Spoti, Dec 24
Hujambo mpenzi msikilizaji wa RT na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa....
Soka U23: Iran yainyuka Syria
Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 imeichachafya Syria mabao 3-1 katika mchuano wa kirafiki, uliopigwa siku ya Ijumaa. Katika mchuano huo uliochezwa katika uwanja wa kisiwani Kish, kusini mwa Ghuba ya Uajemi, vijana wa Iran waliitandaza ngozi na kutawala mchezo. Mabao ya timu hiyo ya Iran yalifungwa na Vahid Namdari, Alireza Arta na Mohammad Reza Azadi.
Awali timu hiyo ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 iliisasambua Syria mabao 2-0 katika mchuano wa awali wa kirafiki. Vijana hao wa mkufunzi Zlatko Kranjcar wanatumia michuano hii ya kirafiki kama sehemu ya maandalizi ya mashindano ya Mabingwa wa Asia yatakayoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia AFC mwaka 2020. Timu hiyo ya Iran imeorodheshwa katika Kundi C pamoja na Iraq, Yemen na Turkmenistan. Michuano hiyo ya AFC U-23 Championship itafanyika nchini Thailand mwaka 2020, na timu zitakazofuzu hapo zitajikatia tiketi ya kushirikishi mashindano ya Olimpiki mwaka huohuo.
Mieleka: Iran yatwaa taji la Ardabil
Timu ya mieleka ya mtindo wa Greco-Roman ya Bimeh Razi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Kombe la Dunia la Klabu Bingwa katika mashindano ya kimataifa yaliyofanyika mjini Ardabil, kaskazini magharibi mwa Iran. Wanamieleka hao stadi wa Iran walitwaa taji hilo siku ya Ijumaa baada ya kuwalemewa mahasimu wao wa Russia katika fainali, na kuwashinda kwa alama 8-2.
Klabu nyingine ya Iran ya Sina Sanat Izeh iliwapeleka mbio wanamieleka wa Uturuki na kuibuka mshindi wa tatu. Klabu ya Bimeh Razi ya Iran wiki iliyopita, ilitwaa pia taji la Mieleka ya Kujiachia (Freestyle).
Klabu Bingwa Afrika
Simba wanacheka, Kogalo wanalia! Klabu ya soka ya Simba ya Tanzania siku ya Jumapili ilikata mzizi wa fitina, baada ya kuiadhibu Nkana Red Devils ya Zambia katika mchuano wa Ligi ya Klabu Bingwa Barani Afrika (CAF Champions League). Simba imetinga hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 4-3 huku Nkana ikiangukia Kombe la Shirikisho Afrika. Simba walishuka dimbani katika mchezo huo wa nyumbani katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam, hiyo ikiwa ni mechi ya marudiano ya mzunguko wa kwanza. Simba walikuwa wanaingia uwanjani wakihitaji ushindi wa kuanzia goli 1-0, hiyo ni baada ya mchezo wa kwanza walioucheza mjini Kitwe Zambia, kufungwa kwa magoli 2-1. Presha ilikuwa kubwa katika mchezo huo ukizingatia kuwa Simba hawakuwahi kuwatoa Nkana mara zote walizocheza.
Simba licha ya kutanguliwa kwa goli la mapema na kupewa mzigo wa kuhitaji magoli matatu ili wafuzu, walifanikiwa kupindua matokeo na kuwafunga Red Devils wa Zambia kwa magoli 3-1 na kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF Champions League kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 10. Magoli ya Simba yalifungwa na Jonas Mkude dakika ya 29, Meddie Kagere 45 na Clatous Chama kunako dakika ya 88. Nkana walifunga goli la mapema katika dakika ya 17 wasijue hilo ndilo litasalia kuwa bao la kufitia machozi. Kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF Champions League kumeipaisha Simba, na kocha wao Patrick Aussems alikuwa na haya ya kusema.
