Feb 04, 2019 08:11 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Feb 4

Hujambo mpenzi msikilizaji na haswa mpenzi na mfuatiliaji wa spoti, na karibu tuangazie baadhi ya matukio ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita....

Kombe la Asia: Qatar yatwaa ubingwa

Timu ya taifa ya soka ya Qatar imetwaa ubingwa katika michuano ya Kombe la Asia. Hii ni baada ya kuibamiza Japan mabao 3-1 katika mchuano wa kusisimua wa fainali uliopigwa Ijumaa katika Uwanja wa Mohammed bin Zayed mjini Abu Dhabi. Dakika 12 baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza ngoma, kiungo machachari wa Qatar Almoez Ali alifunga bao la aina yake, hili likiwa bao lake la tisa katika mashindano hayo ya kikanda. Mpira ulipaa juu ya kichwa chake huku akidondoka chali wakati wa kuvuta shuti hilo la mkasi. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 na mwenye asili ya Sudan sio tu anakuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi kwenye michuano hii, bali pia amevunja rekodi iliyokuwa imewekwa na Muirani Ali Daei mwaka 1996. Bao la pili la Qatar lilipachikwa wavuni na Abdul-Aziz Hatem dakika saba baadaye. Vijana wa Samurai Blue walijipapatua na kupata goli moja kunako dakika ya 69 kupitia mchezaji Takumi Minamino, na kuvuruga mchezo wa Qatar. Hata hivyo Waqatari waliimarika tena na kufunga bao la tatu na la ushindi katika dakika ya 82 kupitia mkwaju wa penati, na hivyo kuzamisha kabisa jahazi la Wajapani. Bao hilo lilifungwa na Akram Afif.

Kiungo machachari wa Qatar Almoez Ali pamoja na wenzake wakishangilia bao

 

Hii ni mara ya kwanza kwa Qatar kutwaa Kombe la Asia, jambo ambalo linaonekana kuwa mafanikio makubwa licha ya nchi yao kukabiliwa na mzingiro na vikwazo kutoka kwa Saudia na wapambe wake kwa miaka kadhaa sasa. Qatar ilitinga fainali baada ya kuibamiza wenyeji Imarati mabao 4-0, huku Wajapan wajikatia tiketi ya fainali baada ya kuisasambua Iran mabao 3-0.

Kocha wa Iran aachia ngazi

Katika hatua nyingine, mkufunzi wa timu ya taifa ya kandanda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Carlos Queiroz aliondoka Tehran kuelekea Lisbon, Ureno baada ya kuwanoa vijana wa Team Melli kwa muda wa miaka minane. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 aliachia ngazi muda mfupi baada ya Iran kukubali kichapo kutoka Japan katika mchuano wa nusu fainali ya Kombe la Asia. Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (FFIRI) limethibitisha kuwa Queiroz hakuongeza muda wa mkataba wake.

Carlos Queiroz

 

Anakuwa mkufunzi aliyeifunza timu ya Iran kwa muda mrefu zaidi. Katika kipindi alichokuwa hapa nchini, Mreno huyo ameiongoza timu ya soka ya Iran kushida michuano 60, kutoa sare 27 na kufungwa katika mechi 13. Imedokezwa kuwa Queiroz ambaye aliwahi kuionoa klabu ya soka ya Real Madrid yumkini akaelekea Colombia kuendeleza taaluma yake ya ukufunzi. Msemaji wa Wizara ya Michezo ya Iran, Maziar Nazemi, amesema miongoni mwa wakufunzi wanaotazamiwa kurithi mikoba ya Quieroz ni pamoja na Zinedine Zidane, Jose Mourinho na Jurgen Klinsmann.

Ligi ya Mabingwa Afrika; Simba yaendeleza rekodi ya kichapo

Kwa mara nyingine tena klabu ya Simba ya Tanzania ilichezea mkong'oto na kupokea kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Al Ahly ya Misri, katika mchezo wao wa ugenini wa Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League). Simba walipokea kichapo hicho Jumamosi jioni licha ya Waarabu kukosa huduma za nyota wao mmakinifu Ramadhan Sobhi ambaye anauguza jeraha. Katika kipindi cha kwanza Simba waliruhusu magoli 5 kutikisa nyavu, lakini kuongeza nidhamu ya ulinzi katikakipindi cha pili, walifanikiwa kuzuia goli lolote. Magoli ya Al Ahly yalifungwa na Sulaya dakika ya 3, Maaloul dakika ya 23, Ajayi dakika ya 31 na Walid aliyefunga magoli mawili katika dakika ya 34 na 40.

