Ulimwengu wa Michezo, Feb 18
Hujambo mpenzi msikilizaji wa na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa...
AFC: Zob Ahan yatinga hatua ya muondoano
Klabu ya Zob Ahan ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetinga hatua ya muondoano katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia ya AFC, mwaka huu 2019. Hii ni baada ya kuichachafya klabu ya al-Kuwait bao moja bila jibu katika mchuano wa mkondo wa pili uliopigwa katika uwanja wa Foolad Shahr mjini Isfahan, katikati mwa nchi Jumanne ya wiki iliyopita. Nusra mchuano huo uishie kwa sare tasa, lakini bao la dakika za nyongeza la Christian Osaguona Ighodaro lilitosha kuipa klabu hiyo ya Iran pointi 3 muhimu.
Zob Ahan ambayo ilimaliza ya pili katika mashindano ya mwaka 2010 ya AFC Champions League, sasa inatazamiwa kutoana udhia na al-Gharafa katika mchuano wa muondoano, na timu itakayopeta katika mechi hii itatinga hatua ya makundi. Klabu nyingine ya Iran ya Saipa pia imetinga hatua ya muondoano, baada ya kuipa kichapo cha mbwa klabu ya India ya Minerva Punjab, kwa kuichabanga mabao 4-0.
Sasa klabu hii ya watengeneza magari ya Iran inatazamiwa kupepetana na klabu ya al-Rayyan ya Qatar katika mechi ya muondoano.
Karate: Iran yazoa medali kochokocho
Makarateka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali saba katika mashindano ya Ligi Kuu ya Katare 1 yaliyofanyika mjini Dubai, huko Imarati. Wanakarate wa Iran waling'ara katika mashindano hayo ya kikanda yaliyofanyika katika Ukumbi wa Michezo wa al-Wasl mjini Dubai, na kujinyakulia medali saba za shaba. Katika pambano la wanawake kategoria ya wanakarate wenye kilo chini ya 55 mtindo wa Kumite, binti wa Kiirani Fatemeh Chalaki alimuonesha kivumbi Mmisri Salma Elshafi na kutwaa shaba.
Mwanadada mwingine wa Iran Rozita Alipour alimzindia ujuzi Merve Cuban wa Uturuki na kumshinda kwa alama 3-0 na kuipa Iran shaba nyingine. Katika safu ya wanaume, Amir Reza wa Iran alimpeleka mchakamchaka raia wa Austria katika pambano la makarateka wenye kilo sisizozidi 67 na kuibuka kidedea, huku Hamoon Derafshipour, Zabihollah Poorshab na Sajjad Ganjzadeh wakiibuka washindai pia katika mapambano yao ya makarateka wenye kilo zisizozidi 67, zisizozidi 84 na zaidi ya 84 kwa usanjari huo.
Wanawake Waislamu kuvaa hijabu katika ndondi
Shirikisho la Ndondi Duniani AIBA limepasisha uamuzi wa kuwapa idhini wanamasumbwi wa kike wa dini ya Kiislamu kuvaa hijabu wakiwa katika mapambano ya kimataifa. Baada ya kufanya mkutano mjini Istanbul nchini Uturuki, Kamati Kuu ya shirikisho hilo imesema, "Wanawake sasa wataruhusiwa kuvaa hijabu iwapo watafanya hivyo kwa msingi wa mafundisho wa dini yao."
Vazi hilo la stara linalovaliwa na wanawake Waislamu sasa limejumuishwa katika orodha ya sare za wanamasumbwi zinazotambulika kimataifa. Uamuzi huo wa Shirikisho la Ndondi Duniani kuruhu uvaaji wa hijabu katika mapamabno ya kimataifa umepokewa na mikono miwili na wadau katika uga wa michezo, haswa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya wanamasumbwi bingwa wanawake wa Kiislamu ima walistaafu ndondi mapema kwa kukatazwa kuvaa hijabu au kunyimwa fursa ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa wao wao kushikilia kuwa lazima wapambane huku wakiwa wamevalia vazi hilo la heshima.
