Jan 05, 2019 07:43 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 815, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 114 hadi 116 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ مَنَنَّا عَلَىٰ مُوسَىٰ وَهَارُونَ

Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni.

وَنَجَّيْنَاهُمَا وَقَوْمَهُمَا مِنَ الْكَرْبِ الْعَظِيمِ

Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na tabu kubwa.

وَنَصَرْنَاهُمْ فَكَانُوا هُمُ الْغَالِبِينَ

Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizotaja baadhi ya neema ambazo Allah SW alimjaalia Nabii Ibrahim (as). Aya hizi tulizosoma zinaashiria rehma na fadhila za Mola Mwenyezi kwa Nabii Musa na ndugu yake Haruna (as). Kwanza zinaeleza kwa ujumla kwamba Allah aliwajaalia kuwa miongoni mwa waja aliowakirimu kwa neema zake, kisha zikabainisha baadhi ya neema hizo. Fadhila na ihsani ya kwanza ya Mwenyazi Mungu Mtukufu kwa Manabii Musa na Haruna na kaumu yao ya Bani Israil ilikuwa ni kuwakomboa na madhila na dhulma za Firauni na watu wake, na kuwawezesha kuwashinda maadui zao hao. Firauni alikuwa mtawala dhalimu na mwagaji damu wa Misri aliyekuwa akiwafanya watumwa na kuwatumikisha wanaume wa Bani Israil, kuwafanya wajakazi wanawake wao na kuwachinja watoto wao wa kiume. Ni katika mazingira hayo, Allah SW alimpa Utume Nabii Musa (as) na kumpa jukumu la kwenda kuwakomboa Bani Israil. Kwa imani thabiti aliyokuwa nayo kwa Allah SW, Mtume huyo aliweza kuandaa mazingira na njia ya kuwaokoa Bani Israil na kuwatoa kwenye mateso na madhila hayo makubwa. Kwa rehma za Mwenyezi Mungu na juhudi zake, Bani Israil waliuvuka mto Nile salama u salimini; na Firauni na jeshi lake wakaghariki kwenye maji ya mto huo. Na hivyo ndivyo Bani Israil, waliokuwa hawana silaha yoyote mikononi mwao, walivyoweza kumshinda Firauni na jeshi lake lililojizatiti kwa silaha na wakaweza kukomboka na kujitoa kwenye makucha ya dhalimu huyo. Baada ya kuangamizwa Firauni na watu wake, Bani Israil walimilikishwa mali na utajiri wao pamoja na makasri na mabustani yao. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kwamba, rehma na ihsani ya Allah kwa Mitume waliopita huwa sababu ya kupata faraja na utulivu waumini katika zama zote za historia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuondokewa na majonzi, huzuni na mashinikizo ya kinafsi na kupata utulivu wa kiroho ni miongoni mwa neema kubwa za Allah. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu huwa daima wanawafikiria watu wanaoonewa na kunyongeshwa, na wanawahurumia na kuwa pamoja nao katika mateso na majonzi yao.  Nyoyo za waja wa kweli wa Allah hupoa na kutulia pale watu wanaodhulumiwa wanapokomboka na dhulma na madhila ya madhalimu na majabari, na kuishi katika utulivu na amani.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 117 hadi 119 ambazo zinasema:

وَآتَيْنَاهُمَا الْكِتَابَ الْمُسْتَبِينَ

Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha.

وَهَدَيْنَاهُمَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ

Na tukawaongoza kwenye Njia Iliyo Nyooka.

وَتَرَكْنَا عَلَيْهِمَا فِي الْآخِرِينَ

Na tukawaachia (jina jema) kwa walio (kuja) baadaye.

