Ulimwengu wa Michezo, Jul 8
Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kuanzia Michuano ya AFCON hadi fainali ya Kombe la Dunia kwa Wanawake....
Iran yatwaa ubingwa wa mieleka ya Greco-Roman
Timu ya mieleka aina ya Greco Roman ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Ubingwa wa Makurutu ya Asia mwaka huu 2019, katika mji wa Nur-Sultan nchini Kazakhstan. Iran ilitwaa taji taji hilo siku ya Ijumaa, baada ya kuzoa alama 181, huku ikitwaa medali nne za dhahabu, mbili za fedha na shaba moja. Wanamichezo waliotwalia Iran dhahabu katika kategoria tofauti ni Amir Reza Dehbozorgi (48kg), Saeid Esmaeili (51kg), Saeid Karimizadeh (92kg) na Hojjat Rezaei (65kg). Kwa kila medali ya dhahabu waliyoshinda, wimbo wa taifa wa Iran ulihinikiza katika ukumbi wa michezo wa Nur-Sultan.

Nishani za fedha za Iran zilitiwa kibindoni na Danial Sohrabi katika safu ya wanamieleka wenye kilo 60 na Reza Saki kilo 71, huku Shahrokh Mikaeilizadeh akiipa Iran shaba katika kategoria ya wanamieleka wenye kilo 110. Mwenyeji Kazakhstan imeibuka wa pili huku nafasi ya tatu ikitwaliwa na India. Siku ya Jumamosi, Iran ilianza vyema pia mashindano ya mieleka mtindo wa Free-Style, na hadi tunaenda mitamboni, Amir Hossein Motaghi na Amir Hossein Firouz Pour walikuwa washainyakulia Iran medali za dhahabu.
Tetesi za Soka
Klabu ya soka ya Esteghlal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inammezea mate mshambuliaji wa Mali, Cheick Tidiane Diabaté na yumkini ikimsajili kujiunga na timu hiyo karibuni hivi. The Blues ya Tehran inataka kuimarisha safu yake ya mbele, na ndiposa inataka kumsajili raia huyo wa Mali mwenye umri wa miaka 32. Diabate alianza safari yake ya kandanda nchini Ufaransa kwa kuichezea klabu ya Bordeaux, kabla ya kujiunga na Ajaccio, Nancy na Metz.

Januari mwaka jana, mchezaji huyo nyota alijiunga na klabu ya Benevento ya Serie A kwa mkopo. Katika mechi 39 alizoichezea timu yake ya taifa, Diabate alifanikiwa kucheka na nyavu mara 15.
Michuano ya Afcon
Timu ya taifa ya soka ya Afrika Kusini siku ya Jumamosi ilipata ushindi muhimu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Afcon inayoendelea nchini Misri, baada ya kuwacharaza wenyeji Mafarao bao 1 bila jibu. Katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Bafana Bafana walikabiliana vikali na Waarabu na nusra mchezo huo uishie kwa sare tasa katika dakika 90 za ada. Hata hivyo Thembinkosi Lorch alifyatua kombora kunako dakika ya 85 ambalo lilimuacha taabani kipa wa Misri, Mohamed Elshenawy.

Afrika Kusini sasa watapambana na Nigeria katika mchezo wa robo fainali. The Green Eagles wa Nigeria wametinga robo fainali baada ya kuwabandua nje ya mashindano mabingwa watetezi Cameroon katika mchezo wa Jumamosi. Kutokana na kichapo hicho cha Jumamosi, Hani Abou Rida, Rais wa Shirikisho la Soka Misri ametangaza kujiuzulu. Rida ambaye ameliongoza shirikisho hilo tokea mwaka 2016, amesema kujiuzulu kwake ni sehemu ya kubebea dhima ya kuondolewa Misri nje ya Afcon mapema. Rida amejizulu sambamba na kumpiga kalamu nyekundu kocha mkuu wa timu hiyo Javier Aguirre ambaye mkataba wake ulipaswa kuisha mwaka 2022. Rida kwa sasa ambaye ni mjumbe wa CAF na FIFA ametangaza kuendelea na nafasi moja tu ya kamati ya maandalizi ya michuano hiyo hadi pale itakapo malizika. Wadadidi wa masuala ya spoti wanasemaje kuhusiana na kichapo hicho dhidi ya wenyeji Mafarao?
Senegal wamefanikiwa pia kutinga robo fainali ya Afcon baada ya kuitungua Uganda bao 1-0 kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora. Sadio Mane ambaye pia anakipiga Liverpool aliwapa Senegal bao la uongozi mapema kabisa baada ya kupokea pasi kutoka kwa M’Baye Ning.
Uganda walijitahidi kutaka kusawazisha bao mara kadhaa lakini juhudi zao ziligonga mwamba ikiwemo shuti kali la Emmanuel Okwi lililookolewa na mlinda lango wa Senegal Alfred Gomis. Uganda Cranes ambayo ilianza vyema mashindano haya kwa kuisasambua Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mabao 2-0 mjini Cairo, ilikuwa tumaini pekee la nchi za Afrika Mashariki, baada ya Tanzania na Kenya kuondolewa mapema. Siku ya Jumapili, Madagascar ambayo inashiriki Afcon kwa mara ya kwanza, iligaragarazana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa masikitiko DRC iliondolewa katika michuano hiyo ya Afcon kufuatia kupoteza kwa mikwaju ya penati kwa mabao 4-2. Hii ni baada ya dakika 90 za ada na 30 za nyongeza kumalizika kwa sare ya kufungana magoli 2-2. Ushindi huu unaifanya Madagascar iendelee kusonga mbele kimiujiza.
Haya yanaarifiwa huku Rais wa klabu ya TP Mazembe ya Kongo DR, Moise Katumbi akikanusha vikali tuhuma za gazeti moja la Madagascar kwamba alimhonga kipa wa Zimbabwe kwenye mechi ya Afcon kuwania kufuzu 16 Bora dhidi ya DR Congo. DR Congo inayonolewa na Mwinyi Zahera ilishinda mabao 4-0 kwenye mchezo huo na kufuzu jambo ambalo liliibua mijadala mingi. Kupitia ujumbe wake kwenye Twitter yake, Katumbi amesisitiza madai hayo ni ya hovyo na kwamba hata siku mechi hiyo inachezwa hakuwepo Misri alisharudi zake Congo.

