Ulimwengu wa Michezo, Machi 31
Hujambo mpenzi msikilizaji wa na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa…..karibu.....
Iran yatinga Kombe la Mabingwa wa Asia 2020
Timu ya taifa ya soka ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Mabingwa wa Asia mwakani, licha ya kutoa sare tasa na Iraq katika mchuano wa Jumanne iliyopita. Ingawaje Iran ilionesha mchezo mzuri ikiupigia nyumbani katika Uwanja wa Kitaifa wa Azadi hapa jijini Tehran, lakini kuliona lango la wageni. Hata hivyo mechi hiyo ilishuhuhudia mashambulizi ya hapa na pale. Kabla ya mchezo huo wa Jumanne, Iran ilikuwa imeibamiza Yemen mabao 3 bila jibu, katika mchezo wa Kundi C uliopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Azadi hapa mjini Tehran.
Kadhalika timu hiyo ya Iran ilikuwa imeichabanga Turkmenistan mabao 3-1 katika mchuano wake wa ufunguzi wa mechi za kusaka tiketi ya kushiriki mashindano ya kikanda ya mwaka ujao 2020 nchini Thailand. Mashindano hayo ya AFC U23 Championship yatafanyika kati ya Januari 8 na 26 nchini Thailand. Washindi wa makundi 11 pamoja na timu bora nne zilioibuka mshindi wa pili zimejikatia tiketi ya kushiriki michuano hiyo ya Januari 2020. Timu zitakazofuzu Thailand, zitajipatia nafasi ya kushiriki Mashindano ya Olimpiki kati ya Julai na Agosti mwaka ujao 2020 mjini Tokyo nchini Japan.
Debi la Sarkhobi; Persepolis yainyuka Esteqlal 1-0
Watani wa jadi wa soka hapa nchini, klabu ya Esteqlal na Persepolis kwa mara nyingine tena zilishuka dimbani siku ya Jumamosi kuvaana katika mchuano wa kusisimua, ambao wadadidi wa spoti wanasema ni kuamua timu itakayobeba taji la Ligi Kuu ya Soka ya Iran.
Katika debi hilo la 89, Wekundu wa Tehran walipata ushindi hafifu wa bao 1-0, na kujihakikishia alama tatu za kuifanya isalie kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Soka nchini. Kwa sasa Persepolis inaongoza kwa alama 48, ikifuatiwa na Teraktor Sazi yenye alama 46. Kwa kichapo cha Jumamosi The Blues ya Tehran haina budi kutosheka na nafasi ya tatu ikiwa na alama 43.
Voliboli; Klabu Bingwa Afrika
Timu ya wanawake ya voliboli Pipeline kutoka Kenya imejipatia medali ya shaba katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kuichabanga GS Patrollers ya Algeria kwa seti 3-0 jijini Cairo nchini Misri. Wanadada hao wa Kenya, ambao ndio timu ya pekee kutoka Kenya iliyofika robo fainali mwaka huu, walisherekea ushindi huo baada ya kutwaa medali hiyo waliyovuna kwa kuisagasaga Petroliers kwa alama 25-22, 25-17, 25-18 katika mechi ya kusisimua ya kutafuta mshindi wa tatu. Licha ya kutinga robo fainali, klabu nyingine ya Kenya Prisons ilishindwa kusonga hatua ya robo fainali, pamoja na KCB ambayo iliumizwa na Carthage ya Tunisia.
Amnesty yasema Bahrain inatumia mashindano ya magari kujikosha
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema Bahrain inaendelea kutumia mashindano ya magari ya Langalanga maarufu kama Formula 1 kwa ajili ya kujikosha. Samah Hadid, Mkurugenzi wa Amnesty katika eneo la Asia Magharibi aliyasema hayo siku ya Alkhamisi na kuongeza kuwa, utawala wa Manama unaokandamiza wananchi unataka kutumia mashindano yajayo ya Formula 1 (F1) kujaribu kusafisha sura yake iliyochafuliwa na rekodi mbaya ya kukanyaga haki za binadamu. Mashindano hayo yanatazamiwa kufanyika kati ya Ijumaa ijayo hadi Jumatatu katika mji mkuu Manama. Amebainisha kuwa, "Badala ya kujikosha, serikali ya Bahrain inapaswa kutazama upya sheria zinazopiga marufuku uhuru wa kujieleza sambamba na kuanzisha mchakato wa kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa." Mkurugenzi wa Amnesty International katika eneo la Asia Magharibi ameongeza kuwa, "Nyuma ya shamrashamra za F1, kuna upande wa pili wa kutisha nchini Bahrain. Dola ni kandamizi na yeyote anayeikosoa serikali hata kwenye Twitter tu, anafungwa jela."
