Mar 17, 2019 07:39 UTC
  • Jumapili, tarehe 17 Machi, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 10 Rajab 1440 Hijiri, sawa na tarehe 17 Machi 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, kufuatia kushindwa Roma na Waislamu, hatimaye ardhi takatifu ya Baytul-Muqaddas ilikombolewa na Waislamu. Baada ya kudhihiri Uislamu sambamba na kupanuka kwa tawala za Kiislamu, kulijiri vita vya kwanza kati ya Waislamu na Waroma, huko kaskazini mwa Bahari Nyekundu. Katika utawala wa Omar bin al-Khatwab, jeshi la Waislamu liliwashinda Waroma na kuyatawala maeneo ya kusini mwa Palestina. Baada ya kushindwa huko, mfalme wa Roma alituma jeshi kubwa katika ardhi za Palestina. Hata hivyo vita vikali vilivyojiri huko Palestina, kwa mara nyingine tena vilipelekea Waroma kushindwa na Waislamu na kuuawa kiongozi mkuu wa jeshi la Roma mwishoni mwa vita hivyo, huku mji wa Damascus ukitwaliwa na Waislamu. Baada ya hapo Waislamu waliishi huko Palestina na Sham. Mwaka 1097 Miladia, Wakristo walianzisha Vita vya Msalaba kwa lengo la kutaka kuiteka Baytul-Muqaddas na baada ya mapigano kadhaa kati ya pande mbili, hatimaye mwaka 1250 Miladia, mji huo uliingia katika himaya ya Waislamu chini ya uongozi wa Salahuddin Ayyubi.

Ardhi takatifu ya Baytul-Muqaddas

Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita alizaliwa Abdullah Bin Hussein maarufu kwa jina la Ali Asghar, mtoto wa Imam Hussein Bin Ali Bin Abi Twalib (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Ali Asghar alizaliwa kipindi ambacho Yazid Bin Muawiya ndio kwanza alikuwa ameshika uongozi ambapo pia alikuwa ameanzisha mashinikizo na vitisho dhidi ya baba yake Imam Hussein (as) akimtaka atoe baia kwake. Kwa kuzingatia kuwa mjukuu huyo wa Mtume alimtambua vyema Yazid kuwa mtu muovu na asiyefaa, alikataa kutoa baia kwa mtawala huyo. Ni kwa msingi huo ndio maana siku 18 baada ya kuzaliwa mwanaye huyo (Ali Asghar) akaondoka mjini Madina akiwa pamoja na watu wa familia yake. Nafasi muhimu ya mtoto huyo ilikuwa katika jangwa la Karbala, Iraq wakati wa kujiri vita kati ya jeshi la Yazid na Imam Hussein (as). Wakati wafuasi wote wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) walipokuwa wameuawa shahidi, Imam Hussein alimchukua mtoto wake huyo aliyekuwa na umri wa miezi sita kipindi hicho na kutoka naye nje ya hema kwa lengo la kumuombea maji kutokana na kiu kali iliyokuwa inamkabili. Kinyume na ilivyotarajiwa kiutu, maadui wa Uislamu waliokuwa wamewazuilia maji watu hao wa familia ya Mtume hawakuwa tayari kumpatia maji mtoto huyo mchanga na badala yake Harmalah Bin Kahil al-Asadi, kutoka katika jeshi la Yazid na bila ya huruma alimlenga mtoto huyo kwa mshale wenye ncha tatu ulioikatakata shingo yake na kumuua shahidi Ali Asghar papo hapo.

Siku kama ya leo miaka 1245 iliyopita sawa na 10 Rajab 195 Hijria, alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina, Imam Muhammad Taqi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume (saw). Imam Taqi (as) alichukua jukumu la kuuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha (as). Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya 'Jawad' yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu mkubwa aliokuwanao. Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa masaba wa siku hii, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi al Jawad (as) ambaye amesema: "Kumtegemea Mwenyezi Mungu ni ngazi ya kuelekea kwenye ukamilifu. Mwenyezi Mungu humuokoa mtu huyo na kila baya na kumlinda na kila uadui."

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, wawakilishi wa nchi za Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg, walitia saini mkataba wa ushirikiano wa pamoja mjini Brussels, Ubelgiji. Katika mkataba huo uliofahamika kwa jina la "Mkataba wa Brussels", nchi hizo zilikubaliana kuanzisha mfumo wa ulinzi wa pamoja na kupanua uhusiano wao wa kiuchumi na kiutamaduni. Aidha mkataba huo ndio uliokuwa chachu ya kuanzishwa kwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO. Kwani ni baada ya hapo ndipo yalifanyika mazungumzo kati ya Marekani, Canada na baadhi ya nchi wanachama wa Mkataba wa Brussels huko mjini Washington, Marekani ambapo baadaye kuliundwa Shirika hilo la NATO mwezi Aprili 1949.

NATO

Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita inayosadifiana na tarehe 26 mwezi Esfand mwaka 1373 Hijria Shamsia aliaga dunia Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ahmad Khomeini, mwana wa Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sayyid Ahmad Khomeini alizaliwa mwaka 1324 Hijria Shamsiya katika mji mtukufu wa Qum nchini Iran na kuanza kujifunza elimu ya kidini kwa baba yake. Sayyid Ahmad Khomeini alikuwa na nafasi muhimu katika kuwaunganisha wanamapinduzi na Imam Khomeini wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Sayyid Ahmad Khomeini