Ulimwengu wa Spoti, Jan 7
Hujambo mpenzi msikilizaji na hususan mfuatiliaji wa spoti, na karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali ya dunia.....
Kombe la Asia
Michuano ya Kombe la Asia imeng'oa nanga huku timu mwenyeji Umoja wa Falme za Kiarabu ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na Bahrain katika mechi ya ufunguzi Jumamosi. Nusra mchuano huo wa Kundi A uishie kwa sare tasa, lakini mchezaji Mohamed Al Rohaimi aliuvunja mzingiro na kuifungia Bahrain bao la aina yake kunako dakika ya 78.
Huku zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo umalizike, kiungo Ahmed Khalil alisawazisha mambo ya kuwapa ahueni wenyeji. Katika mechi nyingine za ufunguzi, bingwa mtetezi, Australia imeanza vibaya mashindano hayo, kwa kukubali kuzabwa bao moja la uchungu na Jordan. Bao hilo la pekee na la ushindi la vijana wa Kiarabu lilivurumishwa kwenye nyavu na Anas Bani Yaseen katika dakika ya 26.
Huenda Australia itapunguza machungu yake hayo itakaposhuka dimbani kuvaana na Palestina katika mechi ya Kundi B Januari 11, wakati ambapo Syria itakuwa inatoana udhia na Jordan. Katika mechi nyingine ya ufunguzi ya Kundi B, vijana wa Kipalestina waliilazimisha Syria sare tasa ya kutofungana, ingawaje Syria ilitawala mchezo huo katika takriban muda wote. Mambo yalizidi kuwaendea segemnege Palestina katika dakika ya 69, baada ya mchezaji wake Mohammed Saleh kupigwa kadi nyekundu. Hata hivyo hawakuruhusu goli. Kwengineko, India iliigaragaza Thailand mabao 4-1, huku straika mkongwe Sunil Chhetri akifanikiwa kucheka na nyavu mara mbili. Bao la kufutia machozi la Thailand lilifungwa na nahodha wa timu hiyo, Teerasil Dangda.
Baada ya kupambana na Yemen katika mchuano wake wa ufunguzi, timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatazamiwa kuvaana na Vietnam Januari 12, katika Uwanja wa Al Nahyan mjini Abu Dhabi, huku ikicheza mchuano wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Iraq, katika Uwanja wa Al Maktoum mjini Dubai Januari 16. Duru ya 17 ya mashindano hayo ya kibara yanayofahamika kama AFC Asian Cup ilianza Jumamosi ya Januari 5 na inatazamiwa kufunga pazia lake Februari Mosi. Mashindano ya mwaka huu yanaonekana kuwa makubwa zaidi, kwa kuwa yanazishirikisha nchi 24, kutoka 16 huko nyuma. Mashindano hayo ya kikanda yameandaliwa na Shirikisho la Soka Asia CAF.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi
Michuano ya Kombe la Mapinduzi inaendelea kurindima visiwani Zanzibar, huku klabu ya Simba ikifanikiwa kutinga nusu fainali japo kwa taabu. Simba walishuka dimbani Jumapili kuvaana na KMKM, lakini walicheza mchezo uliokuwa kinyume kabisa na matarajio ya mashabiki wao, na kupata ushindi mwembamba wa goli moja. Bao hilo la pekee la Simba lilitiwa kimyani na chipukizi Rashid Juma katika mchezo huo wa Kundi A uliopigwa Jumapili usiku katika Uwanja wa Amani.
Kocha mkuu wa Simba Patrick Aussems baada ya vijana wake kujikatia tiketi ya nusu fainali ya michuano ya Mapinduzi Cup, amekiondoa kikosi hicho visiwani humo na kukipeleka Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika (CAF Champions League) dhidi ya Js Saouro. Aussems ameeleza kuwa kwa sasa licha ya timu yake kupata ushindi mwembamba dhidi ya KMKM kwa goli 1-0 tena kwa tabu, amesema hajali kuhusiana na matokeo anachojali ni jeraha la mchezaji wake Erasto Nyoni aliyeumia goti lake la kulia, hivyo kwa sasa Simba inaondoka na italeta team B. Katika mechi nyingine iliyopigwa wikendi, Azam FC iliisasambua Yanga mabao 3-0 katika hatua ya makundi. Magoli ya Azam yalifungwa na Obrey Chirwa aliyetikisa nyavu za Yanga mara mbili, huku goli la tatu likifungwa na Ennock Atta. Matokeo hayo yameifanya Azam FC kuwa na alama nne wakati Yanga wana pointi tatu, hivyo watahitaji ushindi katika mechi yao dhidi ya Malindi ili kujiweka pazuri na kuweza kutinga hatua ya nusu fainali.