Wachezaji wa Simba ya Tanzania

 

Klabu hiyo ya Tanzania ilipokea kipigo kingine cha mabao 5-0 kutoka kwa AS Vita katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Kinshasa huko Kongo DR Jumamosi ya Januari 20. Simba sasa watacheza mechi yao ya nne nyumbani dhidi ya hao hao Al Ahly mnamo February 12 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Kwengineko, wafalme wa soka Afrika TP Mazembe ya Kongo DR iliipa kichapo cha mbwa wageni wao kutoka Tunisia, klabu ya Club Africain na kuweka rekodi mpya katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mechi hiyo ya Jumamosi, Wakongomani hao walivunja rekodi ya mabao iliyowekwa na Mimosa ya Kodivaa ilipoigaragaza CR Belouizdad ya Algeria mabao 7-0 mjini Abidjan miaka 18 iliyopita. Mazembe walifanya mauaji hayo ya kimbari Jumamosi mjini Lubumbashi, ikiwa zimepita wiki mbili tu tangu nayo iadhibiwe na CS Constantine ya Algeria. Mazembe ya DRC ilikubali kipigo cha mabao 3-0 ilipotoana jasho na CS Constantine katika mchezo wa kundi C wa ligi hiyo. Hata hivyo Constantine inaongoza kundi hilo ikiwa na alama 6, Mazembe alama 3, huku Club Africain ikiwa katika nafasi ya tatu bila alama yoyote. Klabu ya Ismaily ya Misri ilibanduliwa nje ya mashindano hayo baada ya mashabiki kuzua tafarani uwanjani.

Waydad ya Morocco inaongoza Kundi A baada ya kuizaba Enugu ya Nigeria bao 1-0, kupitia mkwaju wa penati.

Kombe la Shirikisho; Gor yavaana na Zamalek

Klabu ya Mahia ya Kenya siku ya Jumapili ilishuka dimbani kuvaana na Zamalek ya Misri katika mechi ya Kombe la Shirikisho. Katika mechi hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Kasarani jijini Nairobi, Gor ama ukipenda Kogalo waliwabamiza Waarabu mabao 4-2, huku Nyarwanda Jacques Tuyisenge akipachika wavuni magoli mawili. Magoli ya Nicholas Kipkirui na nyota wa soka Dennis Oliech yalitosha kuzamisha kabisa jahazi la Zamalek. Mabao mawili ya Waarabu hao wa Misri yalifungwa na mchezaji Ibrahim Hassan katika dakika za 25 na 43.

Mchezaji wa Kogalo akimkabili Mmisri ugani Kasarani

 

Zamalek na Gor Mahia zipo katika Kundi D ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Ushindi huo unaiweka Gor Mahia katika nafasi nzuri katika kundi hilo huku wakitafuta tiketi ya kufuzu katika robo fainali ya michuano hiyo. Klabu ya Gor Mahia ya Kenya ilitinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho licha ya kuambulia sare tasa ilipokwaruzana na New Stars de Douala mjini Limbe nchini Cameroon.

Dondoo za Hapa na Pale

Mabaki ya ndege iliyotoweka kwenye rada ya Manche mnamo Januari 21 mwaka huu ambayo ilikuwa imembeba mchezaji wa klabu ya Cardiff City raia wa Argentina, Emiliano Sala pamoja na rubani wake, yamepatikana. Karibu wiki mbili baada ya kutoweka, ndege hiyo ambayo ilikuwa ikitokea Ufaransa kuelekea Wales imepatikana kwenye bahari ya Manche. Msemaji wa shirika la Uingereza la kuchunguza ajali za ndege (AAIB) ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Ninaweza kuthibitisha kuwa ndege imepatikana." Uchunguzi mpya ulioendeshwa na kampuni ya Blue Water Recoveries (BWR) umewezesha mabaki ya ndege hiyo kupatikana mapema Jumapili asubuhi," amesema mkuu wa BWR, David Mearns.

Mashabiki wakimuomboleza mchezaji wa klabu ya Cardiff City raia wa Argentina, Emiliano Sala

 

Katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, klabu ya Machester City iliichabanga Arsenal mabao 3-1 siku ya Jumapili. City wakiupigia nyumbani Etihad, waliupa maana msema usemao kuwa mcheza kwao hutuzwa. Kiungo Sergio Aguero alipachika wavuni mabao matatu ya hatrick, la kwanza akilitia kimyani sekunde chache baada ya kuanza mchezo. Mabao mengine aliyafunga katika dakika za 44 na 61. Hii ni mara ya 10 kwa mchezaji huyo kufunga mabao ya hatrick katika ligi ya Premier. Silaha za Wabeba Bunduki zilifanikiwa kufyatua risasi moja tu, katika dakika ya 11 kupitia mwanajeshi wao Laurent Koscielny.

Kwengineko Manchester United ilipata ushindi hafifu wa bao 1 bila jibu ilipokabana koo na Leicester City siku hiyo ya Jumapili. Bao hilo la kipekee na lilowapa Mashetani Wekundu alama 3 lilifungwa na Marcus Rashford katika dakika ya 9, baada ya kupokea pasi iliyokwenda shule kutoka kwa Paul Pogba. Sasa barubaru huyo amefikisha jumla ya magoli 100 (karne) katika ligi ya EPL. Liverpool wanasalia kilele mwa jedwali la Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, wakifuatiwa na Man City, huku Tottenham wakifunga orodha ya tatu bora. Kwa sasa Man U hawana budi kuridhika na nafsi ya tano, chini ya Chelsea.

………………….TAMATI……………