Jun 23, 2019 17:52 UTC
  • Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-17

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 17 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia sisitizo la Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini (MA) kuhusiana na uhuru wa wanawake kuwa ni moja ya masuala muhimu yaliyopewa kipaumbele na mtukufu huyo.

Ndugu wasikilizaji katika fasihi ya siasa za dunia vyama na makundi ya kisiasa yanatajwa kuwa mhimili unaoendesha demokrasia. Kwa ibara nyingine ni kwamba, mhimili wa demokrasia unahitajia msaada wa vyama vya kisiasa kuelekea kwenye harakati yake, ambapo mahusiano ya kisiasa nayo huwa ni moja ya masuala muhimu ya mifumo ya demokrasia. Kwa imani ya weledi wengi wa masuala ya kisiasa, vyama na mirengo ya kisiasa na kiraia ni moja ya nembo muhimu za mifumo ya kidemokrasia, kwa kuwa vinahesabika kuwa jukwaa kuu la kudhihirishwa uhuru wa kujieleza na ushiriki wa kisiasa. Katika mifumo hiyo vyama huwa vina mpaka wa kati katika mfumo wa kisiasa unaotawala ambapo raia hupata njia ya kuwasilisha matakwa yao. Moja ya sifa za pamoja za vyama na makundi ya kisiasa, ni kufanya juhudi kwa ajili ya kufikia madaraka kupitia njia za amani na kisheria na pia kupanga mikakati kwa ajili ya kulinda madaraka hayo kupitia sheria, ili kuweza kutekeleza siasa na mipiangilio inayolenga kwenye ustawi na maendeleo. Licha ya kwamba katika baadhi ya nchi na kutokana na kuwa na dosari mfumo unaotawala au udhaifu wa utamaduni wa kisiasa wa ushirika, vyama vya kisiasa huwa vinajitenga mbali na shughuli zao nyingi za msingi.

Siasa nchini Iran zinaendeshwa kwa namna bora kabisa kwa kuzingatia misingi ya demokrasia halisi

 

Hata hivyo katika muundo wa fasihi ya kisiasa masuala yanayotegemea demokrasia, huwa na mapokezi chanya kwa mnasaba wa nafasi ya vyama na mirengo ya kisiasa katika kuinua kiwango cha ustawi wa kisiasa ndani ya jamii husika. Katika uwanja huo kufikia ustawi na maendeleo ya jamii na hata kuendelea uthabiti wa kimfumo, ni mambo ambayo yana umuhimu mkubwa.

*******

Uanzilishi wa vyama na mirengo ya kisiasa nchini Iran ni wenye historia ya zaidi ya karne moja. Ukweli ni kwamba, baada ya kufikiwa ushindi wa mapinduzi ya katiba dhidi ya mfumo wa kidikteta uliokuwa ukitawala nchi hii, kulianza mazingira ya ustawi wa kisiasa nchini Iran na moja ya matokeo yake ilikuwa ni kuundwa vyama vya kisiasa. Kwa kuzingatia kuwa vyama vya kisiasa nchini Iran ni vyenye historia ndefu, lakini vyama na mirengo ya kisiasa haikuwa na hali nzuri katika mfumo wa kisiasa uliokuwepo huko nyuma, hadi kufikia kipindi cha kujiri Mapinduzi ya Kiislamu. Mifumo ya kidikteta ya kisiasa, kujikita na kupinga serikali sambamba na kugawanywa madaraka ya kisiasa, kukosa tajriba nzuri ya ushiriki wa kisiasa wa wananchi na kadhalika kuundwa kwa vyama vya kikatiba na serikali ya kimuundo, ni miongoni mwa mambo yaliyovifanya vyama vya kisiasa kutoingia katika ulingo huo kabla ya ushindi ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Shah kushoto, alikandamiza wapinzani kwa msaada wa Wamagharibi waliokuwa wakimlinda

 

Hata hivyo mambo mawili ya upenyaji na uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi tofauti kwa namna ya jumla na pia vyama vya kisiasa kwa namna maalumu na kadhalika hali ya vyama vya kisiasa katika nchi zisizostawi ikiwemo Iran, ambazo kiujumla vyama vyake vya kisiasa vilikuwa vina matatizo mengi kutokana na kufuata mfumo wa vyama vya nchi za Magharibi yanapaswa kuongezwa kwenye orodha hiyo. Kiujumla tunaweza kusema kuwa hali ya vyama vya siasa nchini Iran kabla ya Mapinduzi ilikuwa ikiiga nchi za Magharibi hususan kuhusiana na suala la kiwango cha uhuru wa kisiasa wa wananchi na makundi ya kisiasa na pia kiwango cha kujitawala nchi. Hali hiyo iliyoathiriwa moja kwa moja na uingiliaji wa kigeni, haikuwa nzuri kiujumla.

