Jan 15, 2019 06:29 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii (4)

Sehemu ya Tatu: Mapinduzi ya Kiislamu yalivyojipambanua na mapinduzi mengine makubwa duniani. Msikilizaji mpenzi wa Radio Tehran, ni matumaini yangu kuwa hujambo popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza kipindi hiki kinachokujia kila wiki, siku na saa kama hii, kinachozungumzia Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii.

Endelea kuwa nami hadi mwisho wa mazungumzo yetu, ili kuweza kufaidika na yale niliyokuandalia katika mfululizo huu wa tatu, ambapo tutaendelea kuzungumzia mambo yanayoyatafautisha na kuyapambanua Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengine makubwa duniani.

******

Nukta moja muhimu zaidi inayoyapambanua na kuyatafautisha Mapinduzi ya Kiislamu na mapinduzi mengine makubwa, ni hali ya kijiopolitiki ya Iran. Iran iko kwenye eneo la Mashariki ya Kati, ambalo kabla yake, hayajawahi kutokea Mapinduzi ya Kiislamu au mapinduzi mengine, katika nchi yoyote ile ya eneo hili. Kwa hivyo Mapinduzi ya Kiislamu, yalikuwa mapinduzi ya mwanzo katika Mashariki ya Kati, yakiwa ni mabadiliko ya aina yake kutokea katika eneo hili, ambalo madola ajinabi yana satua na ushawishi mkubwa ndani yake. Nukta nyingine kuhusu hali hiyo ya jiopolitiki ni kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu yalitokea nchini Iran, ambayo ilikuwa moja ya nchi wazalishaji wakubwa wa mafuta na gesi duniani; na nishati mbili hizo zilikuwa na nafasi muhimu kutokana na taathira zao kwa siasa za kimataifa. Umuhimu wa mafuta na gesi ya Iran ulikuwa moja ya sababu kuu zilizoifanya Iran iwe na umuhimu kwa madola makubwa. Tunaweza kusema pia kwamba, moja ya sababu kuu za kutokea mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 19 Agosti mwaka 1953 (28 Mordad mwaka 1332) hapa nchini Iran, ilikuwa ni hatua ya kutaifishwa mafuta, iliyochukuliwa mwaka 1951 (1329) na kukatwa mikono ya Uingereza iliyokuwa ikiunyonya utajiri huo wa Iran. Mazingira kama hayo, hayakuwahi kuwapo kabla katika nchi nyingine yoyote ile yalikowahi kutokea mapinduzi. Zaidi ya hayo ni kwamba, mtikisiko uliojitokeza kutokana na kupanda bei ya mafuta katika muongo wa 1970, uliuathiri pia hata mfumo wa kimataifa, na kutokea mapinduzi nchini Iran kungeliweza kusababisha kupanda tena bei ya mafuta, ambayo yana umuhimu mkubwa sana kwa uchumi wa dunia. Suala hili, mbali na kubainisha umuhimu wa kijiopolitiki iliokuwa nao Iran, linaonyesha pia jinsi utawala wa kifalme wa Iran ulivyokuwa ukipata uungaji mkono maalumu wa madola makubwa kutokana na kudhamini nishati ya mafuta na gesi kwa nchi za viwanda; lakini pamoja na kuwepo hali na mazingira hayo, Mapinduzi ya Kiislamu yaliweza kutokea nchini Iran.

Ustawi uliopatikana katika uzalishaji wa feleji nchini Iran katika kipindi cha miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu

 

