Ulimwengu wa Michezo, Machi 25
Hujambo mpenzi msikilizaji na haswa mfuatiliaji wa masuala ya spoti na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.
Tiketi za AFC U-23, Iran yazinyuka Yemen, Turkmenistan
Timu ya taifa ya soka ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanza vyema kampeni ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Mabingwa wa Asia mwakani, baada ya kuibamiza Yemen mabao 3 bila jibu. Katika mchezo huo wa Kundi C uliopigwa Ijumaa katika Uwanja wa Taifa wa Azadi hapa mjini Tehran, vijana wa Iran walimakinika na kucheza soka lililokwenda shule. Bao la kwanza la timu hiyo inayofahamika kama Omid Iran lilifungwa na Reza Shekari, huku somo yake Reza Jabire akifunga la pili kunako dakika ya 65. Bao la Muhammad Mehdi Khani lililiyumbisha na kulipigisha mawimbi jahazi la wageni.
Licha ya ushindi huo, lakini timu hiyo ya Iran ilipoteza fursa nyingi ya kuongeza mabao katika mchuano huo dhidi ya Yemen. Kabla ya hapo, timu hiyo ya Iran ilikuwa imeichabanga Turkmenistan mabao 3-1 katika mchuano wake wa ufunguzi. Kitumbua cha wageni kiliingia mchanga baada ya beki wao kujifunga mwenyewe kunako dakika ya 35 na kuanza hapo mambo yalizidi kuwaendea segemnege. Bao la pili la Iran lilifungwa na Omid Noor-Afkan, huku Reza Jabireh akiupiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la timu hiyo ya Asia ya Kati. Siku ya Jumanne, timu hiyo ya Iran ambyo kwa sasa ipo katika nafasi ya pili kwenye Kundi C itakuwa na kibarua kigumu itakapovaana na Iraq. Mashindano ya Olimpiki ya AFC U-23 Championships yanatazamiwa kufanyika kati ya Julai na Agosti mwaka ujao 2020 mjini Tokyo nchini Japan.
Mieleka; Iran yatwaa ubingwa
Timu ya taifa ya mieleka ya Iran ya Kiislamu imetwaa ubingwa wa Mieleka ya Greco-Roman katika mashindano ya mabingwa wa bara Asia wenye chini ya umri wa miaka 23 huko Mongolia. Hii ni baada ya kuzoa medali kochokocho, zikiwemo 4 za dhahabu. Wanamieleka hao wa Kiirani waliozoa jumla ya alama 202, wametia kibindoni pia fedha 3 na shaba 2 katika mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama Greco-Roman U23 Senior Asian Championships.
Kyrgyzstan, Kazakhstan, India na Mongolia zimetwaa nafasi ya pilisi hadi 5 kwa usanjari huo kwenye mashindano hayo ya kikanda. Mashindano hayo yaliyopigwa katika mji wa Ulaanbaatar yalianza Machi 21 na kufunga pazia lake Jumapili ya Machi 24.
Afrika Mashariki yatinga Afcon kimtindo
Kwa mara ya kwanza katika historia, Afrika Mashariki itawakilishwa na mataifa matano katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Afcon mwaka huu 2019. Timu hizo ni Uganda, Kenya, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Tuanze na Tanzania ambayo imeingia kwenye madaftari ya historia baada ya kufuzu katika fainali za Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 38, kwa kuichabanga Uganda mabao 3-0 katika mechi ya mwisho ya kufuzu ya Kundi L, iliyochezwa Jumapili jioni katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam. Mabao ya Tanzania yalifungwa na wachezaji Simon Msuva katika dakika ya 21 ya mechi hiyo, huku beki Erasto Nyoni akifunga bao la pili kupitia mkwaju wa penalti. Agrey Moris naye alihakikisha Tanzania inapata ushindi wa kuridhisha, baada ya kuifungia Taifa Stars bao la tatu katika dakika 57, kupitia shambulizi la kichwa lililomwacha taabani kipa wa Uganda Dennis Onyango. Nderemo, vifijo na hoi zilihinikiza katika Uwanja wa Taifa, lakini pia ushindi huo wa aina yake ulisababisha msisimko miongoni mwa mashabiki waliokuwa wakiufuatilia nyumbani, akiwemo Rais John Magufuli. Waziri wa Michezo Harisson Mwakyembe na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa wageni waheshima walioshuhudia mchuano huo mubashara katika Uwanja wa Taifa. Mara ya mwisho kwa Tanzania kufuzu katika fainali za Afcon ilikuwa ni mwaka 1980 nchini Nigeria, na mara hii imefuzu kwenda nchini Misri, chini ya kocha Emmanuel Amunike raia wa Nigeria. Licha ya kufungwa, lakini Uganda imefuzu katika fainali hiyo ikiwa inaongoza kundi hilo kwa alama 13, huku Tanzania ikiwa ya pili kwa alama nane. Kutofungana kwa Cape Verde na Lesotho, jijini Praia pia kumeisaidia Tanzania kufuzu Afcon.
