Jan 03, 2019 12:19 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 813 na sura tunayozungumzia hivi sasa ni ya 37 na Ass’Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 102 ambayo inasema:

فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَىٰ فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَىٰ ۚ قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ ۖ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّابِرِينَ

Basi alipo fika (Ismail) umri wa kuandamana na baba yake katika kazi zake, (baba mtu) alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Ibrahim (as) alimwomba Allah amruzuku mtoto mwema. Aya tuliyosoma inasema: Mtoto ambaye Allah SW alimjaalia kupata Mtume wake huyo, alipochuchuka na kufikia rika la kijana chipukizi, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwamuru Nabii Ibrahim kwa njia ya ndoto amchinje mwanawe huyo katika njia ya Mola wake. Hakuna shaka kwamba  sharti la kutekeleza amri hiyo, mbali na kuridhiwa na baba mtu lilikuwa ni kupata ridhaa ya mtoto mtu pia. Kwa hivyo Ibrahim (as) alimwambia mwanawe Ismail: Nimeamrishwa kufanya jambo hilo, je unao utayari wa kulipokea na kuliridhia jambo hili gumu au la? Nini rai yako? Yaani mtoto kuchinjwa na baba yake mwenyewe?! Ni wazi kwamba kwa mtu wa kawaida, kama ataamrishwa kufanya hivyo na Allah, atauliza tu: Ee Mola wangu, vipi unanitaka nifanye jambo hili?! Kama ungekuwa unataka yawe haya, ni bora tangu mwanzo usingenipa kabisa mtoto kama huyu. Na kama umepanga mtoto huyu auawe katika njia yako, kwa nini jambo hili nilifanye mimi ambaye ni baba yake?! Lakini Mitume, kabla ya kuwa kwao Mitume, walikuwa waja halisi wenye kujisalimisha na kutii kikamillifu maamrisho ya Mola wao. Kwa mtazamo wao, Allah SW ni Mola Mjuzi na Mwenye Hekima; na kwa hivyo kila analoamuru, linatokana na ujuzi na hekima yake isiyo na kikomo. Kwa hivyo hakuna sababu yoyote kwa mimi Ibrahim niliye na elimu na uwelewa wenye mpaka maalumu kutaka kujua kwa ukamilifu sababu ya amri hiyo ya Mola. Lakini jibu la kijana mdogo Ismail, nalo pia likawa ni hilohilo, kwamba ewe baba, kipenzi cha roho yangu, fanya alivyoamrisha Allah; yaweke kando mahusiano ya mzazi na mwana na huruma za kibinadamu, na fikiria kutekeleza amri uliyopewa. Japokuwa hili ni jambo gumu mno, lakini nitastahamili na kuvumilia tabu zote kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mola Mlezi pekee wa ulimwengu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, ndoto za Mitume ni aina moja wapo ya Wahyi wanaoteremshiwa. Lakini kwa watu wengine haiwi hivyo. Kwa hivyo mtu wa kawaida hawezi kutegemea ndoto aliyoota na kuifanya hoja ya kujiwajibishia jambo yeye mwenyewe au watu wengine. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, mapenzi ya mtoto yasimzuie mtu kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu au kufanya madhambi na kumwasi Mola. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, kuweza kutekeleza mtu wajibu wake kunahitaji subira na istiqama. Kwa hivyo ugumu wa jambo usitufanye tuasi na kukhalifu kutekeleza amri za Mola wetu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 103 hadi 105 ambazo zinasema:

 فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ

Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji.

وَنَادَيْنَاهُ أَن يَا إِبْرَاهِيمُ

Tulimwita: Ewe Ibrahim!

قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا ۚ إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ

Umekwisha isadikisha ndoto. Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa watendao mema.

Baada ya Ismail kutoa ridhaa yake na kutangaza utayari wa kutekeleza amri ya Allah, ambalo lilikuwa dhihirisho la jinsi baba  na mtoto wake walivyojisalimisha kwa Mola wao, Nabii Ibrahim aliulaza uso wa mwanawe kifudifudi juu ya ardhi, akawa ameshajiandaa tayari kumchinja. Ni katika lahadha na hali hiyo ikanadi sauti kumwambia, ewe Ibrahim, sisi hatukutaka umchinje mwanao, tulichotaka ni kuupima moyo wako, kuona unavyoweza kujivua na kutekwa na mapenzi ya mwana; na naam, wewe umeufuzu mtihani huu mgumu. Tulilokuamrisha ndotoni ulitekeleze umelitekeleza kwa ukamilifu na umeonyesha kuwa una nia na dhamira ya kweli ya kutekeleza amri ya Mola wako na wala huna ajizi wala ulegevu katika kufanya hivyo. Ijapokuwa Ismail hakuchinjwa, lakini nia ya Nabii Ibrahim (as) ilikuwa ni kumchinja mwanawe katika njia ya Allah. Na kwa hivyo badala ya kutekeleza amali yenyewe, alitakabaliwa kwa nia yake hiyo tu aliyokuwa nayo. Kimsingi katika mafundisho ya Uislamu kima na thamani ya kila tendo linategemea nia na dhamira yake, na ndipo ikafika hadi nia anayokuwa nayo muumini ya kufanya jambo la heri ikawa na thamani zaidi kuliko amali yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kujisalimisha kwa Allah na kuwa na t’aa kamili ya kutekeleza maamrisho yake ni moja ya sifa za ukamilifu wa Mitume na mawalii wa Allah. Kimsingi ni kwamba, amali yenye thamani hasa ni ile inayofanywa kwa kujisalimisha kwa Mola na kwa ajili ya kupata radhi zake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakati mwengine maamrisho ya Allah huwa ni kwa ajili ya kumtahini mja. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba hakuna mpaka na kizuizi cha kufikia ukamilifu wa umaanawi. Kuna wakati kijana chipukizi (kama Ismail) huweza kukwea kwa kasi daraja za ukamilifu, akaandamana na kupiga hatua mbele sambamba na mawalii wakubwa wa Allah (kama Ibrahim (as)) katika njia hiyo. Vile vile aya hizi zinatuelimisha kuwa, wema na ihsani hauko katika masuala ya fedha tu, lakini kuyatoa mhanga mtu maisha yake katika njia ya Allah, nayo pia ni aina mojawapo ya wema na ihsani. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 813 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, aviongoe vizazi vyetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

 

Tags