Jan 21, 2019 07:03 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Jan 21

Hujambo mpenzi msikilizaji wa na haswa mpenzi na mfuatiliaji wa spoti, na karibu tuangazia baadhi ya matukio ya michezo ndani ya siku saba zilizopita.

Kombe la Asia: Iran yatinga robo fainali

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumapili ilishuka dimbani kuvaana na Oman katika mchuano wa muondoano wa Kombe la Asia. Katika mchuano huo wa kusisimua uliopigwa katika Uwanja wa Mohammed bin Zayed mjini Abu Dhabi, Iran iliisasambua Oman mabao 2-0, na hivyo kujikatia tiketi ya kucheza robo fainali. Nusra Oman ipate goli la kwanza na kuwa kifua mbele baada ya kupewa penati, dakika tatu tu baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza mchezo, lakini kipa matata wa Iran Alireza Beiraanvand akaupangua mkwaju huo uliopigwa na Ahmed Al Mahaijri. Kiungo wa Iran, Alireza Jahanbakhsh alistafidi na uzembe wa mabeki wa Oman na kujaza wavuni bao la kwanza kwa Iran katika dakika ya 32.

Wachezaji wa Team Melli wakishangilia bao

 

Dakika tisa baadaye, mshambuliaji wa Iran Mehdi Taremi alipigwa kiatu katika sanduku la hatari la Oman na Muomani Saad Al Mukhaini. Timu hiyo ya Iran ikapewa penati, ambapo nahodha wake Ashkan Dejagah hakusita kupachika kombora wavuni, na kuihakikishia Iran ushindi.

Katika kipindi cha pili vijana wa Kiirani walipoteza fursa kibao za kuongeza mabao, lakini mastrika wakacheza ndivyo sivyo, labda wakitosheka na alama tatu muhimu ambazo walikuwa washavuna. Baada ya ushindi huo mnono, vijana wa Team Melli sasa watavaana na China katika robo fainali siku ya Alkhamisi katika Uwanja wa Mohammed bin Zayed.  China imetinga robo fainali baada ya kuizaba Thailand mabao 2-1.

Wachezaji wa kandanda wa Iran

 

Kabla ya hapo, Iran iliendelea kuwa kilele mwa Kundi D licha ya kuilazimisha Iraq sare tasa katika mchuano mwingine wa Kombe la Asia huko Imarati Jumatano iliyopita. Katika mechi hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa Al Maktoum mjini Dubai, timu mbili hizo zilitoana jasho lakini hakuna aliyefanikiwa kuona lango la mwingine, hii ikiwa ni mara ya saba kwa watani hao wajadi kukutana katika mechi za AFC Asia Cup. Iran imeshinda taji hilo mara 3, mara ya mwisho ikilitwaa kombe hilo zaidi ya miongo mitatu iliyopita. Iraq ilishinda kombe hilo mara ya mwiso mwaka 2007.

Kwengineko, Qatar licha ya kutokuwa na mashabiki uwanjani, ilifanikiwa kuigaragaza Saudi Arabia mabao 2-0 katika mchuano wa Kundi E siku ya Alkhamisi. Mabao hayo ya Qatar yalipachikwa wavuni na Almoez Ali. Qatar inatazamiwa kutinga robo fainali kiwepesi, kwani mchuano ujao itakula kwenye sahani moja na Wairaqi.

Iran U-23 yaipepeta Kuwait

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 iliigaragaza Kuwait mabao 5-0 katika michuano wa mataifa manne uliopigwa Qatar siku ya Ijumaa. Timu hiyo ya mabarobaro wa Iran inayofahamika kama "Omid" au matumaini, ilipata mabao mawili katika kipindi cha kwanza, kupitia wachezaji Alireza Arta na Allahyar Sayyadmanesh. Kipindi cha pili mambo yalizidi kuwaendea ndivyo sivyo Waarabu wa Kuwait, na Iran ilifanikiwa kuongeza mabao matatu kupitia Younes Delfi, Amir Hossein Hosseinzadeh na Omid Nourafkan. Iran ilikubali kuchachawizwa na Tajikistan katika mchuano wake wa kwanza, na kuzabwa mabao 2-1. Sasa vijana hao wa Kiirani watalazimika kuishinda mwenyeji Qatar ili iitwae taji hilo. Hapo kabla, timu hiyo ya Iran iliichachafya Syria mabao 3-1 katika mchuano mwingine wa kirafiki, na pia kuambulia sare ya bao 1-1 na Jordan. Vijana hao wa mkufunzi Zlatko Kranjcar wanatumia michuano hii ya kirafiki kama sehemu ya maandalizi ya michuano ya Mabingwa wa Asia itakayoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia AFC mwaka 2020. 