Baada ya aya zilizotangulia kutaja neema ya kukombolewa na kuokolewa Bani Israil na madhila na mateso ya Firauni, aya tulizosoma zimezungumzia na kutilia mkazo neema kubwa zaidi waliyojaaliwa watu hao, ambayo ni kuteremshiwa Kitabu cha mbinguni cha kuiongoza na kuielekeza jamii yao kwenye saada na fanaka ya duniani na akhera. Ni wazi kwamba jamii iliyokomboka na kutoka kwenye makucha ya ufirauni inahitajia sheria na kiongozi wa kidini ili ipate kutengenea na ili isije mara nyingine kukumbwa tena na udikteta na uistikbari. Kwa hivyo kuteremshwa Taurati, ambayo ndani yake mlikuwa na sheria zilizohitajiwa na kaumu ya Bani Israil, na vile vile kuwa na kiongozi mweza kama Musa (as) zilikuwa neema kubwa zaidi kwa kaumu hiyo ili kuwezesha kujengwa jamii safi na salama ya kuelekea kwenye ukamilifu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwaokoa na kuwatoa watu kwenye makucha ya dhulma na udikteta kunawafungulia kwa wepesi zaidi njia ya kuufikia uongofu wa Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa vitabu vya mbinguni vinamfunza mwanadamu njia na namna sahihi ya kuishi, lakini ni kwa sharti kwamba visitiwe mkono, vikabadilishwa na kupotoshwa. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mwenyezi Mungu amewasifu na kuwaenzi Mitume wake ndani ya Qur’ani; na kutajwa kwa wema na kuacha jina jema ni moja ya rasilimali ya kijamii ya Mitume wote katika zama zote za historia. Aya ya 120 hadi 122 za sura yetu ya Ass ’Affat ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu ya leo. Aya hizo zinasema:

سَلَامٌ عَلَىٰ مُوسَىٰ وَهَارُونَ

Amani kwa Musa na Haruni.

إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ

Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema.

إِنَّهُمَا مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ

Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio waumini.  

Katika sehemu ya mwisho ya mfululizo wa aya hizi zinazo wazungumzia Manabii Musa na Haruna (as), Allah SW amewatakia amani na rehma Mitume wake hao na kulitaja hilo ndani ya Qur’ani ili liwe somo kwa waumini, kwamba kila wakati wawe wakiwasalia na kuwatakia rehma na amani waja hao wateule na kuenzi kazi ngumu na kubwa mno waliyoifanya. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba rehma na amani ya Allah kwa Manabii hao wawili na waumini ni jambo la kuendelea na la kudumu; na kwa hivyo katika zama zote za historia, kila mtu aliye muumini, msafi na mwenye kuwatendea watu mema atakuwa miongoni mwa wenye kupata neema na malipo hayo. Aya ya mwisho tuliyosoma kuhusu Manabii Musa na Haruna (as) imeashiria daraja ya uja halisi na kujisalimisha kwao kwa Allah SW na kueleza kwamba, wao walikuwa miongoni mwa waja wetu walioamini. Istilahi hii imetumiwa ndani ya Qur’ani kuhusiana na Mitume wote kwa kuwataja kuwa ni ibaad, kwa maana ya watumwa au waja halisi wa Mwenyezi Mungu. Neno abd, ni kinyume cha neno maulaa, likimaanisha sifa ya kusalimu amri kikamilifu waliyokuwa nayo Mitume kwa maamrisho ya Allah, kinyume na walivyo watu wengi ambao hawatii maamrisho yote ya Mola kwa ukamilifu wake; bali hutekeleza yale tu wanayojua sababu na hekima ya kuamrishwa kwake, yenye maslaha na yasiyo na madhara kwao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwasalia na kuwatakia rehma na amani waja wateule wa Allah ni jambo zuri ambalo ametufunza Mola wetu; na hii inamaanisha kwamba sala hizo na salamu tunazozituma, zinapokewa na waja hao watukufu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hatua yoyote inayochukuliwa kwa madhumuni ya kubainisha mafundisho ya dini na kuiongoza jamii kuelekea kwenye uongofu ni aina mojawapo ya wema; na hiyo ni moja ya sifa maalumu za waja wa kweli wa Allah. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, rehma za Allah kwa watenda mema ni kaida na utaratibu wenye kuendelea katika zama zote za historia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 815 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwafikishe kufanya mambo mema na ya heri yatakayokuwa sababu ya kutajwa kwa wema na watakaokuja baada yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakشatuh.

Tags