Jumatano, tarehe 17 Aprili, 2019
Leo ni Jumatano tarehe 11 Sha'aban 1440, Hijiria, sawa na tarehe 17 Aprili 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1407 iliyopita, alizaliwa mtukufu Ali bin Hussein, maarufu kwa jina la Ali Akbar, mwana mkubwa wa kiume wa Imam Hussein (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) mjini Madina. Ali bin Hussein ambaye alifanana sana na babu yake Mtume Mtukufu (saw), alinufaika sana na bahari ya maadili mema na mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuwa pamoja na babu yake Imam Ali (as) na baba yake Imam Hussein (as). Mtukufu Ali bin Hussein, alikuwa maarufu kwa jina la Ali Akbar yaani Ali mkubwa kutokana na jina lake kufanana na majina ya mdogo wake ambaye pia alikuwa na jina hilo la Ali. Ali Akbar alikuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya baba yake dhidi ya dhulma na uasi wa utawala wa Bani Umayyah. Aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria baada ya kuingia katika medani ya vita na kupigana kishujaa katika mapambano ya jeshi la Yazid bin Muawiyah na Imam Hussein (as) na wafuasi wake.
Siku kama ya leo miaka 911 iliyopita alifariki dunia, Sanai Ghaznawi Hakim Abul-Majd Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran mjini Ghaznen. Alizaliwa mwaka 467 Hijiria, na akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi ambapo pia ndani yake ameweka wazi fikra za kiakhlaqi na irfani za malenga. Aidha vitabu vya 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi.
Katika siku kama ya leo miaka 370 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Shaaban 1070 Hijria, Mohammad Taqi Majlisi maarufu kama Majlisi wa Kwanza, msomi na Arif mkubwa Muirani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1003 Hijria Qamari katika mji wa Isfahan ambao zama hizo ulikuwa mji mkuu wa silsila ya watawala wa Safavi. Alizaliwa wakati Iran ilikuwa inashuhudia ustawi mkubwa wa kiutamaduni na kielimu. Familia ya Allamah Majlisi ilikuwa ya wasomi na wanazuoni kiasi kwamba alipata sehemu ya masomo yake kutoka kwa baba yake na jamaa zake wengine katika familia. Baada ya kujifunza fiqhi, itikadi na tafsiri katika darasa la Sheikh Bahai, alipata umashuhuri kama alim na arif mkubwa. Alikwea daraja la juu la masomo baada ya kutembelea mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq. Baada ya kurejea Isfahan alijishughulisha kufunza na kutambulika kwa umahiri wake katika fiqhi, hadithi, tafsiri na itikadi.
Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani, mmoja wa maulama wachaji-Mungu wakubwa na mwanamapambano. Alizaliwa mwaka 1262 Hijiri mjini Isfahan, Iran. Baba na babu yake, walikuwa kati ya maulama wakubwa wa eneo ambapo naye pia alipata kusoma kutoka kwao elimu mbalimbali. Baada ya Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani kusoma baadhi ya masomo ya kidini kutoka kwa baba yake (yaani Muhammad Baqir Agha Najafi) alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo mjini hapo. Miaka mitano baadaye alirejea mjini Isfahan na kuwa mmoja wa maraajii wakubwa wa mji huo. Aidha mbali na masuala ya kidini, Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani alikuwa mwanaharakati mzuri wa masuala ya kisiasa. Katika uwanja huo, msomi huyo alipambana vikali na upotoshaji wa kifikra na kiutamaduni na kadhalika ufisadi wa watawala dhalimu wa wakati huo. Wakati huo huo aliongoza harakati za kimapambano dhidi ya ukoloni wa kigeni hususan Uingereza. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Fiqhul-Imaamiyyah' 'Bahth Fii Wilaayati Haakimul-Faqih' na 'Dalaailul-Ahkam.'
Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, sawa na tarehe 17 Aprili 1915, kwa mara ya kwanza kabisa duniani ilitumiwa gesi ya kubana pumzi ya wanadamu vitani. Hatua hiyo ya kinyama ilichukuliwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Ujerumani ilitumia gesi hiyo ya kubana pumzi dhidi ya askari wa Uingereza na Ufaransa na kuua askari wengi wa vikosi vya waitifaki. Wajerumani walipata ushindi katika vita hivyo vilivyokuwa mashuhuri kwa jina la Vita vya Gesi.
Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, raia wa Scotland kwa jina la John Logie Baird, alifanikiwa kuvumbua televisheni ambayo hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa katika upashaji habari duniani. Baird alikuwa mmoja wa wavumbuzi wakubwa wa enzi zake. Baada ya hapo mtu wa kwanza kutengeneza televisheni iliyoimarika zaidi alikuwa ni Giovanni Caselli, raia wa Italia ambaye mnamo mwaka 1862 alifanikiwa kutengeza chombo ambacho kwa kutumia mfumo wa telegrafi kiliweza kutoa ramani na picha. Televisheni ya kwanza ambayo ilionyesha vizuri picha, ilianza kutumika tarehe 17 mwezi Aprili mwaka 1926 kwa ajili ya klabu ya kifalme nchini Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Aprili 1946, Syria ilijipatia uhuru wake kutoka kwa askari wa kigeni waliokuwa wakiitawala nchi hiyo. Syria na baadhi ya ardhi zinazoizunguka awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Sham, na kabla ya kudhihiri dini tukufu ya Uislamu ilikuwa chini ya udhibiti wa Iran, Ugiriki, Misri na Roma. Ardhi hiyo ilikuwa makao ya utawala wa Ugiriki na baada ya kukaliwa kwa mabavu na Misri, baadaye ilichukuliwa na utawala wa Othmaniya. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya kuporomoka utawala wa Othmaniya, Syria ilikoloniwa na Ufaransa. Kufikia Juni 1941, wakati wa vita vya pili vya dunia, askari wa Uingereza na Ufaransa waliikalia kwa mabavu nchi hiyo, hadi kufikia mwaka 1946 wakati ilipojipatia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, mwafaka na tarehe 17 Aprili 2004, vifaru vya utawala wa Kizayuni wa Israel vilishambulia gari lililokuwa limembeba Dakta Abdulaziz Rantisi, mwanaharakati wa Palestina na kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, na kumuuwa shahidi. Dakta Rantisi alichaguliwa kuiongoza harakati ya Hamas baada ya kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwasisi na kiongozi wa harakati hiyo. Rantisi alizaliwa mwaka 1964 katika mji wa Yafa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na alihitimu elimu ya tiba kama daktari katika chuo kikuu cha Alexandria nchini Misri.