Nukta nyingine inayoyatafautisha Mapinduzi ya Kiislamu na mapinduzi mengine makubwa ni kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa mapinduzi ya kwanza ya kidini duniani na yakawa sababu ya kuhuika dini katika mfumo wa kisiasa wa Iran na hata katika siasa za kimataifa. Kabla ya kutokea Mapinduzi ya Kiislamu, zilikuwa zimejitokeza harakati nyingi za Kiislamu za Kishia na zisizo za Kishia katika Ulimwengu wa Kiislamu, ambazo zilileta vuguvugu la kujivua na pingu na minyororo ya unyonyaji na udikteta. Lakini hakuna hata moja kati ya mavuguvugu hayo lililogeuka kuwa mapinduzi yenye idiolojia makini na ya nchi nzima na kuwahamasisha wananchi wote waungane pamoja dhidi ya mfumo tawala. Lakini Mapinduzi ya Kiislamu yalizitumia thamani za kidini na kimadhehebu na kuthibitisha uwezo yalio nao kimuundo, kwa kuwezesha kutokea mapinduzi halisi ya Kiislamu nchini Iran. Mapinduzi ya Kiislamu, yalibadilisha kikamilifu misingi ya mahusiano ya kisiasa, kijamii na kiutamaduni ndani ya Iran, huku yenyewe yakiwa yamejumuisha pamoja vielezo vya mapinduzi ya kisiasa na kijamii. Ayatullah shahidi Murtadha Mutahhari ameeleza katika tathmini na tafsiri yake aliyotoa kuhusu maana ya Mapinduzi ya Kiislamu, kwa kueleza kwamba, mapinduzi hayo ni tawi mojawapo la mapinduzi ya Manabii, hususan mapinduzi ya zama za mwanzoni mwa Uislamu. Ayatullah Mutahhari ameeleza yafuatayo katika kitabu chake kiitwacho, "Kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu": "Mapinduzi ya zama za mwanzoni mwa Uislamu, pamoja na kuwa mapinduzi ya kidini na Kiislamu, wakati huo huo yalikuwa mapinduzi ya kisiasa, kimaanawi, kijamii, kiuchumi na kimaada pia. Yaani, uhuru, ukombozi, uadilifu, kutokuwepo ubaguzi wa kijamii na mianya ya kitabaka yamo kwenye maandiko ya mafundisho ya Kiislamu. Hakuna hata moja kati ya hayo yaliyoashiriwa, ambalo liko nje ya Uislamu; na mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, sababu yake ni kuwa hayakujifunga na upande wa kimaanawi pekee, bali yalijumuisha pia ndani yake pande mbili za kimaada na kisiasa kwa kuzioanisha na mafundisho ya Kiislamu yaliyomo ndani ya pande hizo. Kwa mfano, mapambano yenyewe yamefungamana na umaanawi wa kina, na kwa upande mwingine, moyo wa kupigania uhuru na kujikomboa unaonekana katika maamrisho yote ya Kiislamu."

Moja ya picha muhimu za kihistoria. Imam Khomeini akiwa katikati ya umati wa wananchi wa Iran

 

Katika kuzungumzia vielezo na sifa zinazoyatafautisha Mapinduzi ya Kiislamu na mapinduzi makubwa mengine duniani, waandishi wengi wameashiria suala la dini. Miongoni mwao ni Jalal Derakhshe ambaye anaitakidi kwamba: "Mapinduzi ya Kiislamu, kinyume na mapinduzi mengine makubwa kama ya Ufaransa na Urusi, ambayo msingi wake ulikuwa ni kuitenganisha siasa na dini, yalijengeka kutokana na itikadi na imani za watu katika jamii juu ya dini; na Uislamu, ukiwa ni imani na itikadi ya moyoni waliyokuwa nayo wananchi wa Iran, ulikuwa na nafasi kuu katika kupatikana ushindi wa wananchi hao."

Nikki Keddie, naye pia anaitakidi kwamba: "Harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran, ilifanyika kwa lengo la kubadilisha vigezo vya kifikra na kiutamaduni vya Kimagharibi vilivyokuwa vimetawala katika anga ya jamii, na badala yake kuasisi mfumo unaoendana na chimbuko la utamaduni na ustaarabu wa jamii ya Waislamu wa Iran. Kwa kuzingatia kwamba utambulisho wa kihistoria na kiutamaduni wa taifa la Iran, kwa muda wa karne na karne ulikuwa umejengeka na kupata maana yake halisi kwa kufungamana na fikra na amali za kidini sambamba na kuhusishwa dini katika masuala yote ya maisha ya kijamii, uenezaji fikra yoyote iliyokuwa ikipuuza na kutoijali dini, ulisababisha migogoro na misuguano ya kifikra, ambayo taathira zake zilienea hadi kwenye nyuga zote za kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi za Iran. Kwa kukabiliana na mtazamo huo uliokuwa dhidi ya dini, Mapinduzi yalijaribu kutoa jibu mwafaka kwa mgogoro huo mpya; na kwa hivyo lengo muhimu zaidi la Mapinduzi, likawa ni kuhuisha dini na kuleta kigezo kipya kinachotokana na utambulisho wa kidini na kitaifa wa Iran."

Japokuwa ni jambo lisilo na shaka, kwamba masuala ya kiuchumi na kisiasa, nayo pia yalichangia katika kutokea Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, lakini kama wanavyoitakidi wananadharia wengi, sababu kuu iliyowafanya watu wamiminike mabarabarani na kushiriki kwenye maandamano ya umwagwaji wa damu kwa muda wa miezi kadhaa, ilikuwa ni mgongano na mvutano baina ya utawala uliokuwepo na thamani na hukumu za Kiislamu; na kile kilichopiganiwa na kutakiwa badala ya hali hiyo, ni jamii ya Kiislamu itakayosimamisha misingi, thamani na malengo matukufu ya Uislamu.

Mpenzi msikilizaji, sehemu ya tatu ya kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii, imefikia tamati. Usiache kujiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika sehemu ya nne ya mfululizo huu. Nakushukuru kwa kunisikiliza.