Jan 29, 2019 02:46 UTC
  • Jumanne, Januari 29, 2019

Leo ni Jumanne tarehe 22 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na 29 Januari mwaka 2019 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 282 iliyopita alizaliwa Thomas Paine, mwanasiasa, mwandishi na mwanamapinduzi wa nchini Uingereza. Baada ya kuhitimu masomo yake ya sekondari alijishughulisha na harakati mbalimbali ambazo hata hivyo hazikuzaa matunda. Hatimaye mwaka 1774, kabla ya kuanza kwa vita vya kupigania uhuru nchini Marekani, aliingia nchini humo na kuanza kujihusisha na uandishi. Makala yake iliyopewa jina la 'Akili Salama' iliwaathiri sana raia na viongozi wa Marekani na hivyo kuwazidishia ari ya kuendeleza harakati za kupigania uhuru. Baadaye aliandika makala iliyopewa jina la 'Mgogoro wa Marekani' ambayo iliwataka raia wote wa nchi hiyo kupambana na ukoloni. Baada ya kukamilika mapinduzi ya Marekani, Thomas Paine alirejea Uingereza ambapo aliunga mkono harakati ya mapinduzi ya Ufaransa na kuandika kitabu alichokipa jina la 'Haki za Mwanadamu.' Hata hivyo serikali ya Uingereza ilimtangaza Paine kuwa haini na hivyo kulazimika kukimbilia Ufaransa ambapo akiwa huko aliteuliwa kuwa mjumbe wa Jumuiya ya kitaifa. Alifariki dunia mwaka 1802 baada ya kuishi barani Ulaya kwa miaka 15.

Thomas Paine

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita Mfalme Faisal wa Kwanza, mtoto wa Hussein Bin Ali Sharif wa mjini Makkah aliteuliwa kuwa mfalme wa Iraq katika mazingira yaliyoandaliwa na Uingereza. Katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Uingereza ilimuahidi Sharif wa Makkah kuwa mtawala wa Hijazi endapo angekubali kupambana na mtawala wa dola la Othmania ambaye alikuwa ameungana na Ujerumani. Hata hivyo kinyume na ahadi yake, London ilimuingiza madarakani Abdul Aziz bin Saud kutawala ardhi ya Hijazi. Uingereza ilichukua hatua hiyo baada ya kuona kuwa, misimamo ya Abdul Aziz ambayo ni ya Uwahabi, ilikuwa inakubaliana sana na sera zake za kuwagawa Waislamu na hatimaye kuwatala. Katika kujaribu kumbembeleza Hussein Bin Ali Sharif, London ilimteua mtoto wake wa kiume aliyeitwa Faisal wa Kwanza na kumpa uongozi wa Syria. Hata hivyo Ufaransa iliyokuwa imeikalia kwa mabavu Syria ilipinga uteuzi huo na hivyo ikaamua kumfukuza kutoka Syria. Baada ya hapo London ilimteua tena Faisal wa Kwanza kuwa mtawala wa Iraq ambayo wakati huo, ilikuwa koloni lake. Faisal wa Kwanza aliendelea kuwa kiongozi nchini humo hadi mwaka 1933 ambapo alifariki dunia. Katika kipindi chote cha utawala wake alikuwa akitumikia maslahi ya mkoloni Mwingereza.

Mfalme Faisal wa Kwanza

Katika siku kama hii ya leo miaka 93 iliyopita alizaliwa mjini Punjab, mashariki mwa Pakistan, Mohammad Abdus Salam, mwanafizikia mkubwa wa nchi hiyo. Alikuwa na juhudi kubwa kwenye masomo tangu akiwa kijana mdogo na akiwa na umri wa miaka 14 alijiunga na Chuo Kikuu cha Mjini Punjab. Baada ya kupata shahada ya uzamili katika chuo kikuu hicho, Abdus Salam alijiunga na chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza. Hatimaye akiwa katika chuo hicho, Abdus Salam alijiunga na taaluma ya fizikia ambapo mwaka 1951 alifanikiwa kupata tuzo ya Adams. Katika mwaka huo huo msomi huyo alirejea nchini kwake na kujishughulisha na kazi ya ukufunzi. Hata hivyo kukosekana kwa zana na vitendeakazi, kulimfanya arejee tena nchini Uingereza na baadaye kusafiri latika nchi nyingi za Ulaya ambapo aliongoza taasisi kadhaa za kielimu barani humo. Mohammad Abdus Salam, alifariki dunia mwaka 1996.

Mohammad Abdus Salam

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, yaani tarehe 29 Januari mwaka 1963, alifariki dunia mshairi wa Kimarekani Robert Frost. Malenga huyo alizaliwa mwaka 1874. Kipaji chake kikubwa katika sanaa ya mashairi kilimuwezesha kuandika diwani yake ya kwanza ya mashairi akiwa na umri wa miaka 20. Frost aliipa diwani hiyo ya mashairi jina la "A Boy's Will". Malenga huyo mara kadhaa alitunukiwa tuzo ya usanii ya Pulitzer.

Robert Frost

Tarehe 9 Bahman miaka 40 iliyopita watu wengi wa mji wa Tehran walielekea katika msikiti wa chuo Kikuu cha Tehran, baada ya wanaharakati wa kidini kukusanyika katika chuo hicho wakipinga hatua ya utawala wa Shah ya kumzuia Imam Khomeini (M.A) kurejea hapa nchini. Watu waliandamana katika miji mingine ya Iran kupinga hatua hiyo, na kutaka kupinduliwa utawala wa kidhulma wa Shah na kurejea Imam Khomeini (M.A) hapa nchini. Siku hiyo wanajeshi wa utawala wa Shah kwa mara nyingine waliwashambulia wananchi,  kujeruhi na kuua shahidi Waislamu wengi miongoni mwao.

Wanaharakati wa kidini wakiwa ndani ya msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran

Na siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja kati ya marajii na maurafaa wakubwa wa Kiislamu wa Iran. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika eneo la Fouman huko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.

Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani