha misuli moto, kuelekea Kombe la Asia la AFC, mwaka ujao 2019. Iran ipo katika kundi moja na Yemen, Iraq na Vietnam. Iran ambayo imeorodheshwa kama timu ya kwanza barani Asia, itafungua kampeni zake za kutwaa Kombe la AFC kwa mchuano dhidi ya Yemen, unaotazamiwa kupigwa Januari 7 mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Iran yatwaa taji la mabingwa wa Taekwondo

Timu ya taekwondo ya Shahrdari Varamin ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kidedea katika mashindano ya dunia ya mchezo huo yaliyofanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Timu hiyo ya Iran imetwaa taji hilo baada ya kuipeleka mchakamchaka Russia katika pambano la fainali, lililopigwa wikendi katika mji wa pwani wa Fujaira, ulioko mashariki mwa Imarati. Varamin ya Iran iliichachafya Russia alama 31-30, katika fainali ya kufa kupona na kujizolea jumla ya alama 165.

Wanataekwondo wakikabiliana

 

Iran iliilemea Kazakhstan kwa alama 49-29 katika kitimutimu cha nusu fainali ya mashindano hayo yanayofahamika kama Fujairah 2018 World Taekwondo Team Championships. Kabla ya hapo, Shahrdari Varamin ya Iran ilizizaba Azerbaijan pointi 66-58, China 45-44 na Uzbekistan 54-37 katika mechi za awali za Kundi B. Mashindano hayo ya dunia yalifungua pazia lake Novemba 22 na kufikia tamati Jumapili ya Novemba 25. 

Soka la Wanawake Afrika

Mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa upande wa wanawake, Super Falcons ya Nigeria, wamefufua matumaini ya kusonga mbele katika fainali za mwaka huu zinazoendelea jijini Accra nchini Ghana, baada ya kuifumua Zambia mabao 4-0 katika mechi yake ya pili ya Kundi G siku ya Jumatano usiku. Huu ni ushindi muhimu kwa Nigeria, ambao walianza vibaya michuano hii baada ya kufungwa na Afrika Kusini bao 1-0.

Hata hivyo, kitumbua cha Equitorial Guinea kimeendelea kuingia mchanga baada ya kupoteza mechi yao ya pili. Timu hiyo imepokea kichapo cha mbwa kutoka Afrika Kusini kwa kusasambuliwa mabao 7-1. Mali kama vile Nigeria, pia imefufua matumaini ya kusonga mbele katika hatua ya mwondoano, kuwania taji hilo la bara Afrika au ukipenda Afcon ya Wanawake, baada ya kuwafunga wenyeji Ghana mabao 2-1 katika mechi yake ya pili siku ya Jumanne jijini Accra. Katika mechi ya kwanza, Mali ilianza kwa mguu wa kushoto baada ya kufungwa na Cameroon mabao 2-1. Hata hivyo, Cameroon imeendeleza rekodi ya ushindi katika mechi ya kundi A baada ya kuichabanga Algeria mabao 3-0.

Casablanca ya Morocco yaelekea kutwaa Kombe la Shirikisho

Klabu ya soka ya Raja Casablanca ya Morocco imebakisha hatua chache itwae Kombe la Shirikisho la CAF kwa mara ya sita, baada ya kuibanjua V Club ya Kongo DR katika mchuano wa aina yake uliopigwa Jumapili. Katika mchuano huo uliochezwa katika Uwanja wa Mfalme Mohammad wa Tano huko Casablanca, ambao ni mji mkuu wa kibiashara wa Morocco, wenyeji walitamalaki mchezo, na kupata ushindi mnono wa mabao 3-0.

Hakuna timu iliyokuwa imeona lango la mwingine katika kipindi cha kwanza, lakini dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili, Soufiane Rahimi aliamua kuvunja mzingiro huo, na kupachika wavuni bao la kwanza la wenyeji, katika uwanja huo uliokuwa umefurika zaidi ya watazamaji 65, 000. Kiungo huyo aliongeza la pili ikiwa imesalia nusu saa mchezo uamalizike. Mchezaji anayeongoza kwa ufungaji wa mabao katika Confederation Cup, Mahmoud Bin Halib alilizamisha kabisa jahazi la Batoto ba Kongo, kwa bao alilolifunga kunako dakika ya 66, kupitia mkwaju wa penati, hilo likiwa ni goli lake la 12 katika mashindano haya ya kieneo.

Mkufunzi wa timu hiyo ya Morocco, Juan Carlos Garrido raia wa Uhispania anatazamiwa kuwa kocha wa kwanza kuongoza vilabu viwili kutwaa Kombe la Shirikisho, ikizingatiwa kuwa aliinoa al-Alhly ya Misri kutwaa taji la mwaka 2014.

Dondoo za Hapa na Pale

Tangazo la Rais wa Liberia George Weah la kuwa na mpango wa kuwajumuisha Wachezaji wa Timu ya Taifa ya soka ya Nchi hiyo katika orodha ya Wafanyakazi wa Serikali watakaokua wanapokea mshahara kila mwisho wa mwezi, limepokewa vizuri na wadau katika uliwengu wa soka, sio tu katika nchi hiyo bali kote barani Afrika. Iwapo azma hiyo itatekelezwa, basi Liberia itakuwa ni taifa la kwanza Afrika kuwalipa mshahara wachezaji wa Timu ya Taifa kila mwisho wa mwezi.

George Weah zama zake uwanjani

 

Weah ambaye binafsi ni galacha wa soka wa zamani, anaamini kuwa wachezaji hao wanastahili mshahara huo wa kila mwisho wa mwezi kutoka kwa serikali, kwani wanajitoa kwa ajili ya taifa lao. Timu ya Liberia iliifunga Zimbabwe 1-0 katika harakati za kutafuta tiketi ya kufuzu fainali ya bara Afrika mwaka 2019 nchini Camerooon.

Timu ya taifa ya basketboli ya Iran licha ya kuwa ugenini iliicharaza Qatar vikapu 75-64 katika mchuano wa kirafiki uliopigwa Ijumaa katika mji mkuu Doha. Timu hiyo ya Iran inatazamiwa kuvaana na Australia katika mchuano mwengine wa kirafiki mnamo Novemba 30 mjini Melbourne na kisha Ufilipino Disemba 3 katika mji wa Pasay.

Na mchezaji nyota wa soka wa Ivory Coast ambaye amewahi kuichezea klabu ya Chelsea Didier Drogba, ametangaza kustaafu kusakata kabumbubu baada ya kuwa uwanjani kwa zaidi ya miongo miwili. Drogba mwenye umri wa miaka 40, anastaafia katika klabu ya Phoenix Rising ya Marekani. Hata hivyo umaarufu wake katika uga wa kandanda ulitokana na umbuji wake alipokuwa Stanford Bridge nchini Uingereza, ambapo aliifungia Chelsea mabao 164 katika mechi 341 alizocheza.

Chelsea ya zama za Drogba

 

………………………TAMATI………………..