Wakati huohuo, azma ya klabu nyota ya Kenya ya Gor Mahia ya kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Barani Afrika imegonga mwamba baada ya timu huyo kuambulia sare ya mabao 3-3 na Lobi Stars ya Nigeria. Kwenye mechi hiyo ya kuwania kufuzu hatua ya makundi iliyochezwa siku ya Jumamosi katika uwanja wa Enugu, Nigeria, K’Ogalo ambao waliingia uwanjani wakiwa kifua mbele baada ya kuwadhalilisha Lobi Stars mabao 3-1 katika mchuano wa mzungumzuko wa kwanza, walihitaji walau ushindi hafifu au wapoteze tu kwa mwanya wa bao moja ili kufuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Klabu nyingine ya Kenya ya Kariobangi Sharks pia imebanduliwa nje ya mbio hizo, baada ya kucharazwa mabao 2-1 na klabu ya Asante Kotoko ya Ghana mjini Kumasi.
Baiskeli: Myarwanda bingwa wa Afrika
Raia wa Rwanda Joseph Areruya, anayeendesha baiskeli katika timu ya Ufaransa Delko Marseille, Ijumaa alitajwa kuwa Mwendesha baiskeli wa Mwaka 2018 wa Afrika na kuwa Mnyarwanda wa kwanza kushinda tuzo ya juu tangu ianzishwe mwaka 2012. Mchezaji huyo mwenye miaka 22 mwaka jana alishindwa na Muafrika Kusini Louis Meintjes na kumaliza akiwa wa pili. Katika mashindano ya mwaka huu Areruya alifuatiwa na Muafrika Kusini Daryl Impey na Mueritrea Amanuel Ghebreigzabhier wakichukua nafasi ya pili na tatu mtawalia. Ushindi wake katika mashindano ya La Tropicale ya Gabon na Tour de l'Espoir ya Cameroun pamoja na medali zake nne katika mashindano ya Mabingwa wa Bara la Afrika mwaka huu umemfanya achukue tuzo hiyo.
Dondoo za Hapa na Pale
Hisia mbalimbali zimeendelea kuibuka baada ya klabu ya Manchester United kumtimua meneja wake Jose Mourinho. Man U walichukua hatua hiyo baada ya klabu hiyo kushindwa kufanya vizuri ilipovaana na Liverpool Jumapili ya wiki iliyopita. Mourinho amekuwa Old Trafford kwa miaka miwili na nusu baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa Louis van Gaal, raia wa Uholanzi, mwezi Mei 2016.
Muda mfupi baada ya Mourinho kutimuliwa mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi ndani ya timu hiyo Paul Pogba ameonesha kufurahishwa na uamuzi huo. Pogba na Mourinho wamekuwa wakihasimiana, kiasi kwamba kipindi fulani wakiwa katika mazoezi kocha huyo alikata kumpa mkono Pogba. Miongoni mwa watu wanaokisiwa kuwa huenda watarithi mikoba ya Mourinho ni pamoja na Zinedine Zidane aliyekuwa meneja wa Real Madrid, meneja wa Atletico Madrid Diego Simeone na meneja wa sasa wa Tottenham Hotspur Mauricio Pochettino na meneja wa zamani wa Chelsea Antonio Conte. Kwa sasa Guna Salskjaer amechukua mikoba ya Mourinho kwa muda.
Na Shirikisho la Soka Duniani FIFA limetangaza kuwa asilimia 50 ya watu wote duniani ilitazama fainali za Kombe la Dunia mwezi Julai mwaka huu nchini Russia. FIFA imenukuu takwimu mpya zilizotolewa na mashirika mbalimbali ikiwemo IWC, zinazoonesha kwamba watu bilioni 3.5 walitazama ima sehemu ndogo, mchuano au mechi zote za mashindano hayo ya kimataifa yaliyofanyika nchini Russia kati ya Juni 14 na Julai 15 mwaka huu.
…………………....TAMATI……………….