Dondoo za Hapa na Pale
Mashindano ya tenisi kwa vijana Afrika wenye umri wa miaka 14 na 16 (Tennis Zonal Championship) yanatarajiwa kufungua pazia lake Januari 7 na kuendelea hadi Januari 15, katika viwanja wa Gymkhana, jijini Dare es Salaam, nchini Tanzania. Rais wa Chama cha Tenisi Tanzania TTA, Denis Makoi amesema nchi 10 zitakazo shiriki mashindano hayo ya kikanda ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Comoro, Sudan, Somalia, Ethiopia, Eritrea, Ushelisheli, pamoja na mwenyeji Tanzania. Washindi watapata tiketi ya kushiriki mashindano ya Tenisi ya Afrika mwezi Aprili mwaka huu, katika nchi za Afrika Kusini na Morocco.
Katika Ligi Kuu ya Soka Uingereza, klabu ya Liverpool ilikubali kupoteza mchezo wake dhidi ya Manchester City kwa kufungwa mabao 2-1 usiku wa kuamkia Ijumaa. Mabao ya City yaliwekwa kimiani na Sergio Arguero na Leroy Sane huku Liverpool ikipata la kufutia machozi kupitia kwa Roberto Firmino.
Ushindi huo wa Manchester City unakuwa wa kwanza baada ya mechi tano mfululizo katika EPL kushindwa kupata matokeo mbele ya Liverpool. Kupoteza kwa Liverpool kumeifanya ikubali kufungwa mabao mawili msimu huu ndani ya mechi moja na ikipoteza mchezo wa kwanza. Licha ya kichapo hicho, lakini Liverpool inaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 54, alama 4 zaidi ya Man City inayoshika nafasi ya pili, huku orodha ya tatu bora ikifungwa na Tottenham yenye alama 48.
Kwengineko, mchezaji nyota wa soka wa timu ya Juventus, Cristiano Ronaldo amenyakua mataji mawili ya kimataifa mjini Dubai, Imarati. Ronaldo amepewa tuzo ya mchezaji bora mwaka 2018 na pia goli lake likatajwa kuwa bao la mwaka. Ronaldo amewapiku wachezaji Antoine Griezmann and Kylian Mbappe katika tuzo hiyo ya Globe Soccer Awards. Nyota wa Brazil, Ronaldo Luís Nazário de Lima ameshinda Tuzo ya Mchezaji Mkongwe (Lifetime Achievement).
Wakati huohuo, Shirikisho la Soka Afrika CAF, Jumanne hii ya Januari 9 linatazamiwa kutoa tuzo za wanasoka wa Afrika waliofanya vizuri mwaka uliomalizika wa 2018. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo itafanyika katika Jiji la Dakar nchini Senegal na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa na michezo, wakiwemo Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Giann Infantino na Rais wa Shirikisho la Kandanda barani Afrika CAF, Ahmad Ahmad.
Mshindi wa mwaka jana, raia wa Misri Mohammed Salah anachuana na mchezaji mwezake wa Liverpool Sadio Mane na nyota wa Arsenal na timu ya Taifa ya Gabon, Pierre Emerick Aubemeyang. Kwa upande wa wanawake tuzo hiyo inawaniwa na mshindi wa mwaka jana Asisat Oshoala wa Nigeria, na raia mwenza Fransisca Ortega, pamoja na Thembi Kgatlana wa Afrika kusini ambaye alikuwa mfungaji bora wa fainali za Afrika za mwaka 2018 zilizofanyika nchini Ghana.
…………………….TAMATI…………….