May 25, 2019 02:22 UTC
  • Jumamosi, 25 Mei, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 19 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka 1440 Hijria sawa na tarehe 25 Mei mwaka 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1400 iliyopita mwaka 40 Hijria Qamaria, Imam Ali bin Abi Talib AS ambaye ni mkwe, binamu na shakhsia wa karibu kwa Mtume Mtukufu SAW, alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya akiwa anaswali swala ya alfajiri katika msikiti wa mji wa Kufa na mtu aliyeitwa Abdur Rahman bin Muljim Muradi. Imam Ali A.S alikufa shahidi baada ya siku 3. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili baada ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW ambaye anaelezwa na historia ya Uislamu kuwa shujaa, mwenye imani, akhlaki njema, elimu na uadilifu. Alipata elimu na mafunzo kutoka nyumba ya Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanamume wa kwanza baada ya Mtume SAW kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali AS alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume SAW katika hali zote za shida na matatizo na hata kuhatarisha maisha yake ili kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu huku akionyesha ushujaa mkubwa katika vita mbalimbali vya haki dhidi ya batili. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali AS alikuwa mpole na mwenye upendo. Kiasi ambacho moyo wake ulikuwa wenye kuathirika sana na kujawa na huruma kwa kuona machozi ya mtoto yatima. Imam Ali AS alipenda haki na uadilifu na kupambana vilivyo na dhulma katika kila njanya. Katika sehemu ya matamshi yake yenye hekima Imam Ali AS anasema: 'Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake siku ya Kiama hali ya kuwa nimewadhulumu waja wake.'

 

Siku kama ya leo, miaka 659 iliyopita, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1360:

Kundi la mabaharia wa Kifraransa lilifika katika Ghuba ya Guinea. Ghuba ya Guinea inapatikana magharaibi mwa bara la Afrika katika bahari ya Atlantiki. Baada ya muda kupita tangu kundi hilo kufika katika Ghuba ya Guinea, ushawishi wa Ufaransa ndani ya bara hilo ulianza, na taratibu ikaanza kuidhibiti ardhi iliyokuja kujulikana baadaye kama Guinea. Nchi ya Guinea iliendesha harakati za mapambano ya miaka mingi hadi ikafanikiwa kupata uhuru wake mwaka 1958. Guinea ina eneo lenye ukubwa wa kilomitamraba zaidi ya 245,000 na inapakana na nchi za Senegal, Guinea Bissau, Mali, Ivory Coast, Liberia na Sierra Leone. 

 

Tarehe 4 Khordad kwa mujibu wa kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya Hijria Shamsia imepewa jina la Siku ya Uhimilivu wa Dezful, ambao ni moja ya miji ya kusini mwa Iran. Sababu ya siku hii kupewa jina hilo ni muqawama na ungangari wa watu wa Dezful kukabiliana na hujuma na mashambulio ya makombora ya utawala wa Kibaathi wa Iraq wakati wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Wakati vilipoanza vita hivyo vya Kujihami Kutakatifu, mji wa Dezful ulishambuliwa kwa makombora zaidi ya 200 na kwa risasi zaidi ya elfu ishirini mpaka ukajulikana kwa jina la mji wa makombora. Pamoja na yote hayo wananchi katika mji huo waliendelea kuonyesha muqawama na uhimilivu kiasi kwamba hata katika mazingira hayo Sala ya Ijumaa iliendelea kusaliwa kila wiki kwa kuhudhuriwa na wananchi na wapiganaji waliokuwa kwenye medani za vita.

 

Na Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1963: Hati ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ilisainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 32 za bara hilo. Marais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Kwame Nkrumah wa Ghana na Ahmed Sekou Toure wa Guinea walikuwa miongoni mwa waasisi wa jumuiya hiyo. Jumuiya ya OAU ilielekeza jitihada zake katika kuleta umoja kati ya nchi za Afrika, kutatua hitilafu kati ya nchi hizo, kutetea haki ya kujitawala ya nchi wanachama na ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika zilizokuwa zingali zinakoloniwa. Mnamo mwezi Julai mwaka 2002, viongozi wa nchi wanachama wa OAU walifanya kikao nchini Afrika Kusini na kuamua kubadilisha jina la jumuiya hiyo kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) sambamba na kuanzisha taasisi kadhaa kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya umoja huo na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama. Hivi sasa Umoja wa Afrika una nchi 54 wanachama. Makao Makuu ya umoja huo yako Addis Ababa, Ethiopia na kikao cha viongozi wa nchi wanachama hufanyika kila mwaka katika moja ya nchi hizo.