Mar 11, 2019 03:54 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Machi 11

Hujambo mpenzi msikilizaji na haswa mfuatiliaji wa masuala ya spoti na karibu katika dakika hizi chache za kutupia jicho baadhi ya matukio muhimu yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.

Futsal ya Wanawake: Iran yaibamiza Russia

Timu ya taifa ya futsal ya wanawake ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Ijumaa ilishuka dimbani kuvaana na Russia katika mchuano wa kirafiki ambapo wanadada hao wa Kiirani waliibuka washindi. Katika mchezo huo, Iran ilifanikiwa kuisasambua Russia mabao 3-2 katika kitimutimu hicho kilichogaragazwa hapa mjini Tehran. Mabao ya wanadada hao wa Iran yalifungwa na Fatemeh Papi, Fatemeh Arjangi na Fereshteh Karimi. Hata hivyo katika mchezo wa marudiano siku ya Jumamosi, Russia ilijipapatua na kupata ushindi dhidi ya Iran. Baada ya mchuano huo wa Jumamosi, mkufunzi wa Iran, Zivar Babaei alisema, "Tulicheza vizuri ila tuliruhusu mabao mawili ndani ya dakika moja kutokana na makosa madogo. Hata hivyo nimeridhika na mchezo wetu dhidi ya moja ya timu nguvu za Ulaya." Timu ya taifa ya futsal ya wanawake ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatumia michuano hii ya kirafiki kwa ajili ya kujitutumua misulu, ikijiandaa kwa mashindano ya Mabingwa wa Futsal Asia mwaka 2020.

Iran yatwaa taji la Karate

Wanakarate wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametwaa taji la mashindano ya kimataifa ya mabingwa wa karate mkoani Kerman, kusini mashariki mwa Iran. Katika kategoria ya vijana wa kiume, Iran iliibuka kidedea huku Iraq na Azerbaijan zikichukua nafasi ya pili na tatu mtawalia. Katika safu ya akina dada,

Makarateka wa Iran

Timu A ya Iran pia imeibuka mshindi, ikifuatiwa na Timu C na Timu B zote zikiwa za hapa nchini, huku nafasi ya nne ikitwaliwa na Afghanistan.

Simba yaangukia pua tena

Bingwa mtetezi wa Ligi kuu Tanzania bara, Simba SC,  imeendeleza rekodi ya kupoteza mechi za ugenini kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya usiku huu kuchapwa mabao 2-0 na wenyeji, JS Saoura Uwanja wa Agosti 20, 1955 mjini Bechar katika Kundi D. Katika mchezo huo Simba ilianza kufungwa katika kipindi cha kwaza dakika ya 18 goli lililofungwa na mshambuliaji Sid Ali Yahia Cherif kwa shuti kali akimalizia mpira uliorudi baada ya kuokolewa na Paul Bukaba kufuatia yeye mwenyewe kuunganisha kwa kichwa krosi ya Mohamed El Amine Tiboutine kutoka upande wa kulia.

Wachezaji wa Simba

Akafuatia Mohamed El Amine Hammia kufunga bao la pili kwa penalti dakika ya 51 baada ya Sid Ali Yahia Cherif kuangushwa na beki wa Simba SC, Paul Bukaba Bundala kwenye boksi. Kwa matokeo hayo, Saoura inapanda kileleni mwa Kundi D ikifikisha alam nane baada ya kucheza mechi tano, ikifuatiwa na Al Ahly, AS Vita zenye pointi saba kila moja, huku Simba SC ikishika mkia katika Kundi D kwa pointi zake sita, huku ikiwa ndio timu iliyofungwa mechi nyingi hadi sasa katika kundi lao. Mechi za mwisho Machi 16, Al Ahly na JS Saoura nchini Misri na Simba SC na AS Vita mjini Dar es Salaam zitaamua timu za kwendsa Robo Fainali kutoka Kundi D. Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo, Afisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram akisema kuwa kwao mapambano bado yanaendelea na wanayo nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa ya vilabu barani Afrika. Kabla ya mchezo wa Simba, ulitanguliwa na mchezo wa AS Vita Club walioikaribisha Al Ahly mjini Kinshasa, ambapo mchezo huo ulimalizika kwa AS Vita kuibuka na ushindi wa bao 1-0, bao lililofungwa na Tuisila Kisinda katika dakika ya 84'. Baada ya matokeo ya michezo hiyo, sasa kundi D linaongozwa na JS Saoura yenye pointi 8 ikifuatiwa na Al Ahly na AS Vita Club zenye pointi 7 huku Simba ikiwa mkiani kwa pointi 6. Mpaka sasa timu yoyote katika kundi hilo inaweza kufuzu hatua inayofuata ya robo fainali endapo itashinda katika mchezo wa mwisho. 

Dondoo za Hapa na Pale

Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys ya Tanzania ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 17 imeisasambua Australia mabao 3-2 katika mchezo wa Pili wa mashindano ya UEFA ASSIST yanayofanyika Uturuki. Magoli ya Serengeti Boys yalifungwa na Kevin John aliyefunga mawili katika dakika ya 16 na 84, huku Edson Mshirakandi akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Autsralia. Mabao ya Australia yalifungwa na Michael Ruhs na Noah Boatics.Katika mchezo wa kwanza wa mashindano ya UEFA ASSIST yanayofanyika Uturuki, Serengeti ilichezea kichapo cha bao 1 bila jibu kutoka kwa Guinea.

