Dec 10, 2018 07:22 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Dec 10

Ufuatao ni ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita....

Futsal: Iran yatwaa ubingwa

Timu ya taifa ya futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Kombe la Mataifa Matatu la Slovak katika mashindano ya mchezo huo yaliyofanyika katika mji mkuu wa Slovakia, Bratislava. Licha ya Iran kulamizimishwa sare ya mabao 3-3 katika mchuano wake wa Jumatano, ilipovaana na mwenyeji Slovakia, lakini hili halikuizuia kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ya pande tatu ya mwaka huu, yanayofahamika kama Slovak Futsal Week. Timu hiyo ya Iran iliichanbanga Russia mabao 5-4 katika mchuano wake wa ufunguzi. Iran imemaliza ya kwanza kwa jumla ya alama nne, huku Russia ikimaliza ya pili ikiwa alama tatu. Mwenyeji Slovakia imevuta mkia na kumaliza kwa alama moja tu licha ya kuchezea nyumbani mbele ya mashabiki wake. Iran imetumia mashindano hayo kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Dunia la Futsal la Mwaka 2020, sambamba na Kombe la Futsal la Mabingwa wa Asia mwaka huo huo. Iran inatazamiwa kuvaana na Serbi katika mechi ya kufunga mwaka.

Makarateka wa Iran wazoe medali China

Makarateka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali lukuki katika mashindano ya Karate 1 Series A mjini Shanghai nchini China. Siku ya Jumapili, Zabiollah Poorshab alitwaa medali ya dhahabu baada ya kumzidia nguvu Mkazaki, Igor Chikhmarev kwa alama 2-0 katika kategoria ya makarateka wenye kilo zisizozidi 84. Iran ilitwaa medali nyingine ya dhahabu baada ya Miad Yari kumpeleka mchakamchaka Eray Samdan wa Uturuki katika kitengo cha makarateka wenye kilo zisizozidi 60.

Makarateka wa Iran

Aidha katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Karate Duniani, Amir Mehdizadeh wa Jamhuri ya Kiislamu alimpeleka mbio Muirani mwenzake, Alireza Shirsefat na kumlemea kwa alama 8-4 na kutwaa medali ya shaba, katika safu ya makarateka wenye kilo chini ya 64. Makarateka 1,176 kutoka nchi 80 duniani wameshiriki mashindano hayo ya (WKF) Karate 1-Series A mjini Shanghai nchini China.

Wakenya watamalaki Singapore Marathon

Wanariadha wa Kenya wamezidi kuwaonyesha walimwengu kuwa wao ni moto wa kuotea mbali ikija katika mbio za masafa marefu. Ndivyo unavyoweza kuelekeza hali katika mbio za Singapore Marathon mwaka huu 2018. Katika safu ya wanaume, wanariadha wa Kenya walizoa nafasi za kwanza 17, wakiongozwa na Joshua Kipkorir aliyetumia masaa 2 dakika 12 na sekunde 12, akifuatia na mwenzake Felix Kirwa (2:13:43), huku Andrew Kimtai akifunga tatu bora kwa kutumia masaa (2:14:30). Katika safu ya wanawake, Prisca Cherono aliibeba bendera ya Kenya na kukata utepe kwa kutumia masaa 2, dakika 32 na sekunded 23. Alifuatwa unyo kwa unyo kwa na wenzake Stella Barsosio (2:33:23), na Jane Jelagat (2:35:38). Cosmas Kimutai na Pamela Rotich wamejizolea Shilingi milioni 5 kila mmoja baada ya kutwaa mataji ya mbio za Singapore Marathon, Jumapili. Duru hii ya 16 ya mbio hizo imevutia wanariadha 48, 400 kutoka mataifa 126 duniani.

Wakati huohuo, Wakenya wameng'ara pia katika mbio za Honululu Marathon jimboni Hawaii nchini Marekani. Titus Ekiru aliibuka kidedea kwa kutumia masaa 2 dakika 9 na sekunde 0, huku nafasi ya pili na tatu zikiwaendea Wakenya wenzake Reuben Kerio Kiprop (2:12:59) na Vincent Yator (2:15:31).

Katika kategoria ya wanawake, Mkenya Vivian Kiplagat alibuka kidedea kwa kutumia 2:36:22, akifuatiwa na Mkenya mwenzake, Sheila Jerotich (2:42:02), huku Mjapani Era Suzuki akifunga orodha ya tatu bora kwa kutumia 2:47:53.

