Jumanne, tarehe 12 Machi, 2019
Leo ni Jumanne tarehe 5 Rajab 1440 Hijria sawa na tarehe 12 Machi 2019.
Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Machi 1930 ilianza harakati kubwa ya uasi iliyoongozwa na Mahatma Gandhi, kiongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa India. Harakati hiyo kubwa ambayo iliwashirikisha wazalendo na wapigania uhuru wa India, ilifanyika kwa shabaha ya kukabiliana na maamuzi mapya ya serikali ya kikoloni ya Uingereza kuhusu ongezeko la ushuru wa chumvi. Katika kukabiliana na sheria hiyo ya kidhalimu, Mahatma Gandhi na wenzake elfu 78 walianza kutayarisha chumvi kutoka maji ya baharini. Wakoloni wa Uingereza walikabiliana na harakati hiyo kwa kuwatia nguvuni makumi ya maelfu ya Wahindi na kuwatia korokoroni. Hali hiyo ilisababisha ghasia na vurugu katika idara za serikali. Mapambano hayo ya Mahatma Gandhi yaliilazimisha serikali ya kikoloni ya Uingereza kusalimu amri na kulegeza misimamo yake.
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita sawa na tarehe 12 Machi 1968 nchi ndogo ya Mauritius iliyoko kusini mwa Afrika ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Waholanzi waliingia Mauritius katika karne ya 17 na wakafuatiwa na Wafaransa karne moja baadaye. Mwaka 1814 Waingereza walikivamia kisiwa cha Mauritius na kukiunganisha na makoloni yao. Kisiwa hicho kina ukubwa wa kilomita mraba elfu mbili hivi na jamii ya zaidi ya watu milioni moja.
Miaka 94 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Sun Yat-sen mwanamapinduzi na Rais wa Kwanza wa China. Sun Yat-sen anayejulikana kama baba wa taifa la China alizaliwa mwaka 1866 huko Nanlang China. Mwaka 1892 alijiunga na Chuo Kikuu na akiwa na umri wa miaka 26 alifanikiwa kupata shahada ya udaktari. Uwanja na mazingira ya Sun Yat-sen ya kuanzisha harakati zake za kisiasa yaliandaliwa baada ya Japan kuishambulia China mnamo mwaka 1894. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanzisha harakati zake dhidi ya mfumo wa kifalme wa Manchu. Baada ya harakati hiyo kushindwa alikimbilia nje ya nchi. Mwaka 1905 alirejea China na kuanzisha Muungano wa Wanamapinduzi wa China lengo likiwa ni kuleta demokrasia katika nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1911 utawala wa familia ya kifalme ya Manchu ulifikia tamati baada ya kupinduliwa. Tukio hilo lilipelekea kutangazwa mfumo wa Jamhuri nchini China na Sun Yat-sen alifanikiwa kushika hatamu za uongozi akiwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya China.
Tarehe 5 Rajab miaka 1196 iliyopita aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea mjini Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Abbasia kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW); jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na alichukua hatua ya kumuua. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni kile kiitwacho "Islahul Mantik."