Mbali na hayo, bingwa mtetezi, Cameroon imeyaaga mashindano hayo ya kikanda baada ya kusasambuliwa mabao 3-2 walipovaana na Nigeria jijini Alexandria. Aidha Jumapili Waarabu wa Algeria waliikandamiza Guinea mabao 3-0 katika Uwanja wa Juni 30 jijini Cairo na kujakatia tiketi ya robo fainali. Mabao ya Algeria yalipachikwa wavuni na Bilal Yusuf, Riyad Mahrez na Adam Ounas.
Kombe la Dunia kwa Wanawake
Marekani na Uholanzi siku ya Jumapili zilishuka dimbani kutoana jasho katika mchezo wa aina yake wa fainali ya michuano ya Kombe la Dunia kwa upande wa wanawake nchini Ufaransa. Kama ilivyotarajiwa, Marekani ilimng'aria myonge katika mchuano huo na kumzaba mabao 2-0. Katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Groupama nchini Ufaransa, Megan Rapinoe alipachika wavuni bao la kwanza kupitia mkwaju wa penati katika dakika ya 61. Rose Lavelle aliongeza la pili nane baadaye na kulizamisha jahazi la Waholanzi. Marekani ilitinga fainali baada ya kuichachafya Uingereza mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali mnamo Julai 2, huku Uholanzi ikijikatia tiketi ya fainali baada ya kuiadhibu Sweden bao 1 kwa mtungi katika mchuano mwingine wa nusu fainali Julai 3.
Dondoo za Hapa na Pale
Bingwa wa riadha wa Kenya, Timothy Cheruiyot usiku wa kuamkia Jumamosi alitwaa ubingwa wa mbio za mita 1,500 za IAAF Diamond League mjini Lausanne, nchini Uswisi. Mkenya huyo alikata utepe kwa kutumia saa 3:28.77 na kuibuka kidedea. Mwanariadha huyo wa Kenya alifuatiwa kwa karibu na Jakob Ingebrigtsen of Norway aliyemaliza wa pili kwa kutumia saa 3:30.82. Nafasi za tatu nan ne zilitwaliwa na raia Djibouti Ayanleh Souleiman (3:30.79) na Filip Ingebrigtsen (3:30.82), huku orodha ya tano bora ikifungwa na Mganda Ronald Musagala aliyemaliza kwa kutumia saa 3:31.33.
Na siku ya Jumapili, klabu ya Kariobangi Shark ya Kenya ilipambana kufa kupona na klabu ya Everton ya Uingereza katika Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi na mchuano huo kuishia sare ya bao 1-1 katika dakika za ada. Mchuano huo wa fainali za Kombe la Sportpesa uliingia katika mikwaju ya penati, ambapo Sharks waliwashangaza wengi kwa kutwaa ubingwa. Kariobangi Shark waliitangulia Everton kwa mabao, kupiti goli la Duke Abuya kunako dakika ya 28, bao ambalo liliwanyayua toka vitini mashabiki zaidi ya 50 elfu waliokuwa wamefurika uwanjani hapo.
Kariobangi Sharks wamepata fursa ya kuvaana na Everton baada ya kuisasambua Bandari bao 1-0 jijini Dar es Salaam Tanzania Januari mwaka huu na kutwaa taji la kieneo la SportPesa. Klabu hiyo ya Kenya imeicharaza Everton wakati huu ambapo taifa hilo linaomboleza kifo cha mwanakandanda mahiri wa zama zake, Joe Kadenge aliyekuwa na umri wa miaka 84.

…………………….TAMATI……………….