Ulimwengu wa Michezo, Feb 10
Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.
Mieleka: Iran yatwaa ubingwa
Timu ya mieleka huru ya Bime Razi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Takhti yaliyofanyika katika Ukumbi wa Imam Khomeini hapa nchini na kufunga pazia lake Februari 8. Katika duru ya 39 ya mashindano hayo ya dunia yaliyofanyika katika mji wa Kermanshah, magharibi mwa nchi, Iran iliibuka kidedea kwa kuzoa jumla ya alama 240. Wimbo wa taifa wa Iran ulihinikiza katika ukumbi huo, kwa ushindi huo mnono wa wanamieleka mahiri wa Iran.
Mashindano hayo yamefanyika kama sehemu ya kuadhimisha miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979. Azerbaijan na Kyrgyzstan zimeshika nafasi ya pili na tatu mtawalia, kwa kuvuna alama 112 na 104. Mbali na nchi hizo tatu, nchi nyingine zilizoshiriki mashindano hayo ya mieleka ya Freestyle ni Uturuki, Russia, Armenia, Hungary, Uholanzi, Belarus, Kyrgyzstan na Georgia.
Futsal: Iran yailaza Serbia
Timu ya taifa ya mchezo wa futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeisasambua Serbia katika mechi mbili za kirafiki mjini Belgrade. Katika mchezo wa pili Jumanne iliyopita, Iran iliizaba mwenyeji Serbia magoli 4-3 licha ya kuchezea ugenini. Mabao ya timu hiyo ya soka inayochezewa ukumbini ya Iran yalifungwa na Hossein Tayyebi (magoli 3 ya hatrick) huku Ali Asghar Hassanzadeh akilizamisha kabisa jahazi la wenyeji kwa bao la nne. Kabla ya mchuano huo, Iran ilikuwa imeichabanga timu hiyo ya taifa ya futsal ya Serbia mabao 6-3, katika mechi nyingine ya kirafiki.
Timu hiyo ya taifa ya mchezo wa futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo iko katika nafasi ya 3 kwa mujibu wa vinwago vipya vya FIFA, inatumia michuano hii ya kirafiki kama sehemu ya maandalizi ya Mashindano ya Kufuzu ya Mabingwa wa Futsal mwaka ujao 2020, na pia Kombe la Dunia la Futsal la mwaka uohuo wa 2020. Team Melli ya Iran pia inatazamiwa kuvaana na Brazil katika mchuano mwingine wa kirafiki mnamo Aprili 8.
Kombe la Dunia U-20
Timu ya taifa ya Senegal ya vijana wasiozidi miaka 20, imekuwa ya kwanza kufuzu katika fainali ya Kombe la Dunia itakayopigwa mwezi Mei mwaka huu nchini Poland. Hii ni baada ya Young Lions of Teranga kuiumiza Ghana mabao 2-0 katika mechi ya mzunguko wa pili ya kuwania ubingwa wa Afrika, katika mashindano yanayoendelea nchini Niger. Senegal wanaongoza Kundi la B kwa alama 9, baada ya kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Mali pia na kuwalaza kwa mabao 2-0. Katika mechi ya mwisho, Senegal ilishuka dimbani kuvaana na Burkina Faso siku ya Jumamosi. Burkinabe walichezea kichapo na kuzabwa mabao 5-1 na mabarobaro hao wa Segenal.
Nigeria nayo inaendelea kuongoza kundi A kwa alama 4, baada ya kutofungana na Afrika Kusini katika mechi yake ya pili. Wenyeji Niger na Afrika Kusini zina alama mbili, huku Burundi ikiwa na alama moja baada ya kuambulia sare ya mabao 3-3 na Niger. Timu tatu tu ndizo zitakazofuzu katika michuano ya Kombe la Dunia na kuliwakilisha bara Afrika.
