Jan 03, 2019 23:22 UTC
  • Ijumaa tarehe 4 Januari 2019

Leo ni tarehe 27 Rabiuthani 1440 Hijria sawa na 4 Januari mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 446 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1573, Papa Gregory VII, kiongozi wa Wakristo katika karne ya 16, aliitisha mkutano maarufu kwa jina la mkutano wa 'upokonyaji'. Mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi wa kidini kutoka nchi za Kikristo, ulichukua uamuzi wa kuwapokonya wafalme wa nchi hizo mamlaka ya kuchagua viongozi wa kidini wa Kikristo. Uamuzi huo uliwakasirisha watawala hao na kusababisha vita vya umwagikaji damu vilivyodumu kwa miaka kadhaa, kati ya Mapapa na Wafalme wa Ulaya.

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1961, ulifanyika mkutano wa kisiasa huko Casablanca nchini Morocco kwa shabaha ya kubuni msimamo mmoja wa kisiasa wa Kiafrika. Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi za Algeria, Ghana, Guinea, Mali, Misri na Morocco. Lengo la mkutano huo lilikuwa kuanzisha kundi moja la kijeshi na soko la pamoja la nchi za Afrika.

Casablanca, Morocco

Tarehe 14 Dei miaka 40 iliyopita wakati wa kilele cha harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah, Jenerali Robert E. Huyser aliyekuwa mshauri mkuu wa kijeshi na Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga la Marekani aliwasiri kwa siri mjini Tehran. Jenerali Huyser alikuwa na jukumu maalumu la kuisaidia serikali ya Marekani katika kuchukua maamuzi ya baadaye na kupata habari za ndani za Iran katika kipindi cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika kipindi chote cha zaidi ya siku 30 za kuwepo kwake mjini Tehran Jenerali Huyser alikutana mara moja tu na Shah na katika kikao hicho iliainishwa saa na siku ya kuondoka Shah nchini Iran.

enerali Robert E. Huyser

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea na kufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa Swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu.

Ayatullah Ahmad Khansari

Tarehe 4 Januari miaka 8 iliyopita alifariki dunia Mohamed Bouazizi, kijana muuza mboga wa Tunisia, siku 18 baada ya kujichoma kwa moto katika mji wa Buzid akilalamikia ukandamizaji na dhulma ya serikali ya nchi hiyo.

Kujichoma moto kijana huyo muuza mboga kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa nchi hiyo na kuwa sababu ya kupinduliwa dikteta Zainul Abidin bin Ali. Kitendo hicho cha Bouazizi pia kilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi.

Mohamed Bouazizi