Katika Ligi Kuu ya Soka Uingereza, mahasimu wa jadi, Manchester United walishuka dimbani Jumapili kuvaana na Arsenali. Gunners wakiupigia nyumbani katika dimba la Eirates, waliupa maana msemo usemao, mcheza kwao hutuzwa. Wabeba Bunduki hao wa Uingereza walifanikiwa kuwatandika Mashetani Wekundu risasi mbili, bila jibu. Mabao ya Arsenali yalitiwa wavuni na Granit Xhaka dakika ya 12 na Pierre Emerick Aubameyang dakika ya 67 kupitia mkwaju wa penati.

Gunners wakishangilia bao

Kipigo hicho kinakuwa cha kwanza kwa Man U katika EPL toka wawe chini ya kocha wao Ole Gunnar Solskjaer ambaye amewaongoza katika michezo 13 hadi sasa wakitoka sare michezo miwili. Arsenal pia inakuwa timu ya kwanza msimu huu kucheza na Man United nyumbani na kufanikiwa kumaliza mechi bila kuruhusu goli katika mchezo.

Mbali na hayo, usiku wa kuamkia Jumatano klabu ya Ajax walitamba kwa kucheza soka la kiwango cha juu na kufanikiwa kuwabandua mabingwa wa ulaya mara 13, Real Madrid katika uwanja wa Santiago Bernabeu na kufuzu kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22. Katika mechi ya awamu ya kwanza Ajax ilizabwa mabao mawili kwa moja lakini katika mchezo wa usiku wa kuamkia Jumatano ndani ya dakika 18 walipata mabao ya mapema kupitia mshambuliaji Hakim Ziyech na David Neres. Kiungo wa Ajax Dusan Tadic alikua moto wa kuotea mbali huku akitengeneza mabao mawili, na kufunga goli la tatu. Real Madrid iliyokuwa inasaka taji la nne mfululizo la michuano hiyo, ilizinduka kwa goli la Marco Asensio katika dakika 20 za mwisho. Lakini kiungo wa Ajax Lasse Schone kupitia mpira wa adhabu dakika mbili baadae aliwanyamazisha vijana wa Santiago Solari ambao walihitaji kufunga magoli matatu zaidi ili kusonga mbele. Kwa ushindi huo Ajax inakuwa timu ya kwanza kufungwa nyumbani katika mchezo wa kwanza na kufanikiwa kupindua matokeo kwenye michuano ya Ulaya. Real Madrid inakuwa bingwa mtetezi wa kwanza kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali ya klabu bingwa ya ulaya tangu Chelsea ifanye hivyo msimu wa 2012-13.

Kwenye mechi nyengine iliyopigwa usiku huo, Tottenham hotspurs waliokuwa ugenini waliwatandika wenyeji wao Borussia Dortmund bao moja bila na kutinga robo fainali ya ligi hiyo bingwa barani ulaya. Usiku wa Machi 6 jijni Paris Ufaransa ulichezwa mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora ya UEFA Champions League kati ya Man United dhidi ya Paris Saint Germain ambao ndio wenyeji wa mechi hiyo, PSG waliingia kucheza game hiyo wakiwa mbele kwa magoli 2-0 waliyoyapata katika mchezo wa kwanza. Mechi ya marudiano mchezo ulibadilika na kujikuta PSG wakipoteza mchezo huo nyumbani kwa kufungwa kwa magoli 3-1 ila wamejikutaka wakiaga michuano hiyo kutokana na wao wameruhusu kufungwa kwa magoli mengi nyumbani kwao.

Katika mechi za awali za Ligi ya Uropa hatua ya 16 bora, Chelsea wakiwa nyumbani wameikaribisha Dynamo Kyiv kwa kuipiga mabao 3-0, mahasimu wa Chelsea washika bunduki Arsenal walikuwa ugenini kwa Rennes na kukubali kichapo cha magoli 3-1, Valencia wao wametoka kifua mbele kwa kuifunga FC Krasnodor bao 2-1, wakati Sevilla zimetoshana nguvu ya bao 2-2 na Slavia Prague, Villareal wameibamiza Zenit St. Petersburg kwa jumla ya bao 3-1, Inter Milan imetoka sare ya bila kufungana na Eintracht Frankfurt, Napoli imefanikiwa kushinda 3-0 dhid ya Salzburg na Dinamo Zagreb imetoaka na ushindi kiduchu wa goli 1-0 dhidi ya Benfica.

Samuel Eto’o

Na nyota wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Cameroon Samuel Eto’o anatazamiwa kupelekwa mahakamani na Bi Adileusi do Rosario Neves kwa madai kuwa amemtelekeza mtoto wake. Neves anasema wakati Eto’o akiwa anachezea Leganes alizaa nae mtoto ambaye kwa sasa ana miaka 19. Lakini Eto’o hakuwahi kumtambua mtoto huyo anayejulikana kama Erika. Wakili wa mama huyo amesema tayari kesi imeshafunguliwa jijini Madrid na itasikilizwa tarehe 24 mwezi ujao wa April.

…………………TAMATI….………….