Mvutano kuhusu ufadhili wa soka ya Zanzibar
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Juliana Shonza amesema Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFA) haliwezi kupokea moja kwa moja fedha za misaada kutoka Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) kwa kuwa sio mwanachama wa shirikisho hilo. Shonza alitoa kauli hiyo Alkhamisi ya Februari 7 akiwa bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu maswali ya mbunge Hatib Said Haji, aliyetaka ufafanuzu kuhusu namna ZFA inavyonufaika na fedha za FIFA.
Akijibu maswali hayo, Waziri Shonza ameeleza kuwa, ZFA haiwezi kupokea fedha za misaada kutoka FIFA moja kwa moja kwa kuwa siyo mwanachama wa shirikilo hilo na sio mwanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF), bali ZFA inapokea fedha hizo kutoka kwa TFF. Mnamo mwaka 2017, Zanzibar ilivuliwa uanachama wa CAF baada ya kudumu kwenye shirikisho hilo kwa muda wa miezi minne tu. Miongoni mwa sababu za Zanzibar kupokonywa uanachama ni kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo sheria za shirika hilo haziruhusu uanachama wa mashirikisho mawili kutoka kwa taifa moja.
Dondoo za Hapa na Pale
Polisi mjini London nchini Uingereza inachunguza tukio kubwa la udhalilishaji na chuki dhidi ya Uislamu. Tukio hilo linahusu video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha shabiki mmoja akimrushia madongo na cheche za kibaguzi kwa misingi ya dini yake mshambuliaji wa klabu ya soka ya Liverpool, Mohamed Salah wakati wa mchezo dhidi ya West Ham uliochezwa Februari 4. Mshambuliaji huyo mzaliwa wa Misri mwenye umri wa miaka 26, alirekodiwa kwenye kipande cha video kwa njia ya simu upande walikokuwa wamekaa washabiki wa timu yake katika uwanja wa nyumbani wakati alipokuwa akijiandaa kuupiga mpira wa kona. Katika taarifa yake, timu hiyo ya West Ham imejiondolea lawama, na kujitenga na shabiki wake huyo mbaguzi. Imesema aliyefanya kitendo hicho cha kibaguzi atakabiliwa na marufuku maisha ya kutoingia kushuhudia michuano ya Liverpool. Vitendo vya kibaguzi na haswa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Uingereza ni mambo ya kawaida kabisa. Julai mwaka jana, ripoti ya asasi isiyokuwa ya kiserikali ilisema uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Waislamu na matukufu yao umeongezeka kwa kiwango cha kutia wasiwasi nchini Uingereza. Shirika hilo linaloitwa Tell Mama lilisema katika ripoti yake ya kila mwaka kwamba, kati ya kesi 1,201 za hujuma hizo zilizonakiliwa na kufanyiwa uhakiki mwaka juzi 2017, kumedhihirisha kuwa kiwango cha chuki hizo kimeongezeka kwa asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka juzi wa 2016. Kiwango hicho ndicho cha juu zaidi tangu shirika hilo lianze kunakili visa vya kuhujumiwa Waislamu, taasisi na maeneo yao ya ibada nchini Uingereza.
Na sasa ni rasmi kuwa aliyekuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya kandanda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Carlos Queiroz amepata kibarua kipya na sasa ataionia timu ya taifa ya soka ya Colombia. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 aliachia ngazi muda mfupi baada ya Iran kukubali kichapo kutoka Japan katika mchuano wa nusu fainali ya Kombe la Asia. Aliondoka hapa nchini akiwa mkufunzi aliyeifunza timu ya Iran kwa muda mrefu zaidi. Mreno huyo amesaini mkataba wa miaka minne na Colombia huku kibarua kigumu kinachomkodolea macho kwa sasa ikiwa ni kuiandaa timu hiyo kwa michuano ya Copa America itakayofanyika nchini Brazil kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu. Hii ni timu ya tano ya taifa kunolewa na Queiroz. Amewahi kuzifunza soka Afrika Kusini, Korea Kusini na Japan, mbali na kuwanoa pia vijana wa klabu ya Real Madrid.
…………………..TAMATI..…………….