Congo Brazaville kuwa mwenyeji wa Afcon 2019?

Waziri wa Michezo wa Congo Brazaville amekanusha madai kuwa nchi hiyo inapania kuwa mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika Afcon mwaka ujao 2019. Hugues Ngouélondélé amesema siku ya Jumamosi kuwa, "Kwa sasa serikali inatoa kipaumbele kwa mambo mengine ya msingi. Imebaki miezi sita kwa mashindano hayo ya kikanda kufanyika, itakuwa vigumu sana tuwe tumekamilisha maandalizi yote." Kauli ya waziri huyo inajiri siku moja baada ya Constant Omari, Naibu Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Afrika CAF kusema kuwa wamepokea barua kutoka Congo Brazavile, wakiomba kuwa wenyeji wa mashindano hayo. Wakati huo huo, Kenya imesema haitaomba kuandaa mashindano yoyote ya kimataifa ya soka hadi wakati viwanja vyake vitakapokuwa viko katika hali nzuri.

Wakuu wa CAF baada ya kuitoa Cameroon tonge mdomoni

Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa amesema kwamba Shirikisho la (CAF) lilikuwa limeomba Kenya kuwazia uenyeji wa Kombe la Afrika (AFCON) mwaka ujao 2019 baada ya kuipokonya Cameroon haki za kuandaa kindumbwendumbwe hicho kutokana na hali duni ya usalama na pia miundombinu isiyoridhisha. Cameroon ilipokonywa uenyeji mnamo Novemba 30 wakati kamati kuu ya CAF ilikuwa na kikao chake jijini Accra, Ghana.

Dondoo za Hapa na Pale

Luka Modric, kiungo wa kati wa kabu ya Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia, ndio mshindi wa tuzo ya mwaka 2018 ya Ballon d’Or. Modric, mwenye umri wa miaka 33, amevunja rekodi ya zaidi ya miaka 10, ambayo imekuwa ikitawaliwa na Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Mchezaji huyo, amepata tuzo hiyo, baada ya kuisadia klabu yake kunyakua ligi kuu ya soka nchini Uhispania mara tatu mfululizo. Aidha, alikuwa wa msaada mkubwa, alipoisadia timu yake ya taifa kufika fainali ya kombe la dunia, licha ya kufungwa na Ufaransa mabao 4-2 mwezi Julai huko nchini Urusi. Anasema kushinda tuzo hiyo ni kutimia kwa ndoto ya muda mrefu.

Luka Modrci, mshindi wa Tuzo ya Ballon d'Or

Kwengineko, Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu 2017-2018, Mohamed Salah amekwea kileleni mwa jedwali la wafungaji wa mabao kwenye ligi hiyo msimu huu wa 2018-2019 baada ya kuongoza Liverpool kuicharaza Bournemouth mabao 4-0 Jumamosi. Mshambuliaji huyu matata wa Misri alifunga mabao matatu ya hattrick katika Uwanja wa Dean Court na kumfikia Mgabon Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal kwa idadi ya mabao.

Mo Salah akitoka uwanjani baada ya kujeruhiwa

Hata hivyo, kutokana na murua na unyenyekevu wake, salah ambaye nyumbani Misri anafahamika kama Mfalme wa Soka, alikataa kupokea tuzo ya mchezi wa mechi MOTM, na badala yake akamuachia mchezaji mwenzake James Milner, ambaye hu ulikua mchuano wake wa 500 wa Ligi Kuu ya Soka Uingereza.

Na Bingwa wa dunia wa mbio za Marathon katika mchezo wa Riadha Mkenya Eliud Kipchoge na Mcolombia, Caterine Ibarguen anayeshiriki mashindano ya kuruka, ndio wanariadha bora wa mwaka 2018. Kipchoge ameshinda tuzo hii baada ya mwezi Septemba kuvunja rekodi ya mbio za Marathon huko Berlin, nchini Ujerumani kwa muda wa saa mbili dakika moja na sekunde 39.

Eliud Kipchoge

Mwanariadha huyo wa Kenya mwenye umri wa miaka 34, anatajwa kuwa mwanariadha bora wa mbio hizi ndefu katika miaka ya hivi karibuni. Kati ya mashindano 11 ya Marathon aliyoshiriki, ameshinda 10 na kushinda mara tatu jijini London na Berlin bila kusahau wakati wa michezo ya Olimpiki mwaka 2016 nchini Brazil.

…………………….TAMATI…………………