Ligi ya Mabingwa Afrika

Klabu ya Simba ya Tanzania ilichezea mkong'oto na kupokea kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa AS Vita katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Kinshasa huko Kongo DR Jumamosi. Mvua ya magoli ilianzishwa na Makusu aliyefunga magoli mawili dakika ya 14 na 73, mengine yalifungwa na Bopunga dakika ya 19, Ngoma dakika 47 na Kupa ukiwa ni mchezo wa kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wanasimba uwanjani

 

Msemaji wa Simba Haji Manara kupitia Instagram yake ameandika kuwa hata Yanga waliwahi kuwafunga, akisema Wekundu wa Msimbazi sio wa kwanza kupokea kichapo cha namna hiyo, na ada ya mchezo kuna kushinda na kushindwa. Kipigo cha mabao 5-0 ilichokipata Simba kutoka kwa AS Vita kimewashusha hadi nafasi ya tatu katika Kundi D. Nao wafalme wa soka Afrika TP Mazembe ya DRC ilikubali kipigo cha mabao 3-0 ilipoana jasho na CS Constantine katika mchezo wa kundi C wa ligi hiyo, wakati ambapo Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilikuwa inaifunga Wayad Casablanca ya Morocco kwa magoli 2-1 katika kundi A. JS Saoura imeilazimisha sare ya 1-1 Al Ahly ya Misri katika mechi ya kundi D.

Kwengineko, klabu ya Gor Mahia ya Kenya imetinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho licha ya kuambulia sare tasa ilipokwaruzana na New Stars de Douala mjini Limbe nchini Cameroon. Katika mchezo huo mzunguko wa pili uliopigwa Jumapili, Kogalo ilihitaji ponti moja tu ili iweze kupete, ikingatiwa kuwa tayari ilikuwa imechabanga klabu hiyo mabao 2-1 walipokutana katika Uwanja wa Taifa wa Kasarani jijini Nairobi mnamo Januari 13. Droo ya makundi ya Confederation Cup inachezeshwa Jumatatu katika mji mkuu wa Misri, Cairo.

Riadha: Wakenya washinda Marathon Houston na Mumbai

Kwa mara nyingine tena wanariadha wa Kenya wameendelea kuihakikishia dunia kuwa wao ni moto wa kuotea mbali katika mbio za masafa marefu. Mshindi wa Chicago Marathon, Brigid Kosgei aliibuka kidedea katika mbio za Houston Nusu Marathon nchini Marekani siku ya Jumapili na kutwaa medali ya dhahabu. Mwanadada huyo wa Kenya alikata utepe katika dakika ya 65:49, na kuvunja rekodi iliyokuwa imewekwa na Mkenya mwenzake, Mary Wacera ya 66:29. Mkenya mwingine Fancy Chemutai aliibuka wa pili, huku nafasi ya tatu ikitwaliwa na Muethiopia Ruti Aga.

Cosmas Lagat akikata utepe wa ushindi

 

Katika mbio za Mumbai Marathon kwa upande wa wanaume, Cosmas Lagat aliibuka mshindi kwa kutumia saa 2:09:15 akifuatia na Mhabeshi Worknesh Alemu aliyemaliza kwa kutumia saa 2:25:45. Wawili hao wamevunja rekodi ya mbio hizo za Tata Mumbai nchini India (IAAF Gold Label), ambapo mbali na medali, wamezawadia kitita cha dola 45,000 za Marekani.

Dondoo za Hapa na Pale

Tasnia ya michezo inaomboleza mauaji ya mwandishi wa habari za uchunguzi Ahmed Hussein-Suale ambaye alipigwa risasi tatu na watu wasiojulikana wakati akitoka katika mizunguko yake akirudi nyumbani kwake mtaani Madina, viungani mwa mji mkuu wa Ghana, Accra. Mauaji ya kikatili kwa mwandishi huyo aliyevumbua kashfa ya rushwa kwa aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Ghana Akwesi Nyantakyo na kusababisha afungiwe maisha kujihusisha na masuala ya michezo, yameibua gumzo kwenye mitandao ya kijamii kote duniani. Mwandishi huyo alijizolea umaarufu nchini Ghana na Afrika kwa ujumla, kutokana na kufichua siri nyingi juu ya kukithiri kwa rushwa kwenye soka barani Afrika, ambapo yeye pamoja na mwenzake walisababisha refa wa Kenya kuondolewa katika orodha ya waamuzi waliochezesha Kombe la Dunia mwaka 2018, baada ya uchunguzi wao kumbaini kwamba alipokea rushwa.

Kwengineko klabu ya Persepolis ya Iran iliisasambua al-Shahaniyah ya Qatar mabao 4-0 katika mchuano wa kirafiki Ijumaa. Mabao ya klabu hiyo ya Iran yalifungwa na Siamak Nemati, Ali Alipour (2) na Soroush Rafiei.

Persepolis ikishangilia goli

 

Na bondia wa Ufilipino Manny Pacquiao amefanikiwa kutetea Ubingwa wake wa Dunia wa Boxing Welterweight kwa kumpiga kwa pointi bondia Andrien Broner wa Las Vegas, Marekani na kuutetea ubingwa wake wa mkanda wa WBA Welterweight. Andrien aliingia ulingoni kupigana na Pacquiao akiwa na uzito sawa (welterweight) ila umri akiwa na umri wa miaka 29, tofauti ya miaka 11 kati yake na Pacquia. Pambano hilo lilichezwa katika Ukumbi wa MGM Grand na kuhudhuriwa na watu zaidi ya elfu 13. Ushindi huo umempa mwandondi huyo wa Ufilipinoi motisha ya kufanya vyema zaidi hapo baadaye licha ya umri wake.

………………….TAMATI………………..