Ulimwengu wa Michezo, Juni 17
Mkusanyiko wa matukio ya spoti kitaifa na kimataifa ndani ya siku saba zilizopita...
Iran yahifadhi ubingwa wa voliboli ya walemavu Asia
Timu ya taifa ya voliboli ya kuketi chini ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imehifadhi taji la mashindano ya walemavu katika mchezo huo barani Asia. Hii ni baada ya kuisasambua China seti 3 za 25-21, 25-7, na 28-26 katika fainali ya mashindano hayo yanayofahamika kama ParaVolley Asia Oceania Sitting Volleyball Championship, iliyopigwa katika Ukumbi wa Michezo wa Huamark katika mji mkuu Thailand, Bangkok siku ya Jumamosi.
Iran ilitinga fainali baada ya kuzigaragaza Japan, Cambodia, Thailand, Kazakhstan, na Korea Kusini katika michuano yake ya awali. Mashindano hayo yalianza Juni 10 hadi Juni 15. Iran ilijikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Paralimpiki ya Tokyo Mwaka 2020, baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya ParaVolley Asia Oceania Sitting Volleyball Championship mwaka jana 2018.
Voliboli: Iran yaziadhibu Poland na Russia
Timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendeleza ubabe wake katika Wiki ya Tatu ya Mashindano ya Ligi ya Mataifa ya mchezo huo mjini Oroumiyeh, katika mkoa wa Azarbaija Magharibi. Timu hiyo ya wanaume ya Iran siku ya Jumapili iliipa kichapo cha mbwa Russia, kwa kuizaba seti 3 kwa mtungi, za 25-20, 26-24 na 25-23 katika mchezo uliochezwa katika Ukumbi wa Michezo wa Ghadir. Mchezaji Amir Ghafour ndiye aliongoza kwa kuifungia Iran pointi nyingi.
Kabla ya hapo, siku ya Jumamosi Iran iliikung'uta Poland seti 3-2 za (25-20, 21-25, 18-25, 25-17, 15-8). Mfululizo huo wa ushindi unaifanya timu hiyo ya Iran isalie kileleni mwa kundi lake. Ushindi huo uliwamimina mashabiki wa timu hiyo mabarabarani, wakishangilia kwa mahoni na vuvuzela.
Mashindano haya yanaofahamika kama Volleyball Men's Nations League yanayosimamiwa na Shirikisho la Voliboli Duniani FIVB, yalianza Mei na yatamalizika mwezi ujao wa Julai. Duru ya mwisho ya mashindano haya yatafanyika katika Ukumbi wa Credit Union 1 Arena mjini Chicago nchini Marekani.
Tanzania yalimwa na Misri mchuano wa kirafiki
Timu ya taifa ya soka ya Tanzania almaarufu Taifa Stars usiku wa kuamkia Ijumaa walitandikwa bao moja la uchungu bila jibu, waliposhuka dimbani kuvaana na Misri katika mchuano wa kirafiki. Licha ya kichapo hicho, lakini wachezaji wa Taifa walionyesha kiwango bora cha soka mbele ya miamba hiyo ya soka barani Afrika. Mchuano huo ulpigwa katika Uwanja wa Burj al Arab uliopo kwenye mji wa Alexandria.
Tanzania ikiwa ugenini katika mchezo huo wa kirafiki wamekubali kupoteza kwa goli 1-0, goli ambalo lilifungwa na Ahmed Mohammad dakika ya 65 ya mchezo huo.
Licha ya juhudi za washambuliaji wa Taifa Stars wakiongozwa na nahodha wao Mbwana Samatta hawakufanikiwa kusawazisha. Kocha Mkuu wa Stars, Emmanuel Amunike amesema kiwango hicho kilikuwa kipimo sahihi kwake na kwa vijana wake na amegundua kasoro za kuzifanyia kazi, kauli ambayo inaungwa mkono na Mbwana Samatta.
Taifa Stars ipo nchini Misri ikijiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) itakayong'oa nanga siku chache zijazo. Nayo timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars ambayo imekwishatangaza kikosi chake, ilicheza mchuano wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuambulia sare ya bao 1-1. Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki ulipigwa katika Uwanja wa Santa Ana Calle mjini Madrid nchini Uhispania.
Kenya ambayo ipo Kundi C pamoja na timu za Tanzania, Algeria na Senegal itaelekea Misri Jumatano, siku tano kabla ya mchuano wake wa ufunguzi wa Afcon dhidi ya Senegal. Michuano hiyo ya Afcon inatazamiwa kung'oa nanga tarehe 21 mwezi huu hadi Julai 19.
Dondoo za Hapa na Pale
Timu ya taifa ya Ureno wamekuwa mabingwa mara mbili kwenye mashindano ya UEFA National League baada ya kuisasambua goli 1-0 Uholanzi kwenye mchezo wa fainali. Goli la Goncalo Guedes katika kipindi cha pili lilitosha kuipa Ureno ushindi wa bao 1-0 mjini Porto. Guedes anayekipiga na klabu ya Valencia ya Uhispania, alifunga kwa kupiga shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Uholanzi Jasper Cillessen. Ureno wamekuwa mabingwa mara mbili katika mashindano manne yaliyopita waliyoshiriki.
Kwengineko, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye amesema mashindano ya Kagame Cup 2019 yataendelea licha ya kutokuwapo Simba na Yanga. Ameiponda Yanga na kuitaja kuwa ni timu isiyo na msaada, ndio sababu hufungwa mabao 5-0 au 6-0 kwenye mashindano ya kimataifa. Mashindano hayo ya timu 16 yatafanyika Julai 17-21. Klabu ya Yanga imesema haitoshiriki michuano ya Kagame Cup jijini Kigali, Rwanda kwa sababu, wachezaji wengi wamemaliza mikataba, wengine wapo na timu ya taifa, na waliobaki wapo mapumziko. Wakati hayo yakijiri, tayari Simba SC ilishatangaza kuwa haitoshiriki mashindano hayo, kutokana na ratiba ya mashindano hayo kuingiliana na ratiba ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi ya Bingwa AFRIKA (CAFCL) na Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (TPL).
Na kwa kutamatisha, klabu ya Yanga ya Tanzania siku ya Jumamosi ilivuna mengi mazuri katika kikao cha kuchangisha na kujadili mustakabali wa timu hiyo ya soka. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, huku mgeni wa heshima akiwa rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete. Aidha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mama Fatma Karume walishiriki kikao hicho na kutoa mchango wao wa hali na mali.
………………….TAMATI…………..