Huku hayo yakijiri, timu ya taifa ya soka ya Burundi kwa mara ya kwanza katika historia imefanikiwa kuweka rekodi mpya katika soka lake baada ya kufuzu michuano hiyo ya mataifa ya Afrika mwaka huu 2019 itakayofanyika nchini Misri mwezi Juni mwaka huu. Burundi imefuzu kucheza michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya mchezo wao kumalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1 ilipokabana koo na Gabon.
Kadhalika timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars imejiunga na timu hizo za Afrika Mashariki, licha ya kushindwa kufurukuta mbele ya Ghana katika mchuano wa Jumamosi. Licha ya kukipigia nyumbani katika Uwanja wa Taifa wa Kasarani jijini Nairobi, Stars walishindwa kung'ara na wakakubali kichapo cha bao 1-0. Mabingwa mara nne Ghana wanalenga kumaliza ukame wa zaidi ya miaka 30 bila taji la Afrika. Nayo Kenya ambayo ilishiriki AFCON mara ya mwisho mwaka 2004, inatazamiwa kuonyesha ufundi wake itakapokutana na miamba ya soka barani Afrika. Bao hilo la ushindi na kipekee la Ghana katika mchuano wa mwisho wa Kundi F lilifungwa na Caleb Ekuban katika dakika ya 83.
Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa hata hivyo amesema Black Stars ya Ghana haina ubavu wa kushinda Kombe la AFCON katika michuano itakalofanyika nchini Misri mwezi Juni 21 hadi Julai 19 mwaka 2019. Anasisitiza kuwa, “Hatutishwi na Black Stars. Mlikuwa timu kubwa sana miaka iliyoenda, lakini si wakati huu."
Wakati huohuo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imefuzu katika fainali ya mchezo wa soka kuwania ubingwa wa mataifa ya Afrika baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Liberia katika uwanja wa Tata Raphael, jijini Kinshasa. Mechi hiyo ilikuwa ni muhimu sana kwa Leopard kupata ushindi lakini bao la Cedric Bakamu lilitosha kuwafikisha vijana wa Florient Ibenge katika fainali yao ya 19.
Zimbabwe nayo imefuzu baada ya kuilaza Congo Brazaville mabao 2-0 katika uwanja wa taifa jijini Harare. Brave Warriors walipata ushindi huo kupitia wachezaji wake Khama Billiat katika dakika ya 20 huku Knowledge Musona akiongeza la pili katika dakika ya 36. Zimbabwe imewahi kufuzu mara tatu katika historia ya Afcon, mwaka 2004, 2006, 2017 na sasa 2019. Mataifa mengine 19 ambayo tayari yamefuzu ni Angola, Madagascar, Tunisia, Misri, Senegal, Nigeria, Mali, Morocco, Algeria, Ivory Coast, Mauritania, Guinea, Ghana, Guinea Bissau, Namibia na Cameroon.
Ndondi: Mwakinyo na Zarika wang'ara
Siku ya Jumamosi mapambano mawili makubwa ya masumbwi yalishuhudiwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi. Tanzania ikiwakilishwa na bondia mtanzania Hassan Mwakinyo, huku mwenyeji Kenya ikiwakilishwa na Fatuma Zarika ambaye alihifadhi taji lake la WBC Super Bantam baada ya kumlemea Catherine Phiri wa Zambia. Zarika 'Iron Fist' mwenye umri wa miak 34 aliibuka mshindi baada ya waamuzi Michael Neequaye (Ghana), Fillemon Meya (Namibia) na Irene Semakula (Uganda) kumpa alama 98-92, 99-91 na 97-93 kwa utaratibu huo.
Hilo lilikuwa pigano la 45 la Zarika ambaye ameshinda mapigano 31 huku Phiri wa Zambia akijivunia ushindi mara 16. Baadhi ya wadadisi wa spoti barani Afrika wanahisi kuwa Zarika alipendelewa na mahakimu kwenye pambano hilo la Jumamosi lililopigwa katika Jumba la Mikutano la KICC jijini Nairobi. Hassan Mwakinyo kwa upande wake alipambana na bondia wa Argentina Sergio Gonzalez ambapo Mtanzania huyo anayetokea Tanga aliibuka kidedea kwa kumpiga hasimu wake Knock Out (K.O) kwenye raundi ya 5 ya mchezo.
……………………TAMATI.……………..