**********

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 17 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ndugu wasikilizaji, Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni nukta ya kuvutia katika historia ya mabadiliko ya kisiasa na kijamii nchini hapa, na hususan hali ya vyama na mirengo ya kisiasa. Imam Khomeini (MA) kama Kiongozi wa mwamko wa mapinduzi ya wananchi dhidi ya udikteta katika miaka yote ya mapambano hayo alikuwa akisisitizia umuhimu wa kuundwa vyama na mirengo ya kisiasa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi. Mtukufu huyo alikuwa akikosoa ukandamizaji wa kipindi cha utawala wa kidikteta wa kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha sambamba na kufichua hali ya vyama vya kimaonyesho na serikali za kibaraka katika kipindi cha udikteta wa kifalme, alifanya juhudi kuweka wazi njama za wakoloni za kuzitumia vibaya ili kuibua tofauti kati ya wananchi. Huku akikosoa maonyesho ya kikatuni ya demokrasia katika kipindi cha ukandamizaji wa utawala wa kidikteta,  aliyataka matabaka ya wananchi kuwa na tahadhari katika kushirikiana na vyama vya kimaonyesho na amri za Shah kama vile chama cha Ufufuo.

Shah alipoingizwa madarakani na Wamagharibi

 

Inafaa kukumbusha kuwa, chama cha Ufufuo ni miongoni mwa vyama ambavyo mwishoni mwa miaka ya kumalizika kwa utawala wa Shah nchini hapa, kilianzishwa na serikali kwa ajili ya kufanya maonyesho bandia ya kidemokrasia ambapo wakati huo Shah mwenyewe aliwataka wananchi wote kujiunga na chama hicho la  hivyo walitakiwa wahame nchi. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifungua aga wa harakati za vyama na makundi ya kisiasa na hata kwa vyama ambavyo kwa mtazamo wa kiitikadi vilikuwa vikikabiliana kikamilifu na idolojia ya Kiislamu. Mwenendo wa kisiasa wa Imam Khomeini (MA) katika miaka ya utawala wake, ulionyesha kwamba binafsi alikuwa akiunga mkono harakati za vyama vya kisiasa maadamu tu vizingatie misingi ya sheria na kulinda usalama katika shughuli zao.

******

Katika kubainisha mwelekeo wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusiana na shughuli za vyama na mirengo ya kisiasa, Imam Khomeini aliilinganisha nafasi ya vyama vya siasa na kiwango cha uhuru wao katika miaka ya mwanzoni mwa ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu na mapinduzi mengine yaliyowahi kutokea duniani kwa kusema: "Hakuna mapinduzi kama ya Iran ambapo baada tu ya ushindi kulifunguliwa njia na shughuli za vyama na makundi yote kwa uhuru." Hotuba ya tarehe 30/5/1362. Aidha tangu mwanzoni mwa mwamko wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa, yaani mwaka 1342 Shamsia sawa na 1963 Miladia, moja ya ukosoaji wake kwa utawala wa Shah, ulihusiana na hali ya vyama vya kisiasa na hali ya mgawanyiko wa kisiasa katika kipindi kile. Sambamba na kukosoa nafasi ya serikali katika kuunda vyama bandia vya siasa na vya kimaonyesho kwa ajili ya kuwavutia wananchi kujiunga na vyama hivyo Imam alisema: "Serikali mbalimbali zinakuja na kuondoka na kila serikali inayokuja huwa inaunda chama. …Kiujumla nchini Iran chama hakina maana. Serikali haitambui chama….wanachokitaka tu ni kuwakusanya watu katika maeneo ili wapige nara za kuwaunga mkono....Katika nchi ambazo vyama hupewa umuhimu, serikali huundwa kutokana na vyama na sio serikali kuundwa kwanza na kisha vyama kuundwa baadaye." Hotuba ya tarehe 18/6/1343.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 17 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini. 

 

 

Tags