Siku ya Jumatano, wanaharakati wa haki za binadamu wakiwemo maafisa wa Human Rights Watch na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafanyakazi, walisema ni kichekesho jamii ya kimataifa kuruhusu mashindano hayo ya kimataifa ya Grand Prix Formula One kufanyika nchini Bahrain, katika hali ambayo utawala wa Aal-Khalifa unaendelea kuwakandamiza wananchi. Aprili mwaka jana, maafisa usalama wa Bahrain waliwashambulia wananchi waliokuwa wamemininika mabarabarani kushiriki maandamano ya kupinga kufanyika nchini humo mashindano hayo ya magari ya Formula 1, ambayo yamekuwa yakifanyika nchini humo tangu mwaka 2004, isipokuwa mwaka 2011. Waandamanaji kadhaa walijeruhiwa na wengine wengi kutiwa mbaroni. Tarehe 14 Februari mwaka 2011 wananchi wa Bahrain walianzisha vuguvugu la mapambano kwa kufanya maandamano ya amani dhidi ya utawala dhalimu na kandamizi wa Aal Khalifa.
Dondoo za Hapa na Pale
Shirikisho la soka Afrika CAF limeweka wazi kuwa kuanzia hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON 2019, wataanza kutumia teknolojia ya video za usaidizi kwa waamuzi VAR (Video Assistant Referee) katika kutolea maamuzi katika game zote za 16 bora. Baada ya kumalizika kwa michezo ya kuwania kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika 2019 (AFCON 2019) zitakazofanyika nchini Misri, kuelekea michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi kuanzia June 19 2019, kwa mara ya kwanza mwaka huu ndio itatumika VAR. Pamoja na kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiipinga teknolojia hiyo kuwa inapoozesha mchezo wakati wa fainali za Kombe la Dunia 2018 zilizofanyika Urusi, imeonekana kuzidi kutawala baada ya kuona inatumika katika AFCON na hata baadhi ya Ligi wameonesha kuikubali, droo ya kupanga makundi ya michuano ya AFCON 2019 itachezeshwa April 12 2019 Cairo Misri.
Kwengineko, azma ya kuwatenga wanariadha wa kike kulingana na viwango vyao homoni za testosterone ni ukiukaji wa haki kimataifa za biadamu limesema baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa. Mshindi wa mbio za Olimpiki mita 800 Caster Semenya, mwenye umri wa miaka 28 raia wa Afrika Kusini, anapinga nia ya Shirikisho la kimataifa la Riadha (IAAF) juu ya mpango kuweka masharti ya viwango vya testosterone miongoni mwa wanariadha wa kike. Umoja wa Mataifa umeitaja mipango hiyo kama isiyo na umuhimu, ya udhalilishaji na yenye madhara. Chini ya sheria za IAAF, mwanariadha wa kike mwenye viwango asilia vya juu vya homoni za testosterone anatakiwa kukimbia na wanaume au kushiriki mashindano ya watu waliobadilishwa mpaka apate tiba ya kupunguza viwango hivyo.
Na klabu ya Manchester United ya Uingereza baada ya kukaa na kumuangalia katika michezo 19 akiiongoza timu yao Ole Gunnar Solskjaer kama kocha wao wa muda, wameamua kumtangaza rasmi kuwa kocha wao mkuu wa kudumu. Man United imeamua kumpa mkataba wa miaka mitatu Ole Gunnar Solskjaer kama kocha wao wa kudumu, awali Man United ilikuwa imemteua Ole Gunnar Solskjaer kama kocha wao wa muda kumrithi Jose Mourinho hadi mwisho wa msimu huu. Solskjaer akiwa na Man United sasa amefanikiwa kuiongoza club hiyo katika michezo 19, amefanikiwa kushinda michezo 14, sare michezo miwili na amepoteza michezo mitatu, kama utakuwa unakumbuka vizuri Ole Gunnar Solskjaer aliwahi kuwa mchezaji wa Man United katika kipindi cha miaka 11 (1996-2007).
..........................TAMATI....................