Aghalabu ya mashirikisho ya michezo duniani yameruhusu vazi hilo la staha kuvaliwa uwanjani katika michezo mbalimbali kama vile taekwondo, karate, mpira wa kikapu na voliboli miongoni mwa michezo mingine. Hata hivyo uamuzi wa AIBA kuruhusu uvaaji wa vazi la stara la hijabu kwa wanandondi wanawake wa Kiislamu umeitia kiwewe Jumuiya ya Kimataifa ya Haki za Wanawake (ILWR), yenye makao makuu yake nchini Ufaransa. Vuguvugu hilo la kifeministi hivi karibuni lilitoa mwito wa kupigwa marufuku hijabu na mavazi mengine yanayoonekana kuwa ya Kiislamu katika michezo ya Olimpiki na Paralimpiki ya mwaka 2024 mjini Paris.
Watani wa jadi Tanzania wavaana tena, wasababisha vicheko na vilio
Watani wa jadi wa soka nchini Tanzania, walishuka dimbani Jumamosi kuvaana tena katika mchuano wa kusisimua wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara. Katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam, klabu Simba ilifanikiwa kuvuna alama tatu na ushindi hafifu wa goli moja kwa nunge, lililofugwa na Meddie Kagere. Kagere alitikisa nyavu kwa goli lake hilo la kichwa kunako dakika ya 71, na kuipa Simba ushindi kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuwalaza Al Ahly ya Misri siku chache zilizopita.
Ushindi huo sasa umeifanya Simba kufikisha alama 39 wakiwa wamecheza michezo 16, huku Yanga wakiwa na point 58 wakiwa wamecheza michezo 24. Kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amesema kuwa klabu yake ilistahili kushinda mchezo huo wa watani wa jadi. Amesema, licha ya kucheza mechi ngumu hivi karibuni, wachezaji wake walijitahidi kucheza vizuri na kuwapongeza kwa kile walichokifanya. Naye mkufunzi mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alieleza kuwa sababu za kikosi chake kupoteza mechi hiyo ni kutokana na kushindwa kuwa wabunifu.
Ushindi huo japo hafifu lakini umetuma vilio na vicheko miongoni mwa mashabiki wa watani hao wa jadi Tanzania.
Dondoo za Hapa na Pale
Klabu ya PSG ya Ufaransa ilivuna ushindi mnono wa mabao 2-0 iliposhuka dimbani kuvaana na Manchester United katika mkondo wa nne wa mechi za Ligi ya Klabu Bingwa Barani Ulaya Jumanne ya Februari 12. Paris Saint-Germain licha ya kuwakosa wachezaji wake nyota kama Neymar Jnr na Edinson Cavani ambao wanauguza majeraha, walipata ushindi muhimu dhidi ya wenyeji wao Manchester United. Mabao ya mabingwa wa Ufaransa yaliwekwa kimyani na Presnel Kimpembe na Kylian Mbappe.
Manchester United wanahitaji miujiza watakapokutana tena na miamba hao wa Ufaransa mjini Paris mnamo Machi 6 ili watinge robo fainali.
Wakati huohuo, mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya Real Madrid, wakiwa ugenini nchini Uholanzi katika uwanja wa Johan Cruijff Arena, waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao Ajax. Mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema, alipachika bao la kuongoza katika dakika ya 60 kabla ya Ajax kusawazisha kupitia Hakim Ziyech katika dakika ya 75. Marco Asensio aliifungia Real Madrid bao la ushindi zikiwa zimesalia dakika nne kabla ya mechi hiyo kukamilika.
Kwengeniko kocha Mauricio Pochettino amewapongeza vijana wake wa Tottenham hususan mchezaji Son Heung-min baada ya kuitandika Borussia Dortmund mabao matatu kwa mtungi kwenye mechi yao ya hatua ya kumi na sita bora awamu ya kwanza iliyopigwa uwanjani Wembley. Lyon watatoana jasho na Barcelona tarehe 19, huku Atletico Madrid wakicheza na Juventus kesho yake, wakati ambapo Schalke 04 watakuwa wenyeji wa Manchester City.
Na inaarifiwa kuwa klabu ya Chelsea ipo mbioni kutafuta saini ya aliyekuwa kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane ili kuchukua mikoba ya Maurizio Sarri. Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 46, Zidane amekuwa nje ya kazi yake kwa muda kidogo tangu kuachana na Real baada ya kuipatia mataji matatu mfululizo ya Champions League.
……………….TAMATI.…………..